Na Mwandishi wetu, DODOMA
MBUNGE wa Viti Maalumu, Catherine Magige, amewalilia vijana kwa kuitaka serikali kuwajiri wanaohitimu vyuo vikuu kwenda kutumikia mahakama mbalimbali nchini badala ya kuwaacha wakihangaika mitaani.
Akichangia katika Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria, bungeni Dodoma, jana, Catherine alieleza kwamba vijana wengi wanaohitimu vyuo vikuu kutoka fani ya sheria wamekuwa wakihangaika mitaani na matokeo yake wengine kujiingiza kwenye mambo yasiyofaa.
Alisema ugumu wa maisha wanaokumbana nao baada ya masomo unawafanya baadhi yao kushindwa kumudu gharama za maisha na matokeo yake kujiingiza kukata tama kimaisha.
Hivyo, aliitaka serikali kuweka mpango ambao utakuwa unawajiri moja kwa moja kutokana na kuonekana uhaba mkubwa wa watumishi wa mahakama, hali itakayosaidia wengi wao kupata ajira kuliko ilivyo sasa.
“Ni muhimu serikali kulitazama hili ili kuwasaidia vijana ambao wanajituma kusoma kwa bidii lakini wanapohitimu masomo yao huishia kuzurura mitaani wakitafuta ajira bila afanikio,”alieleza.
Aidha, aliitaka serikali kuhakikisha inapunguza msongamano wa wafungwa magerezani kwa kuharakisha kesi kuliko ilivyo sasa ambapo kuna mlundikao mkubwa wa keshi katika mahakama nchini.
“Kuwekwe utaratibu maalumu wa kushughulikia kesi hizo ili kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani, maana watu wanakaa kwa muda mrefu sana magarezani bila kutendewa haki,”alisema.
Aidha, aliwataka wabunge kuacha kuingilia mhimili wa mahakama kwa kuujadili bungeni, kwani kufanyua hivyo ni kuvuka mpika ya bunge na matokeo yake kuingilia mhimili mwingine wa dola.
“Lazima tuheshimu mihimili mingine, vinginevyo tunawezakujikuta tukifanya mambo ambayo hayahusiani na kazi za bunge , kitu ambacho kitaleta picha mbaya ya bunge kuingilia mihimili mingine,”alieleza.
Pia, aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni ya mchakato wa katiba, kwani hiyo ndiyo fursa pekee kwa vijana kutambulika katika katiba hiyo kuliko ilivyo sasa.
Alisema kwamba kushindwa kwa vijana kutoa maoni yao katika mchakato huo ni kupoteza fursa adhimu ambayo haitapatikana tena kwa miaka mingi ijayo, hivyo kuwaomba kushiriki kwa wingi katika mchakato huo wa kutoa maoni.
0 comments:
Post a Comment