Napenda
kuujulisha umma kwamba Ijumaa tarehe 4 Oktoba, 2013 niliwasilisha kwa
Katibu wa Bunge muswada binafsi Bungeni kufuta Sheria ya Magazeti ya
mwaka 1976.
Changamoto
iliyopo ni Sheria mbadala ya vyombo vya habari baada ya Sheria ya sasa
kufutwa. Hata hivyo wadau wa habari kama Baraza la Habari Tanzania
wameshafanyia kazi suala hili kwa muda mrefu sana na wana mawazo kuhusu
sheria mbadala.
Nimejulishwa
kuwa muswada wa sheria mpya ya habari tayari upo. Kwa hiyo katika
mchakato wa kujadili muswada binafsi wa kufuta sheria ya magazeti ya
mwaka 1976 mabadiliko yanaweza kufanywa ili kutunga sheria mpya. Hatua
ya kwanza ni kuifuta sheria hii kandamizi ambayo kiukweli tumechukua
muda mrefu sana na baada ya madhara makubwa kufikia hatua ya muswada wa
kuifuta.
Nimeamua
kutumia njia za kawaida za kuwasilisha muswada na kuepuka njia ya
dharura ili kujenga mazingira ya wadau wa habari kushiriki vya kutosha
katika mabadiliko yanayotakiwa. Njia ya dharura ni ya haraka lakini
huziba fursa za kupata maoni ya wadau ambao kimsingi ndio wenye sheria
yenyewe haswa.
Hivyo
nimepeleka muswada leo ili uchapwe kwenye gazeti la Serikali (GN) kwa
mujibu wa kanuni za Bunge, kisha usomwe kwa mara ya kwanza, uende kwa
wadau kwa mjadala na marekebisho na kisha kusomwa kwa mara ya pili na
kupitishwa na Bunge.
Ikumbukwe
kuwa juhudi za kufuta sheria hii ni juhudi za wadau wa tasnia ya habari
na ni juhudi walizofanya kwa muda mrefu sana. Mimi kama Mbunge
ninawasilisha tu kwa sababu taratibu zetu za kuandika sheria zinataka
ama Serikali, Kamati ya Bunge au Mbunge kuwasilisha muswada. Kwa muda
mrefu tumewaangusha wana habari kwa kutosukuma vya kutosha mabadiliko
waliyokuwa wanayapigania. Hata hivyo, kuna msemo wa kihindi 'asubuhi
huanza pale unapoamka'. Sasa tuchukue hatua za kufuta sheria hii
kandamizi.
Zitto Kabwe,Mb
Kigoma Kaskazini
0 comments:
Post a Comment