Mwenyekiti wa taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma
Kikwete, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt Shukuru
Kawambwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya WAMA Nakayama Dkt Ramadhani Dau
na Mkuu wa Shule hiyo wakipokea moja ya Tabuleti 61 alizozitoa kwa
ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Wama Nakayama
iliyoko kijijini Nyamisati, Rufiji, Mkoa wa Pwani leo Januari 27, 2014
toka kwa Mwenyekiti wa taasisi ya kusaidia elimu ya Opportunity
Education Foundation wa Marekani Bw. Joe Ricketts akikabidhi moja ya
Tabuleti 61 alizozitoa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili katika
Shule hiyo.
Mwenyekiti wa taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma
Kikwete, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt Shukuru
Kawambwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya WAMA Nakayama Dkt Ramadhani Dau
na Mkuu wa Shule hiyo wakiangalaia matumizi ya ya Tabuleti 61 katika
darasa la kidato cha pili katika Shule ya Wama Nakayama iliyoko
kijijini Nyamisati, Rufiji, Mkoa wa Pwani leo Januari 27, 2014 toka kwa
Mwenyekiti wa taasisi ya kusaidia elimu ya Opportunity Education
Foundation wa Marekani Bw. Joe Ricketts akikabidhi moja ya Tabuleti 61
alizozitoa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili katika Shule hiyo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea jezi ya timu ya baseball ya Chicago
Cubs toka kwa mmiliki wa timu hiyo na Mwenyekiti wa taasisi ya
kusaidia elimu ya Opportunity Education Foundation wa Marekani Bw. Joe
Ricketts wakati alipomtembelea Ikulu Jumapili Januari 27, 2014
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea moja ya Tabuleti 61 kwa
ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Wama Nakayama
iliyoko kijijini Nyamisati, Rufiji, Mkoa wa Pwani toka kwa Mwenyekiti
wa taasisi ya kusaidia elimu ya Opportunity Education Foundation wa
Marekani Bw. Joe Ricketts wakati alipomtembelea Ikulu Jumapili Januari
27, 2014 .
***********
Serikali inakusudia kutoa maelfu kwa maelfu ya tabuleti
za kufundishia masomo mbali mbali kwa
wanafunzi na walimu wa shule za sekondari nchini kama njia ya ubunifu zaidi, ya
kisayansi na ya uhakika ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya
elimu kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).
Ili kufanikisha mpango huo, Serikali inakusudia
kuingia ushirikiano (partnership) na
taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Opportunity Education Trust ya Marekani
ambayo leo, Jumatatu, Januari 27, 2014, inazindua mpango wa majaribio wa utoaji
wa tabuleti hizo kwa wanafunzi na walimu wao wa shule za sekondari nchini.
Mpango wa Serikali wa kusambaza tabuleti kwa
wanafunzi na walimu wa shule za sekondari ulitangazwa usiku wa jana, Jumapili,
Januari 26, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete wakati alipokutana na kuzungumza na Bwana Joe Ricketts, mwenye
taasisi ya Opportunity Education Trust na mmoja wa matajiri wa Marekani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar
es Salaam, Rais Kikwete amemweleza kwa undani Bwana Ricketts hatua ambazo
zimechukuliwa na Serikali yake kupania na kuboresha elimu tokea mwaka 2006,
hatua ambazo zimechangia kupanua kwa kasi na kwa kiwango kikubwa wigo wa utoaji
elimu nchini na changamoto ambazo zimezuka kutokana na upanuzi huo mkubwa.
Rais Kikwete amesema baadhi ya changamoto hizi
ni ukosefu wa walimu, na hasa walimu wa masomo ya sayansi, na ukosefu wa vitabu
vya kufundishia changamoto mbili kubwa ambazo zinatatuliwa na matumizi ya tabuleti.
“Mbali na
upanuzi mkubwa wa nafasi za wanafunzi kupata elimu ya ngazi mbali mbali, pia
tumepanua sana ufundishaji wa walimu. Mwaka 2005, vyuo vyetu vyote vilikuwa
vinatoa walimu 500 sasa tunatoa walimu 12,000 kwa mwaka. Hivyo, tunaamini kuwa
katika mwaka mmoja ama miwili ijayo, tutakuwa tumemaliza tatizo la walimu wa
masomo ya sanaa,”
Rais Kikwete alimwambia Ricketts na kuongeza:
“Lakini
bado tunakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi, kama zilivyo nchi nyingine.
Tuna upungufu wa walimu 26,000 na kwa mwaka vyuo vyetu vyote vinahitimisha walimu
2,100 tu. Hii ina maana kuwa itabidi kusubiri miaka 13 kuweza kumaliza tatizo
hili kwa mahitaji ya sasa. Hili haliwezekani na hii ndiyo maana halisi ya
kutumia sayansi na teknolojia ya namna hii kufundishia wanafunzi wetu.”
Rais Kikwete alisema kuwa matumizi ya teknolojia
kufundishia nchini ni jambo linalowezekana kwa urahisi kwa sababu mtandao wa
mawasiliano wa National Fibre Network
ambao karibu umefikia kila wilaya sasa.
Rais Kikwete alimshukuru Bwana Ricketts na taasisi yake kwa kukubali kuchangia maendeleo
ya sekta ya elimu nchini kwa kusambaza teknolojia ya kisasa kama moja ya njia
za ubunifu zaidi za kufundishia hasa masomo ya sayansi.
Chini ya mpango huo wa majaribio wa kusambaza
teknolojia hiyo ya kisasa, taasisi ya Opportunity
Education Trust inatoa tabuleti 1100 kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa
sekondari katika shule 33.
Bwana Ricketts ambaye ni mwenyeji wa Omaha,
Nebraska alimwambia Rais Kikwete: “Hapa
tunafanya majaribio na Tanzania ni nchi ya kwanza duniani miongoni mwa nchi
ambazo tunaunga mkono mipango ya maendeleo kunufaika na mpango huo wa
majaribio. Ni azma yetu kuwa baada ya kuwa tumefanya tathmini ya mafanikio na
changamoto za hatua hii ya majaribio, tutaupanua mpango huu kushirikisha shule
nyingi zaidi kwa kushirikiana na Serikali kwenye mpango wake mkubwa wa
kusambaza teknolojia hii katika shule zote za sekondari hapa Tanzania.”
Bwana Ricketts na wataalam wake pamoja na
maofisa wa Serikali wameanza kutekeleza mpango huo leo, Jumatatu, Januari 27,
2014, kwa kutoa tabuleti kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wama Nakayama
iliyoko Mkoa wa Pwani.
Baada ya leo, shughuli hiyo itahamia Zanzibar na
Pemba, kabla ya Bwana Ricketts na wataalam wake kutoa tabuleti kwa shule
zilizoko mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kagera na Morogoro.
Shule zinazonufaika katika mpango huo ni za
Serikali na binafsi na kwa kuanzia masomo ambayo yanapatikana katika tabuleti
hizo ni hesabu, jiografia, historia na kiingereza.
0 comments:
Post a Comment