Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika Eneo la
Maziwa Makuu, Mary Robinson akizungumza na waandishi wa habari nje ya
ukumbi wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya yeye na
Bw. Martin Kobler (kulia) ambaye ni Muwakilishi wa Katibu Mkuu katika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa MONUSCO kuwasilisha
taarifa zao mbele ya Baraza Kuu la Usalama, katika mkutano wa ndani wa
Baraza hilo uliofanyika siku ya jumatano. katika mkutano huo wakuu hao
wawili walielezea kuridhishwa kwao na hali ya kijeshi na kisiasa
inavyoendelea katika DRC hususani eneo la Mashariki ya nchi hiyo.
pamoja na mchakato wa utekelezaji wa Mpango Mpana wa Umoja wa Mataifa
kuhusu siasa, amani, usalama na maendeleo katika DRC na eneo la Maziwa
na matarajio kuhusu mazungumzo ya Kampala ( Kampala Talks)
**********
Na Mwandishi
Maalam
Baada ya kundi
la waasi la M23 kudhibitiwa ipasavyo na Jeshi la Umoja wa Mataifa linalotuliza
amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ( MONUSCO) na ambalo ndani yake kuna Brigedi Maalum ( FIB). Jeshi hilo sasa
linaelekeza nguvu zake katika kulishughulika
kundi jingine la FDLR.
“ Nilipata
fursa leo ( jumatano) ya kutoa taarifa
mbele ya Baraza Kuu la
Usalama kuhusu maendeleo ya kijeshi na kisiasa katika DRC. Kwa upande wa kijeshi, baada ya
mapigano yaliyopelekea kudhibitiwa kwa kundi la M23 sasa MONUSCO
imeelekeza nguvu zake kwa
makundi mengine ya waasi na kwa
kuanzia tumeanza na kundi la FDLR ( Democratic forces for the liberation of
Rwanda)”
Hiyo ni kauli na
Bw. Martin Kobler Mwakilishi
Maaluma wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa
MONUSCO.
Alikuwa akiwaeleza waandishi wa habari mara tu baada
ya yeyé na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika Eneo la
Maziwa Makuu, Bi. Mary Robison kumaliza
kutoa taarifa zao mbele ya Baraza Kuu la Usalama lililoketi katika mkutano wake wa ndani uliofanyika siku ya
Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
“Tulianza kulishughulikia kundi la FDLR Novemba 27, na kati ya jana na juzi ( disemba tisa na kumi)
kumekuwapo na hatua kubwa
zinazofanyika za kusafisha maeneo na mitaa muhimu ambayo inashikiriwa na FDLR. Tunaendelea na kazi hii ambayo ni muhimu sana ya kupambana na makundi
yote ya waasi likiwamo hilo la FDLR pamoja na kundi
jingine la ADF ( Allied
Democratic Forces )ambalo lilo katika
eneo la Magharibi sana”. Akasema Bw. Kobler
Akasema
kuanzia hiyo novemba 27 na
siku za hivi karibu baada ya eneo
la Pinga ambalo kwa miaka miwili lilikuwa mikononi mwa FDRL makundi mengine ya waasi
wakiwamo wababe wa kivita , hivi sasa na baada ya kukombolewa na njia kufunguliwa kwenda Goma,
wananchi sasa wanaweza kusafirisha bidhaa zao na kuwatembelea ndugu zao.
Na kuongeza “ Leo nimeleta ujumbe wa matumaini mbele
ya Baraza Kuu la Usalama . Nadhani hali sasa ni tofauti katika DRC na hasa baada ya kumaliza mapigano dhidi ya kundi la M23”.
Akabainisha kwamba
maeneo mengi ambayo yamekombolewa
MONUSCO imeunda ‘visiwa’ vya
uvulivu hali aliyosema imeleta
matumaini makubwa kwa wananchi, matumaini ambayo yanaonekana bayana katika
macho ya wananchi wa maeneo hayo.
Hata hivyo Bw.
Kobler aliyekuwa amefuatana na Bi. Mary
Robison amesema bado kuna hati hati lakini kuna fursa pia, fursa ya kwamba baada ya mafanikio haya yote hali
haiwezi kurejea tena kule tulikotoka na hatuwezi katika miaka michache
ijayo kuanza tena mapigano.
Akafafanua zaidi kwamba nguvu za kijeshi peke
yake hazitaweza kulifanya eneo la
Mashariki ya Kongo kuwa na amani na utulivu wa kudumu kwa kile alichosema,
utashi na ushiriki kutoka kwa wananchi wa eneo
hilo ni jambo linalohitajika
sana.
Akaeleza zaidi kwamba wananchi wenyewe wanatakiwa kushiriki katika utatuzi wa vyanzo ambavyo vimekuwa vikisababisha
mapigano na machafuko ya mara kwa mara
akitaja vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na
kupigania utajiri mkubwa wa
madini ambao nchi hiyo imejaliwa.
“ Kwa
kushirikiana na wananchi tunahitaji kufanya kazi pamoja na kuyashughulikia matatizo yote
yanayochangia migogoro na machafuko,
vinginevyo mafanikio ya kijeshi ambayo
yamepatika hivi karibuni yatakuwa hayana maana yoyote na tutarejea kule tulikotoka” akasisitiza.
Aidha Mkuu huyo
wa MONUSCO amewambia waandishi hao wa habari kwamba pia amelieleza Baraza Kuu la Usalama kuhusu umuhimu wa mchakato wa waasi kujisalimisha mchako unaohusisha pia upokonyaji wa silaha, usambarishaji wa makundi ya waasi na uunganishwaji wa waasi hao katika jamii (
DDR).
Amesisitiza kwamba mchanto huo wa DDR ni muhimu sana
hasa kutoka na dalili za kwamba watu hawaoni tena thamani ya
kuendelea na mapigano. “ wanataka kurejea uraiani na kuishi maisha ya kawaida na huu ni muelekeo mzuri na muhimu
hatuna budi kuitumia fursa hii na hasa katika kuwapa matumaini mapya vijana”.
Akafafanua zaidi kwa kusema kwa mfano asilimia 70 ya watu katika DRC ni vijana wa umri wa miaka
17 ambao anaamini kwamba wanataka kuwa na maisha bora yenye amani, utulivu na
maendeleo.
Akaongeza kuwa baadhi ya wapiganaji wa kundi la FDLR
na ambao wengi wao umri wao ni chini ya miaka 30 na wamezaliwa baada ya
mauaji ya kimbari wanataka sana
kujisalimisha na kwamba katika
miezi ya hivi karibu wamekuwa wakijisalimisha bila ya mapigano yoyote.
0 comments:
Post a Comment