TAMASHA LA MUZIKI LA MZALENDO HALISI 2011 — Tamasha maarufu la sanaa na muziki asilia wa Tanzania litafanyika kuanzia tarehe 17 – 19 mwezi Juni – wote mnakaribishwa! Usikose tamasha linalosherehekea sanaa, utamaduni na muziki asilia litakalofanyika Dar Es Salaam.
Katika tamasha la kwanza lilifanyika mwezi Mei 2010, washiriki walifarijika na mvuto wa uasilia katika sanaa na muziki ulioonekana kwenye jukwaa. Kivutio kikubwa kilitoka kwa Wazazi Cultural Troupe, maarufu kama ‘Segere’. Bendi ya Wahahapa nao waliwasha moto siku waliyovamia jukwaa. Wasanii kama Irene Sanga, Che Mundu, Jhikoman, Mrisho Mpoto na Vitali Maembe walibariki jukwaa ambalo tamasha hilo la kwanza lilifanyika. Vikundi kama Splendid, Black Roots, Chibite, Swahili Vibes, Amani Ensemble na Zemkala viliwakilisha sanaa iliyoshiba matunda ya utamaduni asilia. Wadau wengi waliuliza kuhusu ufinyu wa taarifa na matangazo kuhusu tamasha la Mzalendo Halisi.
VIVUTIO
Tamasha hili la pili litaanza siku ya Ijumaa kama ufunguzi rasmi, ambapo kutakuwa na onyesho la bendi mbili na sherehe ya kutoa Ngao Ya Mzalendo. Ngao hii ni maalum kwa kuenzi kazi za muziki na sanaa kutoka kwa wasanii, bendi au vikundi kutokana na mchango wao katika jamii.
Mpya ya mwaka huu: Vikundi kutoka mikoa ya Mbeya, Dodoma na Morogoro vitashiriki. Pia kikundi cha sanaa na utamaduni kutoka Msumbiji kinatarajiwa kushiriki.
Washiriki watakaorudi: Black Roots, wakiongozwa na “Makombora” – bendi yenye msisimko kwenye jukwaa kutoka Zanzibar. Kikundi kilichowaburudisha wapenzi walioshiriki mwaka jana cha Wazazi – au maarufu kama ‘Segere’ kitashiriki tena kwa mwaka huu.
Matukio na Maonyesho: Wasanii wa sanaa za aina mbali mbali watakuwapo viwanjani, vyakula vya kuvutia vitakuwapo, maonyesho ya vitu vya sanaa kama nguo n.k. Pia kutakuwa na michezo, vivutio kwa watoto.
CHAKULA
Usikose uhondo wa vyakula halisi vya makabila ya hapa nchini. Kutakuwa na vinono vilivyoandaliwa kiasilia kutoka kwa Wagogo, Wachaga, Wandamba na makabila mengine.
MUDA NA KIINGILIO
Muda: Juni 17, Ijumaa saa12 jioni hadi saa 3 usiku; Juni 18, Jumamosi saa 4 asubuhi hadi saa 4 usiku; Juni 19, Jumapili saa 4 asubuhi hadi saa 3 usiku.
Kiingilio: Kitatangazwa baadae.
MAHALI
Viwanja vya Mnazi Mmoja – Dar Es Salaam.
Maswali? Wasiliana na hii namba (+255) 712 380 208
0 comments:
Post a Comment