Nafasi Ya Matangazo

August 06, 2011

Na Anna Nkinda – Maelezo
 06/08/2011 Watoto yatima wametakiwa kumshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya ufadhili wa masomo na kuitumia nafasi hiyo kusoma kwa bidii kwani wako wengi kama wao ambao wanahitaji kusoma lakini hawapati nafasi kama hiyo na hivyo kuishi katika mazingira hatarishi.

 Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais wa Burundi Dk. Denise Nkurunziza Wakati akiongea na wanafunzi wa kike ambao ni yatima wa shule ya Sekondari ya WAMA NAKAYAMA ambayo inamilikiwa na Tasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) iliyopo nyamisati wilayani Rufiki katika mkoa wa Pwani.

 Dk. Nkurunziza aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwatii walimu wao kwani kwa kufanya hivyo watafanikiwa pia wasiipoteze nafasi waliyoipata kwani wengine wanapoteza bahati pale wanapoitapa.

 “Duniani kuna watoto yatima wengi sana hata Burundi ni wengi mimi mwenyewe nyumbani kwangu ninaishi na yatima 15 ambao si ndugu zangu na ninawasomesha ndani na nje ya nchi hii inatokana na  vita, Ukimwi, vifo lakini mjue kuwa Mungu anawapenda sana watoto yatima kwani akiona umeachwa na wazazi yeye  anakuwa baba na mama yako pia yatima  akilia Mungu anamsikia haraka”, aliwafariji watoto hao.

 Mke huyo wa Rais wa Rwanda aliendelea kuwasisitiza watoto hao wasome huku wakiangalia mbele zaidi kwa kufanya hivyo watafanikiwa kwani hakuna anayejua kesho hata wao wanaweza kuwa viongozi wa ngazi ya juu Serikali kwa kuwa namna utakavyojiandaa leo ndivyo unavyojiandalia maisha yako ya baadaye.

 Dk. Nkurunziza alisema, “Mjue kuwa mama Salma amejitoa kwa jili yenu, anawapenda na kuwaandalia maisha yenu ya baadaye ili yawe mazuri jambo la muhimu mpendane na kuishi kama  ndugu na kuwa mfano kwa jamii inayowazunguka kwani ninyi nyote mnatoka katika mazingira yanayofanana”.

 Alimalizia kwa kuwataka watoto hao kuwa na moyo wa kuwasaidia wengine pale ambapo watamaliza masomo yao na kupata kazi kwani wao pia wamesaidiwa wa watu mbalimbali kwa kufanya hivyo watakuwa wameendeleza malengo ya mama Kikwete ya kuwasaidia watoto yatima wanaoishi katika mazingira hatarishi.

 Akimkaribisha Dk. Nkurunziza ili aongee na wanafunzi hao Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete alisema kuwa dhamira ya kuanzishwa kwa shule hiyo ya mfano ya sayansi kwa mtoto wa kike Lazima wawe na Shule bora ya sayansi ya mtoto wa kikendo nia ya kuanzishwa kwa shule hiyo. ni ndoto  aliyokuwa nayo siku nyingi ya kumkomboa mtoto yatima wa kike ili apate elimu sawa na watoto wengine.

 Mama Kikwete ambaye pia ni Mke wa Rais alisema kuwa licha ya Taasisi ya WAMA kujenga shule hiyo pia inafadhili wanafunzi wa shule za Sekondari katika mikoani yote hapa nchini ambapo mwaka 2010 wanafunzi wa kwanza walimaliza kidato cha nne ambapo wengi wao hivi sasa wako kidato cha tano na wengine wamejiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini.

 “Ninawashauri ndoto yenu ya kwanza baada ya kumaliza masomo muwe  walimu wa sayansi ingawa kila mtu ana ndoto zake katika maisha kwani kwa kufanya hivyo mtakuwa mmelisaidia taifa kwa kuwaelimisha watoto wengi zaidi hapo baadaye  pia mkumbuke kuwa bila ya walimu hata nyinyi msingefika hapo mlipo”, alisema Mama Kikwete.

 Aliendelea kusema kuwa Taasisi ya WAMA imefadhili shule ya sekondari  ya Nyamisati ambayo ina wanafunzi 250 kwa kujenga majengo na kutoa thamani nia ikiwa ni kuhakikisha kuwa watoto wa kijiji hicho wanapata nafasi ya kujiunga na elimu ya Sekondari.

 Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi  wenzake Asteria Ndalu alisema kuwa shule hiyo ambayo imewafungulia milango ya maisha ilianzishwa mwezi wa pili mwaka 2010 ambapo hadi sasa kuna wanafunzi 167 wa kidato cha kwanza na cha pili kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.

 “Sisi ni watoto tunaotoka katika mazingira hatarishi lakini hivi sasa tuna matumaini makubwa kwakuwa Mama Kikwete ameona  matatizo yanayotukabili na kuyatatua, kwani matatizo ni sehemu ya maisha ya binadamu kuna wakati unaweza kufanikiwa na kuna wakati huwezi kufanikiwa jambo linalotakiwa ni kupambana na matatizo hayo”,alisema Ndalu

 Wanafunzi hao waliahidi kushirikiana na walimu wao pamoja na jamii inayowazunguka, kusoma kwa bidii na maarifa ili waweze kutimiza  malengo waliyojiwekea na hivyo kutoziangusha juhudi za Mama Kikwete za kumkomboa mtoto yatima wa kike.
Posted by MROKI On Saturday, August 06, 2011 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo