TAARIFA YA UONGOZI WA HOTEL YA PETER SAFARI’s KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSIANA NA MADAI YALIYOTOLEWA NA KOCHA WA TIMU YA YANGA BAADA YA KUMALIZIKA
MCHEZO WAKE NA TANZANIA PRISON TAREHE SEPT 15, 2012.
Ndugu wanahabari,
Karibuni katika mkutano mfupi ambao unalenga
kuzungumzia ama kuelezea masikitiko makubwa dhidi ya Kocha wa Timu
ya Yanga TOM SAINTFIET aliyoyatoa kwa vyombo vya habari kuidhalilisha
hoteli yangu juu ya huduma zake na kiwango chake
alichokiita cha huduma
mbovu!.
Kimsingi management ya Peter
safari’s Hotel na Uongozi wa chama cha wamiliki wa Mahotel Mkoa wa Mbeya,
tumesoma na kusikiliza kwa masikitiko makubwa lawama zilizotolewa na Kocha
huyo kuwa “hajawahi kulala kwenye hoteli ya hadhi ya chini kama
hii katika nchi 20 alizowahi kufanya kazi katika nchi za Afrika”.
Uongozi wa hotel na chama cha
wamiliki wa hotel kwa ujumla kinachukulia suala hili kama kampeni maalumu ya
kudhalilisha na kukatisha tamaa wateja kuiona mbeya haina hotel za hadhi za
kuishi timu na watu wenye hadhi katika jamii, kitu ambacho si kweli na ni
visingizio kutokana kushindwa kwake kuwezesha timu kufikia
matarajio ya mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.
Kimsingi viongozi wa Timu ya Yanga waliomba
kuwalaza wachezaji wawili katika kitanda kimoja tofauti na taratibu za hotel
na hii ilitokana na mipangilio yao hasa kwenye suala la uwezo wa kulipia kila
mchezaji chumba chake, aidha, uongozi wa hotel ulijitahidi kwa kadri ya uwezo
wake kuhakikisha kuwa wachezaji wanapata huduma walizohitaji na hata wakati
mwingine kutoa usafiri kwaajili ya kununua mahitaji ya familia zao kitu
ambacho hakifanyiki maeneo mengine kwa gharama za hotel.
Kwa kutambua madhara yaliyotokana na
matamshi ya kocha huyo raia wa Ubelgiji, Uongozi wa hotel ya Peter
Safaris unayaona matamshi haya kama udhalilishaji
mkubwa na wenye nia mbaya ya kuuharibia mkoa wa Mbeya na kuutangaza vibaya kwa wageni juu ya uwezo wake
katika utoaji wa huduma za hoteli.
Aidha kwakuwa maneno ya kocha
huyo yametamkwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari pasipo
kukanushwa na viongozi wa Timu ya Yanga ambao ndiyo waliofanya maandalizi na
kufanya mazungumzo ya maombi ya kuwalaza wachezaji wawili katika
vyumba ambavyo vina uwezo wa kulaza mtu mmoja (single), Peter safaris
inaliona jambo hilo kama ni sehemu ya kashfa iliyojengwa kwa nia ya
kuiharibia hotel biashara na kuipotezea hadhi mbele ya
wageni na watumiaji wa huduma za PETER SAFARIS ambayo
inaendelea kupanua huduma zake kwa mkoa wa Mbeya na maeneo mengine.
Ikumbukwe kuwa Peter safaris hotels imekuwa
ikipokea wageni wa hadhi mbalimbali wakiwemo viongozi wa ngazi za kitaifa,
wageni kutoka nje wa hadhi za juu na wafanyabiashara wakubwa, hivyo ugeni wa
Yanga na hadhi inayozungumzwa na Kocha huyo hauwezi kufikia mahala pa
kuidhalilisha hotel kwa kiwango hicho ambacho kocha huyo amevitumia vyombo
vya habari licha ya hotel kutopata maoni yoyote baada ya
timu kuhudumiwa kwenye sanduku la
maoni(suggestion box).
Kutokana na hali hii iliyojitokeza, uongozi
wa Hotel unautaka uongozi wa Yanga kuiomba radhi management ya Hotel ya Peter
safaris kwa lugha ya kashfa na isiyoendana na utamaduni wa Mtanzania
kwakuzingatia kuwa wachezaji wakiulizwa namna walivyohudumiwa wasingeweza
kuzungumza hayo ambayo mwalimu wao ameyazungumza kwa utashi wake.
PETER SAFAR’s inalichukulia jambo hili kwa
uzito unaostahili kwakuzingatia kuwa lugha iliyotolewa na mteja
wake huyo imevuka kiwango cha kuvumilika, na njia pekee ambayo tunadhani ni
ya uungwana kabla ya kuingia kwenye taratibu za kisheria ni kuwataka YANGA
kuomba radhi kwa lugha ya dharau na kashfa dhidi ya hotel yetu vinginevyo
tunakusudia kuchua hatua za kisheria kwa kuzingatia kuwa hotel inaendeleshwa
kwa mujibu wa taratibu na sheria zinazotawala huduma za hotel na zile za
mipango miji
ambazo masuala ya usafi ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kukidhi
viwango vya uendeshaji wake.
Ninawashukuruni kwa mahudhulio
yenu
Nawasilisha
MKURUGENZI MTENDAJI
PETER SAFARI’s HOTEL MBEYA.
20/09/2012
|
0 comments:
Post a Comment