Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Mathias Chikawe (pichani juu) atakuwa mgeni
rasmi kwenye mbio za 13 za Kilimanjaro Marathon zinazotarajiwa kufanyika
Jumapili tarehe 1 Machi, 2015 huko Moshi.
Aggrey Marealle, Mkurugenzi Mkuu wa Executive Solutions,
waratibu wa mbio hizo alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana
kuwa Waziri Chikawe ataanzisha mbio hizo
zinazotarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 6,000 kutoka nchi zaidi ya 40 na
atakuwa mgeni rasmi katika sherehe ya kutoa zawadi ambapo atatoa zawadi kwa
washindi 10 wa mbio za 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon.
“Mhe. Chikawe amekubali kuanzisha mbio na kutoa zawadi kwa
washindi wa 42km Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa wanaume na wanawake,”
alisema Marealle. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Leonidas Gama atakuwa ni
kati ya wageni mashuhuri watakaohudhuria tukio hilo.
Marealle aliongeza kuwa Kilimanjaro Marathon ni tukio ambalo
limeendelea kuongeza hadhi ya Tanzania
kimataifa kila mwaka; na imesaidia kutambua na kutoa fursa kwa wanariadha wa
ndani kukua zaidi, kukuza utalii wa Tanzania na watu kupata nafasi ya kufurahi
zaidi.
Alisema mbio hizo zitakuwa na viwango vya kimataifa kama
ilivyo kawaida na zitasimamiwa na Kilimanjaro Marathon Club, Riadha Tanzania na
Chama cha Riadha Mkoa wa Kilimanjaro. Ili kuhakikisha usalama wa wanariadha na
washiriki wote kwa ujumla, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imetoa kibali cha
kufungwa kwa baadhi ya barabara za ndani na nje ya mji wa Moshi ambazo zitatangazwa
badae zitafungwa kwa muda saa 12:15 asubuhi hadi 02:00 asubuhi tarehe 1, Machi
20135ili kuruhusu waanariadha kupita salama kwani mbio hizi zimekuwa na
ongezeko kubwa la washiriki kila mwaka jambo ambalo linalazimu waandaaji
kuimarisha usalama.
Marealle alisema kuwa “Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia
kinywaji chao cha Kilimanjaro Premium Lager ndio wadhamini wakuu wa Kilimanjaro
Marathon na shughuli zingine za burudani baada ya riadha, na wamekuwa wadhamini
wa tukio hili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2003. Juhudi zao katika masoko na
matangazo imekuwa mchango mkubwa katika kukuza mbio hizi. Nawaomba wananchi wa
Moshi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki na
kushangilia watakaoshiriki kwani kuna kuna zawadi za kuvutia kutoka kwa
wadhamini pamoja na medali na fedha taslimu kwa washindi ”.
Marealle alisema kuwa mbio hizi zimejipatia umaarufu mkubwa
kutokana na kuungwa mkono na wananchi wa Moshi na vilevile kuungwa mkono na
serikali ya mkoa pamoja na taasisi kama polisi na manispaa ya Moshi.
Mbio hizo zinaratibiwa na Executive Solutions kwa
kushirikiana na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Kilimanjaro na Kilimanjaro
Marathon Club huku zikidhaminiwa na wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager,
Tigo (Tigo Kili Half Marathon), GAPCO (Walemavu), Simba Cement, KK Security,
Keys Hotel, TPC Sugar, CMC Automobiles
Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, Kibo Palace Hotel, UNFPA na Kilimanjaro Water.
0 comments:
Post a Comment