Mbio
za Kilimanjaro Marathon 2015 zitafanyika kwenye njia ile ile iliyotumika
mwaka jana baada ya kupimwa na kuidhinishwa na shirikisho la riadha
duniani. Njia hiyo ni mzunguko na imelenga kuwafanya wanariadha wakimie
kwa raha na usalama zaidi bila tatizo la msongamano barabarani.
Akizungumzia
njia hiyo Mkurugenzi wa Kilimanjaro Marathon, John Bayo amesema “Ni
njia nzuri sana. Mbio za Full marathon zitaanzia uwanja wa Ushirika na
kwenda kilomita kumi njia ya kuelekea Dar es salaam na kurudia njia hiyo
kupitia geti la Chuo cha Ushirika. Wakati wanariadha wa kilomita 42
wanapita mbele ya geti, wale wa kilomita 21 (Tigo Kili Half Marathon)
watakuwa mbele yao kwa takribani dakika 30 maana mbio yao inaanzia
kwenye geti la Ushirika na kupandisha kuelekea Mweka kwa umbali wa
kiomita 8”.
Baada
ya kilomita 8, njia wataacha barabara ya lami kukimbia kwenye barabara
ya vumbi kwa kilomita mbili kupitia mashamba ya kahawa ili kuipata
Barabara ya Lema ambapo wataendelea kukimbia na kupita Shule ya
Kimataifa ya Moshi na kutelemka kuelekea uwanjani. Bayo alisema kwamba
njia nzima ina viburudisho vya kutosha pamoja na vituo vya maji na vile
vile magari ya huduma ya kwanza.
Mbio
za walemavu zitaanzia uwanja wa Ushirika na kuifata Barabara ya
Kilimanjaro ambayo ni tambarare tupu na ina kivuli hadi Barabara ya Lema
ambapo watageuza na kurudi Uwanjani wakiwa wamekamilisha kilomita 10.
John
Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo
alisema njia hiyo mpya itapendwa na wanariadha kwakuwa inapita maeneo
yenye mandhari nzuri ya miti na mashamba na njia hiyo haina msongamano
na anaamini kwamba washiriki watakimbia kwa raha katika mbio hizo
zitakazofanyika tarehe 1 Machi, 2015.
Aliongeza
kuwa mbio ndefu la Kilimanjaro Premium Lager Marathon za kilomita 42
zitaanza saa 12.30 asubuhi kutokea uwanja wa Ushirika wakati mbio za
Tigo Kili Half Marathon zitaanzia nje ya geti la Chuo cha Ushirika saa
moja kamili asubuhi na kukimbia wakielekea Mweka na mbio yao itaishia
hapo hapo uwanjani. Wakati huo huo mbio za walemavu za Gapco zitaanza
saa 12.45 (saa moja kasorobo) kutokea uwanja wa Ushirika na huku mbio za
kujifurahisha za 5 km Fun Run zikianza saa 1.45 asubuhi kwenye mzunguko
wa YMCA na kumalizikia uwanjani.
Mbio
za Kilimanjaro Marathon 2015 zinaratibiwa na Executive Solutions kwa
kushirikiana na Riadha Tanzania, Riadha Kilimanjaro na Kilimanjaro
Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Tigo,
GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, CMC
Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, Kibo Palace Hotel, UNFPA na
Kilimanjaro Water.
0 comments:
Post a Comment