Nafasi Ya Matangazo

August 29, 2012

 Bw. Eric Berman Mkugenzi  Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa inayohusika na utafiti wa masuala ya silaha ( Small Arms Survey Poject) yenye makao yake Geneva, Uswisi, akifafua jambo wakati wa uziduzi ya taarifa ya utafiti  uliofanyika mwaka huu. Mkurugenzi huyo ameonyesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika kufanya utafiti kuhusu juhusi za Tanzania katika kudhiti silaha haramu.  Amesema taasisi yake imevutiwa sana na  umakini wa tanzania katika zoezi hilo.


Na Mwandishi Maalum
 Taasisi  inayotambuliwa na kuheshimika kimataifa kama chanzo  rasmi cha utoaji taarifa zinazohusu  silaha, imeelezea nia yake ya  kushirikiana na Tanzania  kufanya  utafiti kuhusu zoezi la udhibiti wa silaha haramu.
 
Hayo yameelezwa na Bw. Eric Berman, Mkurugenzi  Mtendaji wa   Taasisi  hiyo ijulikanayo kama Small Arms Survey Project yenye Makao yake Makuu Geneva,  Uswisi, wakati alipokutana  na   kubadilishana mawazo na Meja Wilbert Ibuge, Mwambata Jeshi katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa.
 
“ Tunafahamu Tanzania ni  kati ya nchi zilizomakini kwenye utekelezaji  wa zoezi la udhibiti wa silaha  haramu, ikiwamo uwekaji  wa alama kwenye silaha. Kwa hiyo tungependa kufanya  mazungumzo ya kuangalia namna gani tunaweza kushirikiana nakufanya utafiti kuhusiana na  juhudi zenu hizi”  akasema Bw. Berman.
 
Aidha akaongeza kwamba hata  wenzao kutoka   Taasisi ya Kanda ya Afrika Mashariki inayohusika na  masuala ya  silaha  ndogo ndogo ( RECSA)  pia wamewadhibitishia kwamba  Tanzania  ni kati ya nchi makini.
 
Nia hiyo ya Mkurugenzi  Mtendaji Berman  ya kutaka kushirikiana na Tanzania kufanya utafiti huo,  imefuatia mchango alioutoa Meja Ibuge kwa niaba  ya Serikali ya Tanzania wakati wa Mkutano wa pili wa Mapitio ya Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu silaha ndogo na nyepesi ( United Nations Program of Action).
 
Mkutano huo ambao ni wa wiki mbili  unafanyika  hapa UM, na umefunguliwa  siku ya jumatatu wiki hii na Naibu Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson. Madhumuni  mkutano huu   pamoja na mambo mengine ni  kutathimini mchakato wa utekelezaji wa mpango huo ambao nchi wanachama  waliupitisha  kwa kauli moja mwaka 2001.
 
Katika mchango wake, pamoja na mambo mengine, mjumbe  huyo wa Tanzania katika Mkutano huo, ameeleza kwamba Tanzania  siyo tu imekuwa ikitekeleza kwa vitendo zoezi la udhibiti wa silaha haramu, lakini pia  inaendelea na kazi kubwa ya uwekaji alama kwenye silaha,  zinazomilikiwa na serikali na zinazomilikiwa na watu binafsi.
 
“ Mwaka 2009,  Serikali ya Tanzania  ilianza zoezi la kuweka alama kwenye silaha, hadi leo hii  tayari tumeshaweka alama kwenye silaha zaidi ya 38,000 zinazomilikiwa na serikali na zinazomilikiwa na watu binafsi” akasema Meja Ibuge Na kuongeza kuwa  zoezi hilo limehusisha mikoa 12 ya Tanzania  Bara na kwamba ni zeozi endelevu ambalo lengo lake ni kuhusisha    mikoa yote 30  nchini.
 
 Akafafanua zaidi kwamba serikali kwa kushirikiana  taasisi za  kikanda kama vile RECSA na GZT  imeendelea na  jitihada za kuwajengea uwezo  kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali maofisa wake.
 
“ Tumejidhatiti kuendelea na zoezi hili tukiamini kwamba hatimaye taasisi za kikanda na kimataifa nazo zitaendelea kuchagiza juhudi hizi pamoja na ushirikiano ili hatimaye sote kwa pamoja tufanikishe kuondokana na biashara haramu ya silaha ndogo na nyepesi” akasisitiza Ibuge.
 
Akizungumzia kuhusu  matumizi ya silaha haramu pamoja na usambazaji wake, Meja Ibuge  amesema, Tanzania  inawasiwasi juu ya  hali ya ongezeko la   utengenezaji, uhamishaji na usambazaji  haramu wa silaha hizo ikiwa ni pamoja na  ulibikizaji  usiodhibitiwa.
 
Aidha  akaongeza kwamba Tanzania  inamashaka na kuwapo kwa mlundikano usio wa uwiano  wa mahitajio ya silaha husika kwa matumizi halali kati ya m nchi   zilizoendelea na zinazoendelea. 
 
Akasema  ulundikaji huo wa silaha  kukichangiwa na kutokuwapo kwa udhibiti wa  uzagaaji  wake ni tisho kubwa kwa amani, usalama na maendeleo hususani Barani Afrika.
 
 Utafiti ambao umefanywa na  Taasisi  ya Small Arms Survey project  umeonyesha kwamba kuna takribani silaha ndogo milioni 875 ambazo ziko kwenye mzunguko duniano kote. Silaha hizo zimetengenezwa na  makampuni zaidi ya elfu moja kutoka  karibu nchi100.
 
Aidha  ripoti ya utafiti huo  ambayo ni ya mwaka huu wa 2012 na imezinduliwa  wakati wa Mkutano huu ,  imebainisha kwamba kumekuwapo na ongezeko la dhamani katika  uhamishaji wa kimataifa wa silaha ndogo na nyepesi,  kutoka dola 4 bilioni mwaka 2006 hadi dola 8.5  bilioni mwaka huu.
Posted by MROKI On Wednesday, August 29, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo