Nafasi Ya Matangazo

March 17, 2014

 Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama  akisalimiana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Boma mara baada ya kufunga mafunzo ya sanaa kwa watoto 200 wa shule za msingi tano za wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam jana. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na kufadhiliwa na kampuni ya Msama Promotions. 
 Baadhi ya watoto wa Shule za Msingi kutoka Wilaya ya Ilala wakionesha vipaji vya kucheza ngoma wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya sanaa yaliyoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata),na kufadhiliwa na Kampuni ya Msama Promotions . Jumla ya watoto 200 wamenufaika na mafunzo hayo.
  Mmoja wa wanafunzi akionesha mitindo ya mavazi.
 Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Buguruni Visiwi wakionesha mitindo mbalimbali wakati wa hafla hiyo.
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo ya sanaa kwa watoto yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Basata na kudhaminiwa na Kampuni ya Msama Promotions. Kushoto ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza na Ofisa Tawala wa Kampuni ya Msama Promotions, Hamis Mussa.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza akizungumza wakati wa hafla hiyo.
 Mtoto Mariam Yusuf akisimulia hadithi wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya sanaa kwa watoto wa shule za msiongi kutoka Manispaa ya Ilala. 
 Mtoto Mariam akionesha kipaji chake.
 Watoto wakicheza maigizo.
 Baadhi ya watoto wa Shule ya Msingi Uhuru Wasichana wakiwa katika hafla hio.
 Msama akiagana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Uhuru Wasichana.

DAR ES SALAAM, Tanzania

MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama amepongeza hatua ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kuanzisha mafunzo maalumu kwa watoto wa shule za msingi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa kufunga mafunzo maalumu yanayolenga kuwajenga watoto katika fani ya sanaa na kushirikisha watoto wapatao 200 kutoka shule tano za wilaya ya Ilala, Msama alisema ni jambo zuri kuandaa vipaji vya kesho.

“Mafunzo haya yataweza kuwajenga watoto wetu ambao ndio taifa la kesho, pia kupunguza tatizo la watoto kujiingiza katika mambo mabaya kama matumizi ya bangi, dawa za ulevya, hivyo kuwa mzigo na janga kwa taifa,” alisema Msama.

Shule zilizonufaika na mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Msama kupitia kampuni yake ya Msama Promotions, waratibu wa Matamasha ya Pasaka na Krismas, ni Buguruni Moto, Buguruni Visiwi, Ilala Boma, Uhuru Wasichana na Msimbazi.

Aidha, Msama alihimiza umuhimu wa somo la sanaa shuleni akitaka lipewe msisitizo mkubwa katika kuandaa vijana bora ambao hata kama wakifeli masomo mengine, wanaweza kuwa wasanii bora.
“Somo hili la sanaa mashuleni lipewe uzito unaostaili kama masomo mengine kwa sababu, mtoto akifeli masomo mengine, fani ya sanaa yaweza kuwa msaada kwake,” alisema.

Msama aliwashauri pia Basata kuyapeleka mafunzo hayo hadi mikoani na kupendekeza kwa hatua ya awali waanzie katika mikoa ya Pwani na Morogoro, akiamini kuna vipaji vingi vya sanaa.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisema mafunzo hayo yaliyoanza Machi 1, wanafunzi walikuwa wakifanya mazoezi ya sanaa katika fani utambaji, hadithi, ngoma za asili na maigizo katika maeneo ya shule zao chini ya usimamizi wa walimu wao na waratibu kutoka Basata.


Mngereza alimshukuru mgeni rasmi Msama kwa kudhamini mafunzo hayo akisema amefanya hivyo kwa kutambua umuhimu wa elimu ya sanaa katika maisha ya kila siku.

“Msama ameonesha wazi kuwa yeye ni mdau na mfurukutwa wa sanaa, aliyepania kuendeleza sekta ya utamaduni hasa sanaa kwa kuibua vipaji vya watoto,” alisema.
Posted by MROKI On Monday, March 17, 2014 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo