Na: Frank Sanga na Anthony Kayanda, Kigoma,
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amesema hana mpango
wa kugombea ubunge mwaka 2015 badala yake anajipanga kuwania urais.
Zitto alisema hayo jana alipozungumza na wananchi katika mjadala
ulioandaliwa na asasi ya kiraia ya Meza ya Duara uliokuwa unafanyika
maeneo ya Soko la Mwanga, mjini Kigoma. Zaidi ya watu 200, ambao
walihudhuria katika mjadala huo wa wazi walimuuliza maswali mbalimbali
mbunge huyo, huku mmoja akigusia kuhusu tetesi za mara kwamba Zitto
anataka kugombea urais katika uchaguzi ujao.
“Nimefanya kazi kubwa katika kazi yangu ya ubunge, nimeleta
mabadiliko mengi kuanzia bungeni mpaka jimboni. Nadhani inatosha na hata
nikiongezewa miaka mingine sitaweza kufanya yale yaliyonishinda katika
kipindi cha miaka kumi. “Kama Mungu ataniweka mpaka mwaka 2015,
sitagombea ubunge tena kwa sababu kazi niliyofanya inatosha. Natangaza
rasmi kuwa nitagombea urais kupitia chama changu cha Chadema, bila
kusababisha msuguano wowote na sitaki kuingia katika historia ya
kurudisha nyuma harakati za upinzani kushika dola,” alisema Zitto.
“Nataka kuleta changamoto mpya, nitawaeleza watu wa chama changu nia
hiyo na nitatoa hoja za msingi. Hata kama sitapata ridhaa yao, lakini
huo ndio msimamo wangu. “Iwapo chama kikiona sistahili au sifai,
nitakubaliana na uamuzi huo. Watu wengi wanadhani urais ni cheo, hawajui
kuwa ni nafasi ambayo inakufanya ufanye vitu ambavyo ni vikubwa na vya
maendeleo kwa wananchi.” Atangaza kugombea urais Katika hatua nyingine
Zitto alisema ana mpango wa kuwania urais kupitia Chadema katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. “Kwanza nataka niwahakikishia watu wa
Kigoma msiwe wanyonge…mna uwezo wa kutoa rais wa nchi hii,” Zitto
alianza kujibu swali hilo na kuendelea.
Hata hivyo Zitto alipoulizwa baadaye na Mwananchi kuwa mwaka 2015
atakuwa na miaka 39, hivyo kukosa sifa ya kugombea urais kwa mujibu wa
katiba alijibu; “Nadhani nina uwezo wa kuwa rais, sidhani kama Katiba
inaweza kumzuia mtu mwenye uwezo asigombee na ndio maana ninaamini kuwa
kipengele cha kuwa na miaka 40 kitabadilishwa katika katiba mpya.”
“Nchi za Kidemokrasia lazima vyama vibadilishane utawala wa kuongoza
nchi kama ilivyo katika nchi za Ghana na Zambia. Tanzania inatakiwa
kuiga mfano wa nchi hizo,” alisema Zitto Katika kukazia hilo, Zitto
alisema anashangazwa na umaskini uliopo Tanzania wakati mwaka 1976
uchumi wake ulikuwa sawa na nchi ya Malaysia, lakini mpaka kufikia mwaka
2001, Malaysia ilipunguza idadi ya watu wanaoishi chini ya dola moja
kutoka asilimia 56 mpaka kufikia asilimia tatu huku Tanzania ikipunguza
kutoka 51 mpaka 46. Katika hatua nyingine, Zitto alikana kuwa, Chadema
ni chama cha udini, ukanda, ukabila ila akasisitiza kuwa ni chama cha
kitaifa.
“Ndugu zangu naomba mnielewe, Chadema si chama cha ukabila, ukanda
wala udini bali ni chama cha kitaifa. Hizo ni propaganda za wapinzani
wetu,” alisema Zitto baada ya kuulizwa na mmoja wa washiriki kuhusu
tuhuma za chama hicho kuwa cha Kikanda.
“CCM imewahi kudai CUF ni chama cha Waislamu, na sasa wanasema
Chadema ni chama cha Wakristo, sasa wao CCM ni chama cha wapagani au cha
watu gani?” Alihoji Zitto. Alisema ili kuthibitisha kuwa Chadema si
chama cha Kikanda, matokeo ya urais wa mwaka 2010, Dk Wilbroad Slaa
aliongoza dhidi ya wagombea urais wengine kwa kupata kura nyingi katika
Jimbo la Manyovu mkoani Kigoma na hivyo kufanya kupata asilimia nyingi
kuliko sehemu yoyote Tanzania.
0 comments:
Post a Comment