Afisa
Mahusiano na Habari wa Chama cha Albino Tanzania Bw. Josephat Torner akiongea
na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam kuhusu na uzinduzi wa filamu ya
“Chini ya Kivuli cha Jua” utakaofanyika Mei 2, mwaka huu ambapo Mgeni Rasmi
anatarajiwa kuwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.
Mizengo Pinda. Pamoja nae ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la
Kiserikali la Standing Voice lililofadhili mradi wa uandaaji wa Filamu ya
“Chini ya Kivuli cha Jua” Bw. Jon Beale.
**********
Na Frank Mvungi-Maelezo
Filamu ya Chini ya Kivuli cha Jua kuzinduliwa Jijini
Dar es salaam wiki ijayo ikiwa ni moja ya hatua za kuelekea maadhimisho ya
Mkutano wa Kimataifa kuhusu ualbino unaotarajiwa kufanyika hapa nchini mapema
mwezi Mei mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Afisa Mahusiano na Habari wa Chama
cha Albino Tanzania Bw. Josephat Torner wakati wa mkutano na Waandishi wa
Habari leo jijini Dar es salaam kuhusu uzinduzi wa filamu hiyo.
Bw. Josephat alisema kuwa katika uzinduzi wa Filamu
hiyo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mh. Mizengo Pinda na uzinduzi unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa
Alliance De Francaise uliopo Upanga Jijini Dar es salaam.
Akifafanua Bw. Josephat amesema kuwa lengo kuu la
filamu hiyo ni kuwaelimisha watanzania kuhusu matatizo yanayowapata watu wenye
ulemavu wa ngozi (Albino) hapa nchini ili jamii iweze kushiriki kikamilifu
katika kuondoa matatizo yanayowakabili.
Aliongeza kuwa filamu hiyo imeandaliwa hapa
nchini na baada ya uzinduzi wake itaonyeshwa katika Mikoa ya Kanda ya
Ziwa kwa muda wa miezi 9 ikiwa na lengo la kuwafikishia ujumbe wananchi
kuhusu hali halisi ya maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Katika ziara ya kuonesha filamu hiyo Bw. Josephat
amesema kuwa wataambatana na Madaktari wataalam wa ngozi watakaosaidia kutoa
elimu kwa wananchi kuhusu matatizo ya watu wenye ulemavu wa ngozi na hatua za
kuchukua ili kuwakinga na athari zinazotokana na mazingira.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la
Kiserikali la Standing Voice lililofadhili mradi wa uandaaji wa Filamu hiyo Bw.Jon
Beale alisema filamu hiyo inaujumbe wa kutaka kuonyesha ulimwengu hali halisi
ya maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na hatua ambazo jamii
inapaswa kuchukua katika kuwalinda wale wenye tatizo hilo.
Watanzania wamepewa wito wa kushiriki vyema katika
kuelimisha jamii kuhusu matatizo ya watu wenye ualbino hapa nchini ili kujenga
jamii yenye kuzingatia misingi ya haki na usawa.
Filamu hiyo imeshaonyeshwa katika nchi zisizopungua 50
tangu mwaka 2012 ambapo baadhi ya nchi hizo ni Mexico, Brazil, Marekani,
Australia, Norway, Sweeden, Dernmark pamoja na nchi nyingine za Ulaya na mabara
mengine.
0 comments:
Post a Comment