Mhe.
Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, akitoa msimamo wa Tanzania kuhusu vitendo vya kikundi cha
waasi cha M23 kilichopo Mashariki mwa Congo DRC. Kushoto ni Balozi
Simba Yahya.Picha zote na Tagie Daisy Mwakawago.
Na ALLY KONDO SEIF
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb)
amelaani kitendo cha kikundi cha M23 kuteka mji wa Goma na kutishia
kuteka miji mingine ya Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC). Mhe. Waziri alitoa msimamo huo wakati alipozungumza na Waandishi
wa Habari jijini Dar es Salaam tarehe 22 Novemba, 2012.
Mhe.
Waziri alisema kuwa hali ya usalama mjini Goma ni mbaya kutokana na
mashambulizi hayo ya M23 na hali hiyo ikiachwa iendelee, Tanzania
itaathirika kwa kiasi kikubwa kwani watu wengi watakimbilia hapa nchini
kama wakimbizi.
Aidha,
Mhe. Waziri alisikitishwa na kikundi cha M23 cha kupuuza wito uliotolewa
na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
na Sekretarieti ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) wa kusitisha mapigano
hayo.
Mhe.
Waziri aliendelea kueleza kuwa Tanzania inasikitishwa na jeshi la Umoja
wa Mataifa la MONUSCO lililopewa jukumu la kulinda amani Mashariki ya
DRC kwa kushindwa kuchukuwa hatua za kukomesha mashambulizi hayo na
badala yake kuwa mashuhuda wa mashambulizi yanayofanywa na kikundi cha
M23 dhidi ya Serikali na wananchi wa kawaida.
Aliuomba
Umoja wa Mataifa utoe mamlaka ili MONUSCO iwe na uwezo wa kisheria wa
kukabiliana na waasi wa M23 kama sura ya 7 ya Umoja wa Mataifa
inavyoelekeza badala ya kutumia sura ya 6 ya Umoja wa Mataifa
inayosisitiza umuhimu wa kulinda amani bila kujibu mashambulizi.
Kuhusu
jitihada zinazofanywa na SADC kwa kushirikiana na ICGLR za kutafuta
suluhu ya kudumu ya mgogoro huo, Mhe. Membe alisema kuwa mwezi Agosti,
2012 Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hizo walikutana mjini Kampala, Uganda na
kuamua kuunda kikosi cha kulinda amani ili kitumwe Mashariki ya DRC.
Tanzania iliahidi kuchangia batalioni moja lakini kikosi hicho cha
kulinda amani hakijapata ridhaa ya Umoja wa Mataifa.
Umoja wa
Mataifa hautaki kutoa ridhaa ili kikosi hicho kipelekwe DRC kwa hoja
kuwa tayari jeshi la Umoja wa Mataifa lipo nchini DRC.
Mhe.
Waziri alihitimisha Mkutano wake kwa kutoa taarifa kuwa nchi za SADC na
ICGLR zitakuwa na mkutano nchini Uganda kuanzia siku ya Ijumaa tarehe 23
Novemba, 2012 kujadili hatua za haraka za kuchukuwa ili kukabiliana na
mzozo wa DRC.
0 comments:
Post a Comment