Mkurugenzi wa Idara ya Habari
Maelezo, Assah Mwambene (kushoto) akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari
waliohudhuria Mkutano wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika ukumbi wa
Habari Maelezo leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Meneja Habari Elimu na
Mawasiliano wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Sylvia Lupembe na kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa.
***** *****
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika kuendelea kutoa
ruzuku kwa taasisi za elimu kwa lengo la kuongeza ubora katika utoaji elimu,
pamoja na miradi mingine imelenga kupanua wigo wa elimu jumuishi kwa ngazi
mbalimbali za elimu nchini.
‘Elimu jumuishi’ ni ile inayotambua mahitaji tofauti ya
kujifunza ya wanafunzi ili kuhakikisha wanawekewa mazingira bora yenye kukidhi
mahitaji yao. Tanzania inatekeleza utaratibu huu baada ya kuridhiria mpango wa
utekelezaji Elimu Maalum wa Salamanca mwaka 1994. Mpango unasisitiza kuwa watoto wote wajifunze kwa
pamoja kadri inavyowezekana, bila kujali tofauti za kijiografia, maumbile,
jinsia, uwezo wa kiakili. Changamoto ni
kuhahakikisha kuna vifaa vya kutosha kukidhi mahitaji hayo.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imesaidia kuongeza wigo
wa utekelezaji wa mpango huu kwa kutoa vifaa mbalimbali vya kujifunzia na
kufundishia wanafunzi wenye mahitaji maalum na vifaa saidizi. Jumla
ya taasisi 119 tayari zimeshafaidika na
wanafunzi 3,114 wamenufaika na vifaa hivyo.
Aidha misaada iliyotolewa ni pamoja na:-
(a) vifaa
saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu kama fimbo nyeupe, vifaa vya kuongeza
usikizi, miwani mafuta maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi
(b) vifaa vya
kujifunza na kufundishia kama mashine za maandishi ya nukta nundu, vifaa vya
TEKNOHAMA kama kompyuta maalum kwa wasioona, mashine ya kutoa machapisho kwa
nukta nundu, vitabu vya kiada vya lugha za alama.
(c) Ukarabati
au ujenzi wa miundo mbinu kama madarasa, mabweni ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi
wenye ulemavu;
(d) Kuboresha
mazingira ya vyuo vya mafunzo ya walimu wa elimu maalum.
Kati ya mwaka 2011
hadi 2013, TZS 1,000,940,140.00 zimetumika
kugharamia ununuzi wa vifaa hivyo na
kuvisambaza. Baadhi ya taasisi zilizonufaika ni pamoja na Chuo cha ualimu
patandi- Arusha , Buigiri- Dodoma , Njia panda- Kilimanjaro, Katesh- manyara na
Maisaka Bariadi.
MPANGO ENDELEVU
Utoaji wa vifaa
saidizi na vya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, bado ni kipaumbele TEA na katika mwaka fedha 2012/13
tumetafuta wafadhili ili kwa pamoja tuweze kutoa msaada wa vifaa vya TEKNOHAMA
kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu katika Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania na Chuo
cha ualimu Patandi. Mpango huu utasaidia kuongeza idadi ya waalimu wenye ujuzi
wa elimu maalum.
Aidha kwa upande mwingine, Mamlaka pia imejikita katika
kujenga hosteli za wasichana katika shule za sekondari za kata. Jumla ya
hosteli 30 zinatarajiwa kujengwa katika shule 8 kwa awamu ya kwanza kuanzia
mwaka huu wa fedha . Hosteli hizo zitahudumia wanafunzi wa kike 1,504.
Mradi huu utagharimu jumla ya TZS
bllioni 2.3. na utawezesha kuongeza
uwiano wa kijinsia katika shule za sekondari.
MAMLAKA YA ELIMU
TANZANIA (TEA)
TEA ina jukumu la kuhamasisha jamii kushiriki kuchangia maendeleo
ya sekta ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu na kufadhili miradi ya elimu. Tunatambua jukumu la kuhakikisha
upatikanaji wa Elimu bora letu sote
kila mmoja wetu kwa nafasi yake. Watanzania mmoja moja, makampuni, mashirika tunaomba
muendelee kuchangia Mfuko wa Elimu ili kuisadia serikali kutimiza lengo la utoaji
elimu bora kwa kila mtanzania .
0 comments:
Post a Comment