Nafasi Ya Matangazo

October 18, 2012



Na Father Kidevu Blog
BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo, kesho Ijumaa na keshokutwa Jumamosi, italitikisa jiji la Dar es Salaam kwa shoo mbili za kufa mtu zilizopewa jina la Usiku wa kizazi cha dansi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa bendi hiyo 'Camarade' Ally Choki, katika shoo hizo zitakazoanza leo Ijumaa kwenye ukumbi wao wa White House, ulioko Kimara Korogwe na kumalizikia kwenye ukumbi wa Meeda Sinza kesho Jumamosi, mashabiki wa bendi hiyo watapata fursa ya kupata burudani yenye ladha tofauti na ile waliyoizoea.
Choki alisema, katika shoo hizo mashabiki watashuhudia 'vichwa' vinne vikali vya bendi hiyo akiwamo yeye, Rogert Hega 'Catepiller', Ramadhani Masanja 'Banza Stone' na Khadija Mnoga 'Kimobitel' vikichuana vikali, kila mmoja akionyesha kipaji chake kwa kuimba nyimbo zake zote tangu alipoingia katika kizazi cha dansi.
Alisema kuwa usiku huo wa kizazi cha dansi utawahusisha wanamuziki hao ambao wataunganisha nyimbo zao zote waliowahi kuimba na zikatamba katika bendi mbalimbali, hivyo kupata mchanganyiko ambao hauwezi kupatikana katika bendi yoyote hivi sasa.
Choki alisema yeye binafsi ataimba nyimbo zake zote kuanzia ule wa Jirani aliouimba akiwa Twangapepeta,Umbeya hauna posho, Fainali uzeeni, Chuki binafsi, mtaa wa kwanza na nyinginezo, huku Banza akiimba nyimbo kama Angurumapo Simba, Mtaji wa Masikini, Elimu ya Mjinga ni Majungu, Kumekucha, Mtu pesa na nyinginezo.
Nyimbo nyingine zinazotarajia kuimbwa kwa mtindo wa kuchanganya, maarufu kama 'Extra Bongo Mega Mix' ni Fadhila kwa wazazi namba moja na mbili, za Roggart Hegga, 'Kila Chenye Mwanzo','Game 111' na 'Nguzo Tano' walizoziimba wakiwa na Mchinga Sound G 8, huku Extra Bongo yenyewe ikiongezea nyimbo kama, Mtenda akitendewa, Mjini mipango Laptop na nyinginezo.
Kwa upande wake Khadija Kimobitel yeye amejipanga kuutambulisha wimbo wake mpya ujulikanao kwa jina la Mgeni ambao umekuwa moto wa kuotea mbali kwa siku za hivi karibuni, ukiwainua mashabiki vitini katika kila onyesho.
Aidha, onyesho hilo pia linatarajiwa kupambwa na kikundi cha burudani cha Baikoko na mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya Husein Machozi ambaye atakuwa anatambulisha wimbo wake mpya.
Posted by MROKI On Thursday, October 18, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo