Pichani,
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SHIRIKA la Posta Tanzania, Dr.
Yamungu Kayandabila (katikati) na Postamasta Mkuu Bw. Deos Mndeme
(kushoto) wakipokea cheti maalum kuashiria kufikia viwango vya utoaji wa
huduma bora za kimataifa za Posta. Anayekabidhi cheti ni Mkurugenzi
Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani Bw. Eduard Dayan.
======= ======= ======.
Viwango
vya huduma zinazotolewa na SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC), vimekidhi
viwango vya Shirika la Umoja wa Posta Duniani (Universal Postal
Union-“UPU”).
UPU leo
imetoa cheti maalum kwa Shirika la Posta Tanzania kuwa miongoni mwa
Mashirika wanachama waliofikia viwango vya juu vya utoaji wa huduma za
Posta kwa Tanzania na nchi zote zinazoshirikiana na TPC kwa huduma za
Posta kote ulimwenguni. Shirika la Posta limepata alama 1,765 kati ya
alama 2000 zinazotakiwa, ambazo ni za juu kulinganisha na nchi zingine.
Kamati ya
UPU inayosimamia Masuala ya Upimaji wa Ubora wa Huduma (Quality of
Service Improvement Group Steering Committee) iliridhika na kasi,usalama
na ufuatiliaji wa huduma za kusafirisha barua,nyaraka na vipeto
zinazotolewa na Shirika la Posta Tanzania.
Cheti
hicho cha kuthibitisha Ubora wa Huduma zinazotolewa na TPC,
kilikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta
Tanzania Dr. Yamungu Kayandabila leo jijini Doha, Qatar mbele ya Mkutano
Mkuu wa Kamati Namba 7 ya UPU inayoshughulikia Huduma na Masoko.
Akizungumza
jijini hapa baada ya kupokea cheti hicho, Dr. Kayandabila amesema cheti
hicho ni ushahidi wa dhamira ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na
Wafanyakazi wa Posta kuhakikisha wanatoa huduma bora na zenye kukidhi
viwango vya kimataifa kama nchi zilizoendelea duniani.
Naye
Postamasta Mkuu wa SHIRIKA la Posta Tanzania, Bw. Deos Mndeme ameelezea
furaha yake kwa Shirika kufikia viwango vilivyowekwa na UPU, aidha
amewashukuru na kuwapongeza Wafanyakazi wote wa Shirika la Posta
Tanzania kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na kuliwezesha Shirika
kutimiza viwango vya utoaji wa huduma za Posta hususan usambazaji wa
barua,nyaraka,vifurushi na vipeto hadi kufikia viwango vinavyokubalika
kimataifa.
"Shirika
la Posta linawahakikishia Watanzania na watumiaji wa huduma zetu kote
duniani kuwa tutaendelea kutumia mazingira mapya na teknolojia za kisasa
katika kuboresha huduma huku tukizingatia mkakati mpya wa utoaji wa
huduma za Posta Duniani", Alisema Bw. Mndeme.
Aidha
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Prof. John Nkoma
amesema Tanzania kufikia viwango hivyo vya UPU ni jambo zuri na la sifa
kubwa kwa nchi, lakini pia changamoto kwa Shirika la Posta ambalo halina
budi kuhakikisha kuwa linaendelea kukidhi viwango hivyo siku zote kwa
manufaa ya watumiaji wa huduma za Posta nchini na kwingineko kutokana na
huduma hizi hutolewa kati ya Tanzania na nchi zingine.
"Sisi
TCRA kama wasimamizi wa sekta ya Mawasiliano, zikiwamo huduma za Posta,
tutaendelea kusimamia kuhakikisha viwango walivyofikia wanavidumisha ili
kukidhi matakwa ya huduma bora kwa wateja kwa mujibu wa kanuni na
sheria lakini pia na matarajio ya watumiaji huduma za Posta", alisema
Prof. Nkoma.
Shirika
la Posta Tanzania limepitia mchakato maalum wa Umoja wa Posta Duniani
ili kuthibitisha kuwa limefikia viwango vinavyokubaliwa na nchi
wanachama wa Umoja huo, na sasa ni miongoni mwa Mashirika yanayoaminika
duniani kwa utoaji wa huduma za Posta zinazokidhi viwango vya kimataifa.
0 comments:
Post a Comment