Nafasi Ya Matangazo

September 27, 2013

Na Asteria Muhozya, Mafia
Halmashauri nchini zimetakiwa kuendelea kutenga asilimia tano ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya kuchangia mfuko wa Maendeleo ya wanawake ili kuwawezesha wanawake wengi zaidi kupata mikopo yenye masharti nafuu kupitia mifuko hiyo

Hayo yamesema na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati akihitimisha ziara yake Mkoa wa Pwani katika Wilaya ya Mafia.

Mhe.Ummy ameongeza kuwa, maendeleo katika nchi na jamii yoyote yanaanza na wanawake na kwamba mwanamke akiwezeshwa na kuonyeshwa fursa za kujikomboa kiuchumi anaweza kuleta mabadiliko makubwa katika familia na jamii nzima, hivyo ni wajibu wa halmashauri kuwawezesha wanawake kiuchumi.

“Hili ni agizo la Waziri Mkuu kuhakikisha kuwa halmashauri zinatenga fedha za mfuko wa maendeleo ya wanawake kila mwaka kutoka katika mapato ya ndani. alisema”.

Aidha, ameongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara yake pia itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya mfuko huo kwa Halmashauri zote nchini na kwamba katika mwaka wa fedha 2013/2014 tayari serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni mbili kwa ajili ya mfuko huo.

Wakati huo huo, Mhe.Ummy, amewataka Maafisa maendeleo ya Jamii nchini kushirikiana na wananchi walio katika maeneo yao kwa kuwahamasisha kutambua na kuzitumia fursa zinazowazunguka ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo. Hivyo amewataka maafisa hao kuwasaidia wananchi kupata taarifa zitakazowawezesha kujua namna ya kupata masoko ya kuuza bidhaa wanazozizalisha ikiwemo elimu ya ujasiliamali na taarifa ya uwapo wa vyanzo vya mikopo, huku akitolea mfano wa Benki ya Wanawake Tanzania.

“ Nyie ndio wahamasishaji wakubwa ambao mnafungua njia za maendeleo kwa wananchi, zitumieni taaluma zenu kuwawezesha wananchi kubadilika na kubadili fikra na mitazamo yao ili kujiletea maendeleo yao” amesema.

Akizungumzia kuhusu upungufu wa Maafisa Maendeleo ya Jamii Katika Wilaya, Mhe Ummy amewataka watendaji wa halmashauri nchini kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda la kuhakikisha wana ajiri maafisa maendeleo ya jamii katika kila kata nchini ili waweze kuwasaidia wananchi kujiletea maendeleo yao, familia na Taifa kwa ujumla.

Akizungumzia kuhusu suala la mimba za utotoni baada ya kufanya majadiliano na wasichana wa shule ya Sekondari ya Kitomondo amewataka wasichana hao kujibidiisha katika masomo yao licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili. Aidha, amewaeleza kuwa, ni elimu pekee itakayowakomboa na umaskini na utegemezi na si vinginenavyo, hivyo amewataka kukabiliana na changamoto hizo bila kukatishwa tamaa na mtu yeyote ikiwa ni pamoja na walezi na wazazi.

“Najua kuna baadhi ya wazazi na walezi wanawakatisha sana tamaa watoto wa kike kuendelea na masomo katika shule za sekondari, nawaomba wasichana msikubali kukatishwa tamaa , someni na zingatieni masomo kwani elimu mkombozi wenu pekee atakaewaletea mwanga bora katika maisha yenu” ,amesema. Aidha, Mhe Mwalimu amewaagiza viongozi katika ngazi za wilaya, kata na vijiji kuhakikisha watoto wote wa kike waliomaliza darasa la saba hawaozeshwi kabla ya matokeo ya mitihani hiyo kutolewa.

Vilevile amewataka wanafunzi wanaomaliza darasa la saba nchini kuvitumia Vyuo vya maendeleo ya Wananchi kwa ajili ya kujipatia stadi na ujuzi mbalimbali utakaowasaidia katika maisha yao. Ameeleza kuwa tayari serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imeanza utekelezaji wa kuviboresha vyuo 25 vya Maendeleo ya Wananchi ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata elimu ya ufundi kupitia vyuo hivyo.

Akizingumzia kuhusu ukatili kwa watoto ameeleza kuwa, suala hilo bado ni tatizo kubwa katka jamii na hivyo ameitaka jamii kuhakikisha kuwa watoto wote wanalindwa . vilevile jamii imeaswa kuyatumia madawati ya Jinsia ambayo yameanzishwa katika vituo vya polisi nchini kuripoti habari za ukatili ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Katika ziara yake ya kikazi ya wiki moja mkoani Pwani, Mhe Mwalimu ametembelea Wilaya za Kisarawe, Mkuranga, Rufiji na Mafia ili kufuatilia utekelezaji wa sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996, sera ya Maendeleo ya wanawake na Jinsia ya mwaka 2000, Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya 2008 na Sera ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001.
Posted by MROKI On Friday, September 27, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo