Nafasi Ya Matangazo

July 21, 2015



Mkurugenzi Mkuu Mpya - TCRA, Dk. Ally Y. Simba

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa hivi karibuni alimteua Dk. Ally Yahaya Simba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, (TCRA) kufuatia mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mkuu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano ya 2003 kifungu cha 9 na kifungu cha 13. (TCRA Act, 2003)

Dk. Simba aliteuliwa rasmi kushika wadhifa huo mnamo tarehe 6 Jula1 2015 kwa kipindi cha miaka mitano. Kabla ya uteuzi huo, Dk. Simba alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia tangu Agosti 2013. Dk. Simba ana uzoefu wa zaidi ya miaka 16 katika Sekta ya Mawasiliano ambapo amefanya kazi kwa watoa huduma, Taaluma ya Utafiti, Udhibiti pamoja na Serikali Kuu.

Dk. Simba ana Shahada ya B.Sc. (Hons.) Shahada ya Sayansi ya Elektroniki na Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, aliyopata mwaka 1998. Pia ana Shahada ya Uzamili ya Uhandisi aliyoipata mwaka 2003 na Shahada ya Uzamivu (Ph.D) ya Uhandisi wa Kielektroniki kutoka Chuo Kikuu Cha Hokkaido, Sapporo, nchini Japan, aliyoipata mwaka 2006. Kuanzia mwaka 2006 mpaka 2011, Alikuwa Mtaalamu Mtafiti katika Taasisi ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, huko Tokyo, Japan, ambako alihusika katika kufanya utafiti wa madhara ya ya kiafya kwa mwanadamu kwa kutumia simu za mikononi na kwa kuwa karibu na minara ya mawasiliano.

Mnamo mwaka 2011 hadi mwaka 2013, alifanya kazi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama Meneja Mipango na Utafiti wa Mamlaka.

Dk. Simba ametoa machapisho kadhaa yaliyosambazwa kote duniani katika majarida ya kimataifa na amewasilisha matokeo ya tafiti zake katika zaidi ya mikutano 30 ya kimataifa ndani na nje ya Tanzania. Aidha Dk. Simba alikuwa Kiongozi wa timu ya wataalamu wa Kitanzania iliyoandaa Sheria za Uhalifu wa Mitandao nchini iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni.

Dk. Simba ni Mhandishi Mahiri (Chartered Engineer), aliyesajiliwa nchini Uingereza  katika Baraza la Uhandisi nchini humo na ni “Fellow”  wa Taasisi ya Uhandisi na Teknolojia ya nchini Uingereza, ambako alifanya kazi kama Mshauri wa Kimataifa  wa Usajili wa Wanataaluma Wahandisi kutoka Aprili 2011 mpaka Machi 2014. Pia Dk. Simba ni Mwanachama wa “Institute of Electrical and Electronics Engineers” (IEEE). Hali kadhalika Dk. Simba amechapishwa katika jarida la “Marquis Who's Who in Science and Engineering” katika toleo la 11, la mwaka 2011–2012.

Dr. Simba ni miongoni waliopata Udhamini wa Serikali ya Japan (Monbusho Scholarship) kutoka mwaka 2000 mpaka 2006.
Posted by MROKI On Tuesday, July 21, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo