Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa akizungumza wakati wa majadilino yaliyohusu namna ya kuingiza suala la wazee katika ajenda mpya za Maendeleo baada ya mwaka 2015.
Mkutano huo ulioambatana na chakula cha mchana ulifanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na ulioandaliwa na United Nations Foundation kwa kushirikiana na Mashirika mengine ya Kimataifa. katika mchango wake, Mhe. Lowassa amesisitiza umuhimu wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika kuzikabili changamoto za ongezeko la idadi ya wazee duniani.
Inasemekana miaka michache ijayo idadi ya wazee duniani itazidi idadi ya watoto wadogo chini ya miaka mitano. Pamoja na Mhe. Lowassa wengine waliochangia majadiliano hayo ni Bi. Ann Pawliczko kutoka UNFPA wa pili kutoka kushoto, Bw. Jack T. Watters kutoka Pfizer, Bw. Paul Ong HelpAge International, Bw. Sharig Khoja kutoka United Nations Foundation, aliyeketi karibu na Mhe. Lowassa ni Bi. Jane Barratt aliyeratibu majadiliano hayo.
Sehemu ya washiriki wa majadiliano hayo wakiwamo pia Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa
Mhe. Lowassa akipeana mkono na mmoja wa waandaji wa majadiliano hayo kuhusu Wazee, takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu ( UNFPA) zinazonyesha kwamba mwaka 1950 idadi ya wazee duniani waliokuwa na miaka 60 au kuzidi ilikuwa milioni 205, 2012 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia 810 milioni. Inakadiriwa kwamba idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia Bilioni 1 si zaidi ya miaka kumi ijayo na ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea itafikia bilioni 2. Aidha duniani kote wanawake ndio wanaokadiriwa kuishi umri mrefu zaidi kuliko wanaume.
Mhe. Edward Lowassa akibadilishana mawazo na Balozi wa Zimbabwe katika Umoja wa Mataifa, Bw. Chitsaka Chipaziwa
Na Mwandishi Maalum
Mwenyekiti wa Kamati
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Edward
Lowassa ( Mb) amesisitiza haja na umuhimu wa kuwapo kwa ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika
kuzikabili changamoto zinazotokana na ongezeko
kubwa la idadi ya wazee.
“ Maisha Zaidi ya
miaka 60 hayapashwi kuwa ya utegemezi, unyonge, kutojiweza au kutokuwa na
matumaini. Wazee bado na wanao
mchango mkubwa ndani ya
jumuiya, jamii, na familia
zao ili mradi tu wawezeshwe”.
Na kwa sababu hiyo
anasema Mhe, Lowassa, juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika
nchi zilizoendelea na zinazoendelea Tanzania ikiwamo za utoaji wa huduma za msingi
kama vile Afya , pensheni na uwezeshwaji
zinapashwa kuchagizwa na sekta binafsi.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Mambo ya Nje, na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa(Mb ), ameyasema
hayo siku ya jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wakati
aliposhiriki majadiliano kuhusu namna gani suala la Wazee linavyoweza kuingizwa katika ajenda za
maendeleo baada ya mwaka 2015.
Majadiliano hayo yaliandaliwa na United
Nations Foundation kwa ubia na International Federation of Ageing, Help Age International, AARP, Global Coalition on Aging, mHealth
Alliance na Pfizer
“Kama kundi hili la
wazee likiwezeshwa na kusaidiwa ipasavyo , linaweza kuipatia jamii soko
jipya, ujasiriamali, utoaji wa maamuzi, utoaji wa huduma na utalaamu anuai katika maeneo ya sayansi, teknolojia
na upatanishi” anasema Lowassa
Na kuongeza, ili hayo
yote na mengine mengi yaweze kufanikiwa panahitajika bajeti ya kutosha kwa ajili ya kundi hilo la jamii ikiwa ni
pamoja na kuimarisha mifumo ya pensheni,
huduma za afya ambazo zitakidhi mahitaji ya wazee, huduma za kisaikolojia na
huduma za ulinzi jamii,.
Hata hivyo anasema,
inasikitisha kwamba, katika nchi nyingi za Afrika na nyinginezo hata zile
zilizoendelea bado haziwezi kutoa huduma
za uhakika na zenye viwango vya kukidhi mahitajio ya wazee.
“Mara nyingi huduma
kwaajili ya wazee inabidi zishindane na huduma za makundi mengine kama
vile ongezeko la vijana wasiokuwa na
ajira, upunguzaji wa vifo vya watoto wachanga na wanawake
wajawazito. Hata hivyo pamoja na changamoto zote hizi za vipaumbele hatuwezi
kuendelea na utaratibu huu wa kuchagua. Lazima tutumie maandalizi ya ajenda za maendeleo baada ya 2015 kuwahudumia
wazee” anasisitiza Lowassa.
Akasema Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa kujikumbusha na
kujifunza kwa kosa la kutoingiza suala la Wazee katika utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) yanayoelekea ukingoni, kwa kuhakikisha kwamba Wazee wanaingizwa
katika malengo mapya ya maendeleo baada
ya 2015 kwa kuwa ni suala ambalo haliepukiki
Akizungumzia hatua mbalimbali zinazochuliwa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwahudumia wazee, Mhe.
Lowassa anasema kama ilivyo kwa nchi
nyingine, Tanzania nayo inakabiliwa na ongezeko la idadi ya wazee.
Kwa mfano, amesema asilimia 4.5 ya idadi ya watu, ni
watu walio na umri wa miaka 65 wastani
wa juu zaidi kuliko ule wa
asilimia 3.6 Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“ Asilimia 80 ya
watu hawa wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea kilimo.
Serikali inajitahidi kadri iwezavyo
kutoa huduma za msingi kwa kundi hilo ingawa pia, na kama ilivyo kwa nchi nyingine,
tunakabiliwa na changamoto nyingi kukidhi mahitaji yote ya wazee”. Akabainisha
Akatumia pia fursa hiyo kuyashukuru mashirika ya
kimataifa kama vile Help Age International ambalo limekuwa likiendesha shughuli
zake nchi nchi tangu mwaka 1993.
Akatoa mfano kwa kusema Shirika hilo,
mwezi Juni mwaka huu kwa
kushirikia na Pfizer limezindua mpango wa miaka miwili wa kupunguza athari zitokanazo na magonjwa yasiyoambukiza (NCD) ambayo yamekuwa
yakiwaathiri wazee.
Akasema utoaji
wa huduma hiyo unakwenda sambamba na juhudi za serikali katika kukabiliana
na magonjwa hayo.
Akatoa wito kwa mashirika mengine kuiga mfano huo na
kwamba serikali itakuwa tayari kushirikiano nayo,
Takwimu kutoka
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu ( UNFPA) zinaonyesha
kwamba, katika kila sekunde watu wawili
duniani wanaadhimisha miaka 60 ya kuzaliwa kwao, na kwa mwaka karibu watu milioni 58 wanaadhimisha miaka 60
ya kuzaliwa.
Aidha katika kila watu nane, mmoja ana miaka 60 au zaidi na makadirio
yanaonyesha kwamba ifikapo mwaka 2050
katika kila watu watano mmoja atakuwa na
miaka 60 au zaidi.
Ongezeko la
idadi ya wazee duniani linachangiwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na ongezeko la umri wa kuishi ambapo katika nchi
33 raia wao wanaishi zaidi ya miaka 80
wakati miaka mitano iliyopita nchi ambazo
umri wa kuishi ulifika miaka 80
zilikuwa 19 tu.
Utafiti zaidi unaonyesha , umri
wa kuishi utaongezea hadi kufikia miaka 90 au hata miaka 100.
Japani kwa sasa ndiyo inasemekana kuongoza kwa kuwa na asilimia 30 ya wazee lakini ifikipo
mwaka 2050 nchi 64 zitaungana na Japani
kwa kuwa na asilimia 30 au zaidi ya
wazee.
0 comments:
Post a Comment