RAMBIRAMBI MSIBA WA MATHIAS KISSA
Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za
kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Cosmopolitan na Taifa Stars,
Mathias Kissa (84) kilichotokea leo alfajiri (Juni 24 mwaka huu) kwenye
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Msiba
huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani enzi zake, Kissa akiwa
na timu ya Tabora alitamba katika michuano ya Kombe la Taifa wakati huo
ikiitwa Sunlight Cup. Alikuwa akicheza katika nafasi ya ulinzi.
Baadaye
alijiunga na Cosmoplitan ya Dar es Salaam, na pia kuwa mchezaji wa timu
ya Taifa ambapo enzi zake akiwa na wachezaji kama Yunge Mwanansali
wakiiwakilisha Tanganyika na baadaye Tanzania Bara walitamba katika
michuano ya Kombe la Chalenji wakati huo ikiitwa Gossage, hivyo mchango
wake tutaukumbuka daima.
Kissa
ambaye alipata tuzo ya mchezaji bora wa karne kwa upande wa Tanzania,
tuzo inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
alikuwa ndiye mchezaji msomi kupita wote wakati akichezea timu ya Taifa
akiwa amehitimu elimu ya Darasa la Kumi.
Kwa
mujibu wa binti yake, Erica, marehemu ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa
kiharusi (stroke) alioupata miaka mitano iliyopita, na kisukari. Baadaye
alipata kidonda ambacho ndicho kilichosababisha kifo chake.
Msiba
uko nyumbani kwa marahemu, Masaki, Mtaa wa Ruvu karibu na Shule ya
Kimataifa ya Tanganyika (IST). Maziko yatafanyika keshokutwa, Jumatano
(Juni 26 mwaka huu) kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Kisa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Cosmopolitan na kuwataka kuwa na
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Mungu aiweke roho ya marehemu Kisa mahali pema peponi. Amina
0 comments:
Post a Comment