Nafasi Ya Matangazo

April 01, 2010

inajiandaa kuongeza mshahara wa kima cha chini katika bajeti ijayo ya mwaka 2010/11. Hayo yamo katika hotuba ya Rais leo usiku ambayo ilitangazwa na TBC.


Hayo alisema wakati akizungumzia mgomo wa wafanyakazi ulioitishwa na TUCTA. Rais alisema kwamba ni vyema kama wafanyakazi wakarejea katika meza ya mazungumzo kabla ya kufanya mgomo.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi viongozi wa TUCTA kuufikiria upya uamuzi wao, waachane na mgomo na wakubali kufanya mazungumzo na Serikali na waajiri wengine, kwa kutumia mfumo uliopo kisheria,” alisema Rais.
Alisema anaamini kwa dhati kuwa huo ndio uamuzi wenye maslahi kwa Taifa na kwa wafanyakazi pia na ni njia bora zaidi ya kufikia kwenye malengo yenye maslahi kwao na kwa waajiri wao.

Alikiri kutambua udogo wa mishahara na kusema haitoshi na ndiyo maana hatua za mara kwa mara zinachukuliwa kuiongeza na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Pia Rais alizungumzia masuala mengine na hasa ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya moyo:
Ifuatayo ni hotuba yake kamili:

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWA WANANCHI, TAREHE 31 MACHI, 2010
Ndugu Wananchi,

Kama ilivyo ada naomba kwanza tumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai na kutuwezesha kuwasiliana kwa utaratibu wetu wa kuzungumza kwa njia hii kila mwisho wa mwezi.
Leo, ndugu zangu nina mambo matatu. La kwanza, linahusu shughuli niliyoifanya leo asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Taasisi ya Upasuaji wa Moyo pamoja na Mafunzo ya Tiba ya Maradhi ya Moyo. La pili, ni kuhusu Tamko la Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) la kutaka kuitisha mgomo. Na, la tatu ni salamu za Pasaka.

Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge, tarehe 30 Desemba, 2005, nilipozungumzia mambo mbalimbali ambayo Serikali yetu inatazamia kufanya kwa upande wa kuboresha huduma ya afya, nilitaja dhamira yangu ya kuchukua hatua zitakazotuwezesha kupunguza idadi ya wagonjwa tunaowapeleka nje ya nchi kwa matibabu. Niliposema vile nilikuwa na maana ya kujenga uwezo wetu wa ndani wa kutibu maradhi na kuendeleza afya za Watanzania ili kusilazimike kupeleka wagonjwa nje.


Taarifa zinaonesha kuwa wagonjwa wengi wanaopelekwa nje kwa matibabu ni wale wa maradhi ya moyo, figo, uti wa mgongo, ubongo, mishipa ya fahamu, kisukari na saratani. Katika kipindi cha tangu mwaka 2005 mpaka sasa, kwa mfano, iliamuliwa kuwa wagonjwa 2,115 wapelekwe nje kwa matibabu zaidi. Kati ya hao 1,093 wameshapelekwa na wengineo bado kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. Katika kipindi hicho pia, kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili hiyo kiliongezeka kutoka shilingi 540 milioni (2005/2006) hadi shilingi 7,194 milioni (2009/2010).

Ndugu Wananchi;
Tunalazimika kupeleka baadhi ya wagonjwa wetu nje kwa sababu tatu. Kwanza, uhaba wa wataalamu wa maradhi hayo au wenye ujuzi wa aina ya tiba inayotakiwa hapa nchini. Pili, upungufu au ukosefu wa vifaa vya uchunguzi na tiba ya maradhi hayo hapa nchini. Na tatu, ukosefu wa miundombinu stahiki ya kutolea huduma inayotakiwa kwa maana ya majengo na mengine. Hivyo basi, kauli yangu, siku ile pale Bungeni, ilikuwa inalenga kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo matatu ili tuweze kuwatibu wagonjwa wetu hapa nchini.

Nafurahi kusema kuwa katika miaka hii minne tumefanya jitihada kubwa na kuchukua hatua za makusudi za kukabili changamoto hizo. Kwa upande wa kupunguza upungufu wa wataalamu, hatua zilichukuliwa kuongeza kasi ya kufundisha madaktari bingwa katika fani mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi. Juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda kwani idadi ya madaktari bingwa imeongezeka kutoka 46 mwaka 2005 na kufikia 265 mwaka 2009.

Ndugu Wananchi;
Mwaka 2006 kwa nia ya kujenga uwezo wetu wa ndani wa kufanya upasuaji wa moyo na tiba ya maradhi ya moyo kwa jumla, tulipeleka wataalamu wetu 26 nchini India kwa mafunzo. Wataalamu hao waliporejea nchini waliungana na wenzao waliosomea nchi nyingine na waliopo nchini na kuanzisha shughuli ya upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Tangu mwezi Mei, 2008 mpaka sasa wagonjwa 160 wamefanyiwa upasuaji kwa mafanikio. Hata hivyo, wataalamu wetu hawa wangeweza kufanya zaidi kama wangepata nafasi kubwa zaidi ya kufanyia shughuli yao hiyo. Hivi sasa wanafanyia upasuaji wa moyo kwa kutumia chumba cha upasuaji kilichojengwa katika Taasisi ya Mifupa pale Muhimbili ambayo haitoshelezi mahitaji.

