Na Mwandishi Wetu
BINGWA wa dunia wa mbio za
marathon, Edna Ngeringwony Kiplagat (pichani ) wa Kenya amejitokeza kushiriki zile za
Uhuru Marathon zinazotarajiwa kufanyika jijini Dar ers Salaam Desemba 8, mwaka
huu.
Katibu wa Kamati ya Uhuru
Marathon, Innocent Melleck alisema, wamefarijika kwa kiasi kikubwa kwa Edna
mwenye sifa lukuki katika mbio za marathon kujitokeza kushiriki.
“Kwetu tumefarijika mno
kutokana na ushiriki wa Edna, kwani ni mwanariadha wa kimataifa mwenye rekodi
nyingi za kuvutia na hasa hii ya ubingwa wa dunia kwa upande wa wanawake,”
alisema.
Edna,34, alitwaa ubingwa
wa dunia kwa upande wa marathon mwaka 2011 katika mashindano yaliyofanyika
Daegu, Korea Kusini na akafanya hivyo tena mwaka huu katika mashindano ya dunia
yaliyofanyika Moscow, Urusi.
Pia alishinda katika mbio
za Los Angeles Marathon na New York Marathon zilizofanyika mwaka 2010 na muda
bora zaidi kupata kuuweka katika mbio hizo ni wa saa 2:19:50 katika mbio za
London Marathon mwaka jana.
Pia ametwaa medali
mbalimbali katika mashindano ya vijana wakati anaanza kukimbia mwaka 1996, pale
alipoonyesha uwezo wake katika mashindano ya dunia kwa vijana.
Melleck alisema, umuhimu
wa mbio hizo unaonekana zaidi kwani watu wengi wanazidi kujitokeza kushiriki
nab ado fomu za usajili zinaendelea kutolewa.
Alisema, katika usajili
huo, mshiriki wa kilomita 3 atalipa Sh 100,000 yule wa kilomita 5 Sh 2,000 na
washiriki wa kilomita 21 na 42 watalipia Sh 6,000.
“Pia tunapenda kuchukua
fursa hii kuziomba kampuni au taasisi mbalimbali zinazotaka kudhamini mbio hizo
zijitokeze na kufanya hivyo, kwani nafasi bado ipo na tukumbuke bila amani
hakuna chochote kinachoweza kuendelea, hivyo hata wao pia wanatakiwa kuipigania
amani kwa nguvu zote.”
Mbio hizo zinatarajiwa
kuanza na kumalizikia katika Viwanja vya Leaders, vilivyopo Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment