Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Septemba 6, 2013,
amefungua shule ya kisasa ya msingi ya Ntulya katika kata ya Mondo, Wilaya ya
Misungwi, iliyotolewa kama zawadi kwa wanakijiji cha Ntulya na taasisi moja ya
Marekani.
Aidha, Rais Kikwete amezindua
huduma za x-ray kwenye Hospitali ya Wilaya ya Misungwi mjini Misungwi ikiwa ni
hatua zake za mwanzo kwenye siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya Rais Kikwete
katika mkoa wa Mwanza ambako atakaa siku tano akikagua na kuzindua miradi na
shughuli za maendeleo.
Shule ya Ntulya iliyoko
kilomita 47 kutoka mjini Misungwi ina wanafunzi 466 na walimu 11 na ni zawadi
ya Taasisi ya Africa School House ya Marekani kwa wanakijiji cha Ntulya ambako
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt. Aimee Bessire ambaye
amehudhuria sherehe za uzinduzi wa shule hiyo na mume wake, Mark Bessire
walipata kuishi wakifanya utafiti kuhusu utamaduni wa Kabila la Wasukuma.
Shule hiyo ya kisasa imejengwa
kwa matofali ya kuchomwa na ilijengwa kati ya 2008 na 2010. Ina madarasa 11,
nyumba 10 za walimu na kisima cha maji safi. Kwa jumla shule hiyo ina uwezo wa
kuwa na wanafunzi 600 kwa wakati mmoja.
Akizungumza kwenye sherehe za
leo, Dkt. Bessire ambaye amezungumza kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kiswahili
na Kisukuma, amesema kuwa shule hiyo imejengwa kwa jumla ya sh bilioni 1.038,
na kati ya hizo sh milioni 980 zilitolewa na Africa School House, Halmashauri
ya Misungwi ilichangia sh milioni 28 na nguvu za wananchi zilichangia sh
milioni 30.
Taasisi hiyo ya Marekani pia
imewajengea wanakijiji hao wa Ntulya Kituo cha Afya kwenye eneo hilo la shule
na Dkt. Bessire amesema kuwa Taasisi hiyo ina mipango ya kujenga shule ya mfano
ya sekondari ya bweni ya wasichana.
Dkt. Bessire pia amesema kuwa
yataanzishwa madarasa kwenye shule hiyo kwa ajili ya watu wazima wasiojua
kusoma na kuandika.
0 comments:
Post a Comment