Kikosi cha wachezaji 23 na viongozi tisa kinatarajia kuondoka kesho (Mei 31 mwaka huu) saa 11.10 alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kwenda Abidjan, Ivory Coast kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayochezwa Juni 2 mwaka huu.
Wachezaji wanaoondoka ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Nassor Masoud Cholo, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Waziri Salum, Shomari Kapombe na Juma Nyoso.
Wengine ni Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar, Shabani Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Haruna Moshi na John Bocco.
Wachezaji waliobaki kutokana na kuwa majeruhi ni mshambuliaji Thomas Ulimwengu anayecheza timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kiungo wa Yanga, Nurdin Bakari.
Viongozi wanaofuatana na timu hiyo ni Kocha Mkuu Kim Poulsen, Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Mukebezi (Meneja wa timu), Juma Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Physiotherapist) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Msafara huo unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Crescentius Magori wakati naibu kiongozi wa msafara ni Makamu wa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) Haji Ameir Haji.
Timu hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeagwa leo (Mei 30 mwaka huu) na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala ambaye aliwataka wachezaji hao kwenda kuiwakilisha vizuri Tanzania kwenye mechi hiyo.
Hafla hiyo ya kukabidhi Bendera ya Taifa pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, Rais wa TFF, Leodegar Tenga na Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe.
Mechi itachezwa kwenye Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny jijini Abijan kuanzia saa 11 kamili kwa saa za Ivory Coast.
Mwamuzi atakuwa Slim Jedidi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Bechir Hassani, wote kutoka Tunisia. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Sherif Hassan kutoka Misri. Mwamuzi wa akiba ni Youssef Essrayri pia kutoka Tunisia.
Mtathmini wa waamuzi ni Rachid Medjiba kutoka Algeria wakati Kamishna wa pambano hilo atakuwa Saleh Issa Mahamat kutoka Chad.
Stars itarajea nyumbani Juni 5 mwaka huu saa 1.40 na kuingia moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Gambia itakayofanyika Juni 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment