Nafasi Ya Matangazo

April 05, 2012

Baadhi ya Makada wa CCM wanaowania Ubunge wa Afrika Mashariki
WANACHAMA 24 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamepitishwa katika kura za maoni za wabunge wa chama hicho kugombea Kiti cha Ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki katika Uchaguzi utakao fanyika Bungeni mjini Dodoma April 17, 2012. 

Kwa muji wa taarifa zilizoifikia Blogu hii zinasema kuwa Wanachama hao 24, ni kati ya wanachama 42  waliokuwa wakiwania nafasi hizo.

Aidha wana CCM hao watahitajika tena kufanya kampeni ili waweze kushinda nafasi nane ambazo zinahitajika kutoka CCM huku Mbunge mmoja akitoka upinzani na kufanya idadi ya Wawakilishi wa Tanzania katika Bunge la Afrika mashariki kuwa 9.

Makada wa CCM waliopitishwa kuwania Ubunge wa Afrika Mashariki ni kama ifuatavyo na kura zao katika mabano. 

1. Kundi la wanawake kutoka Zanzibar waliopita na kura zao kwenye mabano ni Septuu Nassor (177), Safia Ali Rijaal (169) na Mariam Usi Yahaya (179).

2. Katika kundi la wanaume upande wa Zanzibar waliopita ni Dk Said Bilal (197), Abdallah Ali Mwinyi(187), Zuber Ali Maulid (176), Dk Haji Mwita Haji (168), Amada Khatibu (167) na Hamis Jabir Makame (143).

3. Kwa upande wa wanawake Bara waliopita ni Angela Kizigha (160), Janeth Mmari (133), Janet Mbene (116), Fancy Nkuhi (147), Shyrose Bhanji (145) na Godberha Kinyondo (115).

4. Wanaume Bara waliopita ni Adam Kimbisa (196), Dk Edmund Mndolwa (159), Siraju Kaboyonga (153), Bernard Mulunya (143), William Malecela (136), Elibariki Kingu (132), Evance Rweikiza (125), Mrisho Gambo (121) na Charles Makongoro Nyerere (113). 

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila alisema hivi karibuni kwamba uchaguzi wa wajumbe tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge hilo la EALA utafanywa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia Aprili 10 hadi 20, mwaka huu. 

Alisema uchaguzi huo unafanyika kwa kuzingatia kuwa muda wa Bunge hilo lililoingia madarakani mwaka 2006, utafikia ukomo wake Juni 4, 2012.

Kwa mujibu wa kanuni, Katibu wa Bunge ndiye Msimamizi wa Uchaguzi huo na atapaswa kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa masharti yanayohusika, kuhusu siku ya uteuzi, ambayo ni Aprili 10 na siku ya uchaguzi, Aprili  17.

Katika Tangazo hilo, Katibu wa Bunge pia atatoa masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wagombea wa vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni kuhusiana na uchaguzi huo kwa ajili ya kuviwezesha kuanza mchakato wa kuwapata wagombea kupitia vyama hivyo ambao majina yao yatawasilishwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.
Posted by MROKI On Thursday, April 05, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo