Mkuu
wa Jeshi la Polisi la Tanzania IGP Said Mwema akimkabidhi kitara Mkuu wa Jeshi
la Polisi la Namibia Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga kama ishara ya
kumkabidhi uenyekiti wa Shirikisho la wakuu wa Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO)
baada ya Tanzania kumaliza uongozi wake kwa kipindi cha mwaka
mmoja.Makabidhiano hayo yalifanyika wakati wa mkutano maalumu wa wakuu hao
uliofanyika nchini Namibia.
|
Inspekta
Jenerali wa Polisi wa Tanzania IGP Said Mwema amekabidhi uenyekiti wa
Umoja wa wakuu wa majeshi ya Polisi kwa nchi za kusini mwa Afrika
SARPCCO baada ya kumaliza kipindi chake cha mwaka mmoja cha kuongoza
umoja huo.
IGP
Mwema amekabidhi uongozi huo kwa Inspekta Jenerali wa Polisi wa Nchi ya
Namibia Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga wakati wa mkutano mkuu
maalumu wa viongozi hao uliofanyika jana katika jiji la Windhoek na kuhudhuriwa na Wakuu wa Polisi kutoka nchi wanachama pamoja na viongozi mbalimbali kutoka INTERPOL na SADC.
Akizungumza
katika mkutano huo IGP Mwema alisema katika kipindi cha uenyekiti wake
walifanikiwa kufanya Operesheni kubwa iliyojulikana kama Operesheni
Usalama ambayo ilijumuisha umoja wa SARPCCO na ule wa Afrika Mashariki
EAPCCO,operesheni ambayo ililitea manufaa makubwa katika kukabiliana na
uhalifu unaovuka mipaka.
Alisema
Nchi wanachama wanapaswa kuendeleza ushirikiano wao ili kuhakikisha
kuwa ukanda wa kusini mwa Afrika unakuwa salama kwa kukabiliana na
uhalifu hasa kwa kupeana taarifa za uhalifu na wahalifu.
Aidha
alisema katika kipindi hicho Tanzania iliweza kuandaa mikutano yote ya
kamati tendaji za SARPCCO ambazo ziliweza kuibua maazimio mbalimbali ya
kupambana na uhalifu ambayo yaliweza kupitishwa na kuwa mikakati
endelevu katika kukabiliana na uhalifu.
Kwa
upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia Luteni Jenerali
Sebastian Ndeitunga alisema atahakikisha umoja huo unakuwa imara na
kupambana na uhalifu unaovuka mipaka kama vile wizi wa magari, wahamiaji
haramu, usafirishaji wa fedha haramu na binadamu, wizi wa mitandao
pamoja na madawa ya kulevya.
Naye
Mgeni rasmi katika mkutano huo Waziri wa Usalama na ulinzi wa Namibia
Immanuel Ngatjizeko alisema serikali ya Namibia itaendelea kushirikiana
na umoja huo kwa kila hali ili kuhakikisha Nchi wanachama na Afrika kwa
ujumla zinakuwa salama.
IGP
Mwema alikabidhiwa uenyekiti wa SARPCCO mwezi Septemba mwaka 2012 mjini
Zanzibar kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Afrika kusini ambapo
kutokana na uenyekiti huo mikutano yote ya umoja huo ilikuwa ikifanyikia
nchini Tanzania.
0 comments:
Post a Comment