Kwenda
kwa: DR ABDALLAH KIGODA,
Waziri wa Viwanda na Biashara
Kuhusu:
BIASHARA YA MIITO YA SIMU (RINGBACK TONES)
Kumekuwa na malalamiko makubwa sana kuhusu
biashara ya mauzo ya nyimbo kama miito kwenye simu. Malalamiko haya yalianzia
kwa wasanii wenyewe na baadaye mimi binafsi niliwasilisha hoja zao Bungeni
mwaka 2012. Hata hivyo, hadi sasa malalamiko haya bado hayajapatiwa ufumbuzi na
hivyo wasanii kuendelea kunyonywa. Tatizo kubwa katika biashara hii ni USIRI na UNYONYAJI kwa wasanii wa Tanzania. Suala la USIRI lipo Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Suala la Unyonyaji lipo Wizara ya
Viwanda na Biashara.
USIRI
Biashara hii ya “Ring Back Tones” (RBT)
hufanywa na Kampuni za simu (Network providers) kwa kununua maudhui
kutoka wachuuzi (Content Providers) ambao nao huingia mikataba na Wasanii
(Content Creators).
Hakuna sheria yoyote au Kanuni hapa nchini
inayoongoza biashara hii na hivyo “Network providers” na “Content
Providers” kuwa watu pekee wenye taarifa zote za biashara hii. Kampuni za
simu hujumuisha mapato ya biashara hii na mapato yake mengine (Not Ringfenced),
hawatoi taarifa za manunuzi ya nyimbo (au ‘content’ nyingine yeyote) kwa wadau
na hasa wasanii. Wachuuzi (Content Providers) nao hawatoi taarifa
za mauzo kwa wasanii na wanatumia uelewa mdogo wa wasanii
kuwasainisha mikataba inayowanyonya. Matokeo yake ni kwamba msanii hupata
kiasi cha asilimia mbili tu (2.5%) ya mapato ghafi ya kazi yake. Hivi
sasa biashara hii inathamani (turnover) ya takribani shilingi 44 bilioni kwa
mwaka.
Suluhisho:
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano
iandike kanuni (regulations) zitakazolazimisha makampuni ya simu kuweka wazi
mapato yatokanayo na biashara ya RBT (Miito ya simu) kila baada ya miezi 4
(disclosure rules). Kanuni hizi zielekeze makampuni kutoa taarifa za
mauzo kwa kila kazi (nyimbo/vichekesho etc.)
UNYONYAJI
Kutokana na usiri ulioelezwa hapo juu,
wasanii wamekuwa wakinyonywa kimapato. Kwa mfano Msanii hulipwa
mapato yatokanayo na ununuzi wa awali wa kazi yake (wimbo) katika mwezi
(downloads).
Lakini mapato yatokanayo na “subscriptions”
ambapo mlaji hukatwa shilingi 30 kila siku msanii hapati chochote. Hivyo
katika mapato ya sh. 1,300 kila mwezi kwa kila mteja kwa kila wimbo, msanii
hupata mgawo wake kutoka shilingi 400 tu za ‘downloads’ na ndio maana wasanii
wote nchini hupata 2.5% ya shilingi 44 bilioni zinazokusanywa na Kampuni za
Simu.
Nchini Marekani biashara ya miito ya simu
(RBT) imetafsiriwa kama maonyesho (Public Performances) na hivyo
“copyright Association” ya Marekani imeweka kiwango cha chini cha mrahaba
(royalty) ambacho msanii hulipwa. Marekani msanii hulipwa asilimia 10 ya
patoghafi linalozalishwa na kazi yake kama muito wa simu.
SULUHISHO
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na
Biashara iandike kanuni kwamba mauzo ya kazi za wasanii kama miito ya simu
inachukuliwa kama ‘performance’ na kwamba Kampuni za simu zitalipa sio chini ya
asilimia 12 (12%) ya mapato ghafi, ambapo asimilia 10% itakwenda kwa
msanii na asilimia 2% COSOTA kwa ajili ya usimamizi na Ulinzi wa kazi za
Wasanii.
HITIMISHO
Kanuni za Uwazi (disclosure rules) katika
biashara hii ya ‘Ring Back Tones’ na mgawo wa haki wa mapato (fair and just
revenue share) ndio suluhisho endelevu na litakaloleta tija kwa wasanii wa
Tanzania na hata Serikali kukusanya mapato stahili. Kanuni (Regulations)
zinazopendekezwa zianze kutumika kuanzia tarehe 1/7/2013
Kabwe
Z. Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini
Dodoma, 13 Mei 2013.
0 comments:
Post a Comment