RAIS wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Jamal Malinzi, amefunga kozi ya wiki mbili ya makocha lesseni C inayotambuliwa na Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) na kuwataka wahitimu hao kufanyia kazi mafunzo waliyoyapata.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya
kufunga mafunzo hayo, Malinzi amesema kuwa anasikitika kuona makocha wanapata
mafunzo kama hayo lakini wanaenda kuweka vyeti vyao ‘makabatini’ na kuacha
kufanyia kazi walichojifunza.
“Hiki mlichokipata kwenye mafunzo
haya mnatakiwa muende mkafanyie kazi kwa kutafuta timu za kufundisha na baada
ya mwaka mmoja ni vizuri mkajiendeleza zaidi ya hapa,” alisema Malinzi
Aidha, amesema kuwa Shirikisho lake
limepanga kuhakikisha baada ya muda litafuta utaratibu wa makocha wenye lesseni
C kuwa kwenye benchi la ufundi la timu za daraja la kwanza na kuwa wasaidizi
kwenye benchi la ufundi la timu za ligi kuu.
“kwa sasa hivi makocha wa ligi kuu
wanatakiwa kuwa na leseni ya daraja B na wasaidizi angalau leseni daraja C, ila
kuanzia msimu wa 2017-2018 mambo yatabadilika na lessen I C aizataruhusiwa
kwenye mabenchi ya ufunzi kwa timu za ligi kuu, mambo yataendelea hivyo mpaka
mwisho tutakuwa na leseni za daraja A,” alisema Malinzi.
Aidha, aliwataka wahitimu hao ambao
wengi wao wanatoka kwenye klabu za daraja la kwanza na wengine wakiwa makocha
wasaidizi kwenye klabu za ligi kuu, kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata
kwenye mafunzo hayo kuzisaidia timu zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama
Cha soka mkoa wa Dar es Salaam, Almas Kasongo, ameishukuru TFF kwa jitihada za
kuendeleza mchezo wa soka nchini na kuelelezea changamoto wanazokutana nazo
katika kuandaa kozi kama hizo kwa vyama vya soka vya mikoa nchini.
“Sisi DRFA tumefanikiwa kuendesha
kozi hii kwa sababu ya uwepo wa timu za Simba, Yanga na Azam kwenye ligi kuu
ambazo ni sehemu ya mapato kwa chama chetu, ila kwa vyama vingine hali inakuwa
ngumu kuandaa na kuendesha mafunzo kama hayo,” alisema Kasongo.
Kozi hiyo ya wiki mbili ilikuwa
ikifanyika kwenye ukumbi wa TFF na kuendeshwa na mkufunzi anayetambulika na
CAF, Salum Madadi ambaye pia ni Mkurugenzi wa ufundi wa TFF.
0 comments:
Post a Comment