Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi akiwaonyesha wadau
waliohudhuria hafla fupi ya makabidhiano chupa ya dawa ya kutibu ugonjwa
wa vikope aina ya Zithromax zilizotolewa na kampuni ya kimataifa
inayofanya utafiti na utengenezaji wa Dawa ya PFIZER kutoka Marekani leo jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi akiangalia moja ya boksi
la dawa za kutibu ugonjwa wa vikope aina ya Zithromax zilizotolewa na
kampuni ya kimataifa inayofanya utafiti na utengenezaji wa Dawa ya
PFIZER kutoka Marekani
leo jijini Dar es salaam. Wengine ni Bi. Caroline Roan makamu wa Rais
wa kampuni hiyo huduma za jamii (katikati) na Dkt. Peter Mbuji Kaimu
Mkurugenzi Idara ya Kinga(kushoto).
***********
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Wilaya
40 nchini zitarajia kunufaika na mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa
Vikope kufuatia kampuni ya kimataifa inayofanya utafiti na utengenezaji
wa Dawa ya PFIZER kutoka Marekani kupitia mpango wa kimataifa wa
kupambana na Ugonjwa wa vikope kuipatia Tanzania msaada wa dawa aina ya
Zithromax kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano ya dawa hizo leo jijini Dar es salaam ,Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa Wizara ya Afya
na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekua ikifanya
mikakati ya kudhibiti ugonjwa wa Vikope na kutoa elimu ya afya kwa
jamii juu ya namna ya kupambana na ugonjwa huo.
Amesema kuwa
Wizara ya afya inaendelea kupambana na magonjwa yaliyosahauliwa ambayo
yamekua yakiathiri watu kwa muda mrefu na kuongeza imekua ikisisitiza
mbinu mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo zikiwemo matumizi ya
dawa, uboreshaji wa mazingira ,matumizi ya maji safi na salama pamoja na
utoaji wa elimu.
Ameongeza
kuwa kampuni ya PFIZER kupitia mpango wa Kimataifa wa kupambana na
Ugonjwa wa Vikope kwa mwaka 2012 imeipatia Tanzania msaada wa chupa
239,952 za dawa ya Zithromax zikiwa katika mfumo wa kimiminika na chupa
za vidonge 17,520.
“Ni
matumaini yangu kuwa dawa hizi zitatoa msukumo wa kuondoa magonjwa haya
kwa sababu tuna mkakati wa jumla wa kutokomeza na kuondoa kabisa
ugonjwa huu na matokeo sasa ni mazuri” amesema.
Kuhusu
usalama na ubora wa dawa hizo Dkt. Mwinyi amesema kuwa dawa hizo
zinakidhi viwango vya kimataifa na zina ubora na usalama kutokana na
matumizi yake katika maeneo mbalimbali nchini toka mwaka 1999.
“Nachosema
sasa tiba tunayo, ubora na usalama wake ni wa uhakika wananchi msiwe na
hofu yoyote kwa sababu dawa hizi hazina madhara” amesisitiza.
Kwa
upande wake makamu wa Rais wa upande wa mahusiano na huduma za jamii wa
kampuni hiyo Bi. Caroline Roan amefafanua kuwa kampuni yake itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwa
ni sehemu ya mchango wake kwa jamii.
Bi.
Caroline amesema kuwa toka mwaka 1999 kampuni ya Pfizer imekuwa ikitoa
msaada wa wa dawa za kukabiliana na ugonjwa wa Vikope/ Takoma kupitia
mpango wa Kimataifa wa kupambana na ugonjwa huo (ITI).
Kampuni
ya Pfizer ambayo imekua ikitoa misaada ya dawa kwenye sekta ya afya
nchini toka 1999 ina makao yake nchini Marekani ni miongoni mwa
makampuni makubwa duniani yanayofanya kazi za utafiti, utengenezaji na
usambazaji wa dawa katika nchi mbalimbali duniani ikiweka msukumo katika
kuhakikisha kuwa binadamu mahali popote pale alipo anapata tiba sahihi
na huduma bora za afya.
0 comments:
Post a Comment