NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MRATIBU Mkuu wa Tamasha la Utamaduni Handeni, maarufu kama ‘Handeni
Kwetu’, Kambi Mbwana, ameapa kuhakikisha kuwa tamasha lao msimu wa 2014
linakuwa la aina yake na kuvunja rekodi ya mwaka jana lilipofanyika kwa mara ya
kwanza wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mbwana alisema kuwa
hiyo ni kutokana na kutamani kushirikisha wasanii wengi kutoka Tanga na
Tanzania kwa ujumla.
Alisema kwamba mwaka jana wasanii zaidi ya 200 walionyesha
uwezo wao kutoka kwa vikundi mbalimbali vya wilayani Handeni na jijini Dar es
Salaam.
“Mwaka jana vikundi zaidi ya 10 vyenye wasanii wasiopungua 15
walipata nafasi ya kupanda jukwaani kuonyesha vipaji vyao, ukiacha wasanii
wanaotoka kwenye Kambi ya jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa Mgambo waliozidi 80.
“Wakati tunajivunia
mafanikio haya, tunaamini msimu huu utakuwa mzuri zaidi tukiamini kuwa
tutavunja rekodi ya mwaka jana, ambapo
tulishuhudia burudani mbalimbali, ikiwamo hadithi zilizohusu watu wa
Handeni,
bila kusahau vyakula vya asili pamoja na michezo waliyokuwa wakicheza
wazee
wetu enzi hizo,” alisema Mbwana.
Kwa mujibu wa Mbwana, mipango ya kuboresha tamasha hilo
imepamba moto ambapo kwa sasa utafiti wa ubora wa vikundi nje ya wilaya ya
Handeni inafanywa ili kuhakikisha kuwa wasanii watakaopanda jukwaani wanakuwa
na uwezo wa juu na kufanikisha kwa dhati kukuza sekta ya utamaduni pamoja na uchumi wa Tanzania.
0 comments:
Post a Comment