Kalala Junior ( Katikati) akiweka hadharani vionjo vya wimbo wake mpya, Nyumbani ni Nyumbani kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa na wanenguaji wa bendi hiyo, Frida Joseph aka Beckham, Sabrina Mathew na Mary Hamis aka Mary Kimwana wakionyesha staili yao mpya.
Kalala Junior akizungumza na katika mkutano wa utambulisho kwenye ukumbi wa MangoGarden, kulia ni kiongoz msaidizi wa Twanga Pepeta, Saleh Kupaza huku kushoto ni Msemaji wa ASET, Mohamed Pizaro na meneja wa ASET, Hassan Rehani.
Na Mwandishi wetu
UONGOZI wa kampuni ya African Stars Entertainment Tanzania (ASET) umemtambulisha rasmi mwanamuziki mwenye vipaji vingi, Kalala Hamza Kalala maarufu kwa jina la Kalala Junior.
Kalala alitambulishwa kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Mango Garden ambapo mbali ya kusema kuwa amerejea kwa lengo la kuendeleza bendi yake hiyo aliyokuwa nayo kabla ya kujiunga na Mapacha Watatu.
Mwimbaji huyo maarufu alisema kwa fumbo kuwa “Koti limembana akiwa na bendi yake ya Mapacha na kuamua kulivua na kuacha kuendelea kulivaa tena” na kujiunga na Twanga.
“Nimefurahi kujiunga na Twanga tena na nimekuja na zawadi za nyimbo mbili, wimbo wa kwanza unaitwa Nyumbani ni Nyumbani ambao kwa sasa upo katika hatua ya mwisho na utatambulishwa rasmi wiki ijayo, ni wimbo ambao unazungumzia mambo mbali aliyokutana nayo katika muziki mpaka kuamua kurejea Twanga,” alisema Kalala.
Alisema kuwa ujio wake wa Twanga siyo wa kulazimishwa, bali umetokana na mapenzi yake mwenyewe na hasa akikumbuka fadhira za ASET ambapo ndipo alipata umaarufu mkubwa.
“Nawaomba wadau wa Twanga wakae mkao wa kula, kwani nimerejea kivingine na watarajie kupata mambo mengi mazuri, nitafanya zaidi ya yale niliyoyafanya zamani, lengo ni kuendelea kushika hatamu katika muziki wa dansi,” alisema Kalala ambaye vionjo vyake ‘vimewashika’ mashabiki wengi wa muziki wa dansi.
Afisa Habari wa ASET, Mohamed Pizaro alisema kuwa ujio wa Kalala umetokana na mpango wao waliouanzisha ujulikano Amsha Amsha Twanga Pepeta Nyumbani ni Nyumbani .
Pizaro alisema kuwa mpango huo ni maalum kwa kuhimarisha bendi yao na hasa kwa wanamuziki ambao wameonyesha nidhamu nzuri wakiwa chini ya ASET na sasa wanatumikia bendi nyingine.
Kiongozi msaidizi wa Twanga Pepeta, Saleh Kupaza alimpokea kwa mikono miwili mwimbaji huyo na kusema kazi ya kujihimarisha zaidi imeanza.
“Karibu nyumbani, si unajua nyumbani ni nyumbani, tunaamini hata hao wengine wanajifanya vichwa ngumu, nao watarejea tu,” alisema Kupaza.
0 comments:
Post a Comment