Nafasi Ya Matangazo

January 16, 2013

Waziri Simba akiangalia baadhi ya vyerehani viwili viliyotolewa na Lions kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wajane. Vyerehani hivyo ni kati ya 100 vitakavyotolewa na Lions kuwawezesha wanawake kujikimu kimaisha.
*****
Na Usu-Emma Sindila na Sakina Mfinanga
 Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto Mhe.Sophia Simba  amekabidhi msaada wa vyerehani  viwili kati ya 100 vilivyotolewa kwa wanawake  wajane wa Mkoa wa  Dar es Salaam  ofisini kwake leo kutoka Taasisi ya Lions Club.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi  vyerehani hivyo, Gavana wa Lions Ukanda wa Tanzania na Uganda, Ndg. Joseph Kiwanuka, amesema taasisi yao imekuwa mstari wa mbele kuisaidia jamii hasa wanawake na watoto, kuboresha huduma za maji kwa kuchimba visima ambavyo huwasaidia wananchi hasa wanaokaa sehemu zenye shida ya maji.

Amesema Lions imekuwa ikisaidia watoto wenye matatizo ya moyo kuwapeleka nchini India kwa ajili ya matibabu,kuwasaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kuwapeleka shule hasa zile za awali na wameanzisha mkakati wa kuwaelimisha wanafunzi mashuleni kuhusu utumiaji wa madawa ya kulevya ili watoto wasijihusishe na vitendo hivyo.

Kwa upande wake Waziri Simba ameishukuru taasisi ya Lions kwa misaada mbalimbali ambayo wamekuwa wakiisaidia jamii na zaidi kwa msaada huo wa vyerehani kwa wajane kwa kuwa utawawezesha kujikwamua kimaisha wao wenyewe,  watoto na familia zao.

Aidha, Waziri Simba amewapongeza Lions kwa kazi kubwa wanayofanya kupitia mradi wao wa kuelimisha wanafunzi juu ya madhara ya utumiaji wa dawa za kulevya na kuongeza kuwa Serikali inafanya jitihada kuhakikisha kila kata inakuwa na shule ili kusaidia kupunguza wimbi la watoto wasiojua kusoma na kuandika.
Posted by MROKI On Wednesday, January 16, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo