Jaji Mkuu
wa Tanzania Mh. Othman Chande (Kulia) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa
habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya
Sheria nchini mwaka 2015. Maadhimisho hayo
yanaongozwa na maudhui yasemayo “
Fursa ya kupata haki: wajibu wa Serikali, Mahakama na wadau”. Kushoto ni Mh.
Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama.
***********
Rais Jakaya Kikwete anatarijiwa kuwa mgeni
rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya sheria nchini (Law Day)
itakayofanyika Februari 4, 2015, katika viwanja vya mahakama vilivyopo mtaa wa
Chimala jijini Dar es salaam.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Othman
Chande amesema kuwa maadhimisho hayo kwa mwaka huu yanaongozwa na maudhui yasemayo “ Fursa ya kupata haki: wajibu wa Serikali,
Mahakama na wadau”.
Amesema kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo
yataambatana na maonesho ya Wiki ya
Shera yatakayofanyika katika
viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia tarehe
30 Januari 2015 hadi
tarehe 2 Februari 2015 .
Mh.Chande ameeleza kuwa
maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini na maonesho ya Wiki ya Sheria yanaashiria
mwanzo wa shughuli za mahakama kwa mwaka 2015
na kufafanua kuwa kipaumbele kitatolewa katika kupunguza mrundikano wa
mashauri ya muda mrefu yaliyoko mahakamani na kushughulikia mashauri yenye
mvuto mkubwa kijamii,miradi mikubwa, uhujumu uchumi, madawa ya kulevya,
Biashara ndani na nje ya nchi na Rushwa.
Kuhusu maonesho hayo
amesema yanalenga kutoa elimu kwa wadau
wa sheria na huduma za kisheria kwa wananchi kuhusu Ufunguaji na uendeshaji wa
mashauri mbalimbali hasa mirathi, Utatuzi wa migogoro kwa njia ya suluhu,
kueleza mfumo mpya wa ulipaji wa tozo za kimahakama kwa njia ya benki, Kutoa
msaada wa kisheria, kutolewa vyeti vya mawakili, kupokea maoni na malalamiko
kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.
Ameeleza kuwa wadau
wakuu watakaoshiriki katika maonesho
hayo ni Mahakama, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Chuo cha Uongozi wa Mahakama-
Lushoto, Taasisi ya Mafunzo ya Uansheria kwa vitendo Tanzania na Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora.
Wadau wengine ni
Taasisi zinazotoa msaada wa kisheria, TAKUKURU, Jeshi la Polisi, Magereza,
Chama cha Mawakili Tanganyika na Tume ya kurekebisha sheria.
Amesema pamoja na
maonesho hayo kutakuwa na matembezi maalum ya kuadhimisha Wiki ya Sheria tarehe
1 Februari 2015 yatakayoongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili Mh. Ali Hassan
Mwinyi kuanzia Mahakama Kisutu kupitia barabara za Serena-Ohio, Gymkana –Obama
Road, Mahakama ya Biashara, Barabara ya Kivukoni, Sokoine , Railway, Nkurumah,
Lumumba na Mkunguni hadi Mnazi Mmoja.
0 comments:
Post a Comment