Mkuu wa mauzo na masoko
wa GSM Media, Elibariki Lukumay,(kulia) akimkabidhi mfano wa hundi Mwenyekiti
wa Chama cha Wandishi wa Michezo (TASWA) Juma Pinto kwa ajili ya kumuaga Rais
Kikwete pamoja na tuzo kwa wanamichezo zitakazofanyika Oktoba 8, Mlimani City,
Dar es Salaam. Katikati ni M/Mkiti wa TASWA, Egbert Mkoko.
Mkuu
wa mauzo na masoko
wa GSM Media, Elibariki Lukumay akizungumza wakati wa mkutano na
wandishi wa habari, Kulia ni Katibu wa TASWA, Amir Mhando na Katikati ni
Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto.
***************
KAMPUNI ya GSM Media ya Dar es
Salaam imetoa Sh milioni 50 kwa ajili ya kudhamini tuzo za wanamichezo
waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Jakaya
Kikwete.
Utoaji wa tuzo hizo utafanyika
Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ambapo wanamichezo
pia watatumia tuzo hizo zilizoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA) kumuaga Rais Kikwete anayemaliza muda wake kikatiba.
Kwa mujibu wa TASWA licha ya
kumuaga Rais Kikwete na kutoa tuzo kwa wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi,
pia chama hicho kitatoa Tuzo ya Heshima Rais Kikwete ikiwa ni kuthamini
mchango wake kwa michezo katika utawala wake.
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari kutambulisha udhamini huo Dar es Salaam jana, mwakilishi wa
GSM Foundation, Elibariki Lukumay, alisema wameguswa na tukio hilo na kuona
kuna umuhimu wa kuiunga mkono TASWA.
“Taasisi yetu ambayo ina
kampuni mbalimbali imeguswa na kitendo ambacho TASWA inakiandaa na kwa kuanzia
tunatoa kiasi hicho cha fedha kufanikisha jambo hilo na tunawaomba wengine pia
waunge mkono.
“Rais Kikwete amefanya mambo
makubwa katika michezo nchi hii, hivyo tukiwa pia wadau wakubwa wa michezo
tumeona ni vyema tuungane na wenzetu wa TASWA katika kumuaga na kumshukuru kwa
mchango mkubwa alioufanya kwa michezo,” alisema Lukumay.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru taasisi hiyo na kusema
kuwa bajeti ya tukio hilo ni Sh milioni 130 na kwamba wadhamini hao wamefungua
milango kwa wengine ili kulifanikisha jambo hilo.
“Tunaamini
mchango wa Rais Kikwete katika medani ya michezo hauna mfano na kila mdau wa
michezo atakubali amefanya mambo makubwa kwa michezo.
“Tunafahamu Rais alivyosimamia
serikali yake kulipia makocha wa michezo ya soka, netiboli na ngumi. Pia
chini ya utawala wake serikali ilipeleka wanariadha wetu China, Ethiopia na New
Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa,” alisema.
Alifafanua kuwa karibu vyama
vyote vya michezo nchini vitashikirikishwa katika tukio hilo ikiwa ni pamoja
kuwa karibu kwa kila hatua na Wizara Ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT). Source: Lenzi ya Michezo Blog
0 comments:
Post a Comment