Nafasi Ya Matangazo

August 09, 2012

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba akiongea na waandishi wa habari ofisi za Tume leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) kuhusu tathmini ya kazi ya Tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya. Kulia ni Katibu wa Tume Bw. Assaa Rashid.
Mwandishi wa Habari wa Radio Deutchelle Welle Bi. Hawra Shamte akiuliza swali katika mkutano kati ya waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba. Mkutano huo ulifanyika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba avitaka vyama vya siasa, asasi za kidini na wanaharakati kuacha kuwaelekeza wananchi aina ya maoni wanayopaswa kutoa kuhusu Katiba Mpya.

Jaji Warioba ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 9, 2012) katika mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia tathmini ya mikutano ya awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika mikoa minane ya Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba.

“Sio wanasiasa tu, watu wote wakiwemo viongozi wa kidini, wanaharakati na taasisi zisizo za kiserikali ziache kuwalazimisha wananchi watoe maoni wanayotaka wao. Wananchi wawe huru kutoa maoni yao,” alisema na kuongeza kuwa vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali ziatapata muda wa kuwasilisha maoni yao Tume.

“Mwananchi akitoa maoni yake binafsi, anakuwa ‘very articulate’ (anajieleza kwa ufasaha), lakini akielekezwa cha kusema, na ukamuomba ufafanuzi, anashindwa hata kueleza,” alisema Jaji Warioba katika mkutano huo uliohudhuriwa na pia na Katibu wa Tume hiyo, Bw. Assaa Rashid na Naibu Katibu Bw. Casmir Kyuki.

Kuhusu idadi ya mikutano iliyofanyika katika awamu ya kwanza, Mwenyekiti huyo amesema Tume yake imefanya mikutano 386 katika mikoa minane ya awamu ya kwanza kwa muda wa mwezi mmoja.

“Wastani wa wananchi 188,679 walihudhuria mikutano hiyo ya Tume. Hii ikiwa ni wastani wa watu 489 walifika kwenye kila Mkutano,” alisema na kuongeza kuwa Tume inaridhika na idadi hii na inaonesha wananchi wana mwamko wa kutoa maoni yao.

Kati ya waliohudhuria, Jaji Warioba alisema, wananchi 17,440 walitoa maoni yao kwa njia ya kuzungumza kwenye mikutano hiyo na jumla ya wananchi 29,180 walitoa maoni yao kwa njia ya maandishi na kuyawasilisha kwenye Mikutano ya Tume.

Jaji Warioba aliongeza kuwa Tume ilipokea maombi na kufanya mikutano nane na makundi maalum yakiwemo Taasisi za Dini na Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika awamu ya kwanza. 

“Kimsingi, Tume imeridhika na kazi ya ukusanyaji wa maoni katika awamu ya kwanza kwani mikutano yote iliyopangwa na Tume imefanyika na imefanyika kwa amani na utulivu na wananchi walivumiliana katika kutoa maoni yao,” alisema.

Akizungumzia changamoto, Mwenyekiti huyo alisema katika mikutano ya Tume, wanawake bado hawajitokezi kwa wingi kutoa maoni yao mbele ya Tume ingawa wanahudhuria mikutano hiyo na kusisitiza kuwa Tume itaendelea kuwahamasisha kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi.

Kuhusu kuanza kwa awamu ya pili ya mikutano ya kukusanya maoni, Jaji Warioba alisema kazi ya kukusanya maoni kwa awamu ya pili inatarajiwa kuanza rasmi tarehe 27 Agosti, 2012 na ratiba ya mikutano hiyo itatolewa na Tume hivi karibuni.

Akiongea katika mkutano huo, Naibu Katibu wa Tume hiyo, Bw. Kyuki alisema kuwa awamu ya pili ya kazi ya ukusanyaji maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya itafanyika katika mikoa saba ambayo ni Mbeya, Morogoro, Lindi, Ruvuma, Kigoma, Katavi na Mwanza.
Posted by MROKI On Thursday, August 09, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo