Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amewaonya wanachama na mashabiki wa
timu hiyo wanaotishia maisha Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano ya imataifa wa
klabu hiyo, Seif “Magari” Ahmed kuwa sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.
Katika taarifa yake
aliyoitoa jana, Manji amesema kuwa si suala jema kwa wanachama kumuhusisha Seif
na matokeo ya timu hiyo ambayo kwa sasa imeshinda mechi moja na kutoka sare
mechi moja katika mzunguko wa pili wa Ligi kuu ya Tanzania Bara.
Manji amesema kuwa
madai kuwa Seif siyo mwanachama halali
wa Yanga hayana msingi wowote na kuyaita madai hayo kuwa ni ya uzushi na
yanaenezwa na maadui zao ambao hawaitakii Yanga mema.
Alisema kuwa hivi karibuni
kumekuwa na madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu,
taarifa za hujuma ndani ya timu ambazo zimewahusisha uongozi na baadhi ya
wanachama jambo ambalo si la kweli.
Alifafanua kuwa ni
haki kwa kwa nia njema kwa wanachama kuhoji mwenendo wa timu yao pale wanapoona-hairidhishi
na ni wajibu wa wanachama kuchanganua mawazo merna na mabaya na siyo kumuhisha
mtu kwa moja kwa moja kutokana na mtazamo hasi walionao.
“Ushindi au
mwenendo mzuri wa timu unatokana na
viwango vizuri, nidhamu na ushirikiano wa wahusika wote, wachezaji,
walimu, viongozi, wanachama na wapenzi kwa ujumla. Uongozi ulikutana na
wachezaji, walimu, baadhi ya wanachama na wapenzi na kuyazungumzia na
kukubaliana kuhusu mapungufu yaliyojitokeza kwa wahusika wote na kuchukua hatua
ya kubadilisha benchi la ufundi,” alisema Manji.
Aliongeza kwa
kusema kuwa uongozi ulifika mbali zaid kwa kutoa adhabu na onyo kali kwa baadhi
ya wachezaji walionyesha utovu wa nidhamu kwa kipindi kilichopita na kusikitishwa
kuona kuwa baadhi ya wadau kwa kutumia vyombo vya habari wanachochea na kutengeneza
uhasama ambao kwa kweli haupo ama kwa faida zao binafsi, au
kwa kutumiwa na watu ambao hawana nia njema kwa klabu.
Manji pia aliwaomba
wadau wote wanamichezo na hasa wahariri wa michezo kudhibiti matumizi mabaya ya
watu au vyombo vya habari yanayochangia sana kuzorotesha michezo nchini.
0 comments:
Post a Comment