Ningependa kutoa tahadhari hasa kwa Wastaafu au wanaotarajia kustaafu,
Idara, Wizara zote zinazoshughulika na wastaafu, Wakurugenzi wa Manispaa na
Halmashauri kujihadhari na watu wanaowapigia simu na kujitambulisha kuwa wao ni
watumishi wa Mashirika ya Hifadhi za Jamii na Idara zingine za Serikali na
kwamba wanashughulika na mafao ya wastaafu.
Ninatoa tahadhari hiyo kwa sababu kwa kushirikiana na LAPF tumefanikiwa
kumkamata mtu mmoja kwa jina la DAVID MAGESA MAKALI @ PETER MABULA na
kumfikisha Mahakamani baada ya kujifanya ni mtumishi wa TAMISEMI, LAPF, PSPF na
OFISI YA KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA na kufanikiwa kuwaibiwa fedha kwa njia ya
mtandao wastaafu kutoka katika mikoa mbalimbali.
Wanachofanya watu hao wanapiga simu Idara mbalimbali na kujifanya wapo
TAMISEMI au Wizara nyingine na kuwataka wawatumie orodha ya wastaafu wa mwaka
fulani pamoja na namba zao za simu. Inaonyeha kwa njia hiyo wameweza kupata orodha
ya wastaafu takriban kutoka katika Mikoa 15 hususan kutoka Idara ya afya.
Wakishapata orodha ya majina ya wastaafu na namba zao za simu humpigia mstaafu
na kujitambulisha anatokea Wizarani na anashughulikia wastaafu ambao inaonekana
walipunjwa kwenye mafao yao na inaonyesha naye amepunjwa kiasi cha milioni
fulani. Ili aweze kumsaidia kurekebisha kumbukumbu na kumwezesha kupata fedha
hizo amtumie kiasi fulani cha fedha. Mstaafu huyo akishamtumia hapatikani tena
kwenye hiyo namba aliyotumia na mstaafu huyo anakuwa ameishaibiwa fedha zake.
Natoa tahadhari kwa wastaafu wasikubaliane na watu wa aina hiyo na
idara mbalimbali zichukue tahadhari kubwa na kila mara wahakikishe
kinachohitajika kinatoka katika idara husika na kwa mtu sahihi.
Pia nichukue fursa hii kutoa tahadhari kwa Vyama vya Siasa, wafuasi wao
na wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwa ujumla katika kipindi hiki cha Kampeni na
baadaye kupiga kura, kutangaza matokeo na kuapisha waliochaguliwa kila mmoja
azingatie utii wa sheria.
Ninatoa wito huo kwa sababu kuna baadhi ya Vyama wameishaanza kukiuka
sheria kwa kuwatumia watoto na kuvuruga mikutano ya vyama vingine. Mfano tarehe
29.08.2015 huko katika kijiji cha Tubugwe Kibaoni Kata ya Chamkoroma Wilaya ya
Kongwa Chama cha CCM kilikuwa kifanye Mkutano asubuhi ambao ulikuwa halali
kulingana na ratiba. Ulishindikana kufanyika baada ya vijana na watoto
wadogo wakiwa na bendera za Chadema kuanza kuzunguka eneo hilo huku wakiimba.
Kama hilo halitoshi walizuia barabara ili wagombea na wafuasi wa CCM wasipite.
Tukio hilo bado ufuatiliaji wa kuwakamata waliohamasisha watoto hao na
kushiriki katika uvunjaji huo wa sheria unaendelea.
Nichukue fursa hii pia kupiga marufuku Vyama vya Siasa vinavyotumia au
wanampango wa kutumia vikundi vyenye muelekeo wa kijeshi mfano Blue
Guard, Red Briged, Green Guard n.k. kwani kazi ya ulinzi Mkoani Dodoma ni ya
Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya dola.
Nitoe rai kwa kila mmoja afuate Sheria Mama Katiba, Sheria ya Vyama vya
Siasa, Uchaguzi na nyinginezo zinazotuongoza katika kipindi cha Kampeni hadi
Uchaguzi ili kuepuka kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Imetolea na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi - Misime D.A (SACP)
0 comments:
Post a Comment