Ujenzi wa jengo tuliloweka jiwe la msingi, leo ndilo jawabu la uhakika la kutatua tatizo hilo. Jengo hilo litakuwa na vyumba vya kutosha vya kufanyia upasuaji na vifaa vya kisasa vya upasuaji, uchunguzi na tiba ya maradhi ya moyo kwa jumla. Jengo hilo litakuwa na vitanda 100 vya kulaza wagonjwa jambo ambalo linatoa fursa ya wagonjwa zaidi ya 300 kutibiwa kwa mwaka.

Napenda kuitumia nafasi hii kwa mara nyingine tena kumshukuru Rais Hu Jintao wa Jamhuri ya Watu wa China kwa moyo wake wa upendo kwetu na kukubali maombi yetu. Ilikuwa mwaka 2006 aliniahidi kuwa wamekubali maombi yetu na leo tunashuhudia utekelezaji unaoanza. Kwa hakika Wachina ni marafiki zetu wa kutumainiwa.

Ndugu Wananchi;
Ukiacha maradhi ya moyo, tumechukua hatua thabiti za kujenga uwezo wetu wa kutibu maradhi ya figo. Tayari tumeshapata na kufunga mashine 7 za kusafishia figo na vifaa vingine muhimu kwa tiba ya maradhi ya figo. Wataalamu wanane waliopelekwa India kupata mafunzo ya tiba ya maradhi ya figo pamoja na upasuaji wamekwisharejea. Wataalamu hao wakiungana na wenzao waliopata mafunzo kwingine, nchi yetu sasa inao uwezo wa kutibu maradhi ya figo na kufanya upasuaji. Kwa sababu hiyo basi, baada ya muda si mrefu Watanzania hawatalazimika kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kusafisha figo au hata kwa ajili ya upasuaji wa figo.

Ndugu Wananchi;
Juhudi zinaendelea kufanywa ili tuweze kujenga uwezo wetu wa ndani wa tiba na upasuaji kwa upande wa maradhi ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu. Tumefikia mahali panapoleta matumaini kuwa huenda tukawa na kituo kikubwa na cha kisasa kwa ajili ya tiba, upasuaji na mafunzo. Tukifanikiwa katika dhamira yetu hiyo, tutakuwa tumepunguza idadi ya watu wanaopelekwa nje kwa ajili ya tiba ya
maradhi hayo.

Ndugu Wananchi;
Juhudi zetu kwa upande wa tiba na upasuaji wa maradhi ya kinywa na meno zimepata mafanikio makubwa. Kwa ushirikiano baina ya Serikali yetu na marafiki zetu kutoka Marekani wakiongozwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Miracle Corners of the World, kumefanyika ukarabati na uboreshaji mkubwa wa jengo la tiba ya meno pale Muhimbili na vifaa vipya na vya kisasa vimewekwa. Hivi sasa Mtanzania halazimiki kwenda nje kwa ajili ya tiba ya meno na kinywa. Na, ukweli ni kwamba kwa ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki sisi sasa ndiyo wenye kituo cha kisasa zaidi na tunatarajia majirani kuja kwetu kupata tiba hiyo.

Ndugu Wananchi;
Baada ya kupata vifaa vipya na vya kisasa vilivyoanza kutumika mwaka wa jana, Hospitali ya Saratani ya Ocean Road imejenga uwezo mkubwa wa uchunguzi na tiba ya saratani. Wagonjwa wengi ambao zamani walikuwa wapelekwe nje sasa wanafanyiwa uchunguzi na kupata tiba hapa nchini. Wapo wanaopelekwa nje, lakini ni pale tu inapokuwa lazima kwa sababu aina ya tiba inayotakiwa inahitaji. Hata hivyo, hatujachoka. Tunaendelea na jitihada za kutafuta vifaa zaidi na kutoa mafunzo kwa madaktari, wauguzi na wataalamu wetu. Aidha, tunaendelea na mipango ya kujenga hospitali mpya mahali pengine. Pale Ocean Road pameshakuwa pafinyu. Vile vile, mipango inaendelea ya kuzijengea uwezo wa tiba ya saratani Hospitali za Bugando, KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Mbeya. Kwa sasa mchakato umeanza kwa Hospitali ya Bugando.

Ndugu Wananchi;
Kazi ya kujenga uwezo wa ndani wa kutibu maradhi ambayo wagonjwa wetu hupelekwa nje inayofanywa na Serikali hivi sasa inaweza pia kufanywa na sekta binafsi. Kwa sababu ya kutambua ukweli huo, Serikali imekuwa inashawishi na kutengeneza mazingira mazuri kwa makampuni, asasi za kijamii, hospitali binafsi na hata watu binafsi wenye wezo kuwekeza katika ujenzi wa hospitali za kutibu maradhi ambayo watu wengi huenda nje kutibiwa. Nafurahi kwamba wito wetu umepokelewa na baadhi ya asasi, hospitali na hata watu binafsi wameanza kujenga hospitali hizo.

Naipongeza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa uamuzi wake wa kuzishawishi hospitali kubwa sita nchini India, za Apollo na Madras Mission, ambazo ndizo wagonjwa wetu wengi wanapelekwa kutibiwa, kuja kufungua matawi yao hapa nchini. Pia, nawapongeza kwa uamuzi wao wa kuzungumza na madaktari wa kutoka hospitali hizo kuja nchini kwa nyakati fulani fulani kukagua wagonjwa wao ambao wangetakiwa kurudi India kwa uchunguzi wa afya zao baada ya kupata tiba. Mambo haya mawili yakifanikiwa yatasaidia kuwezesha watu wengi kupata huduma nzuri itolewayo na hospitali hizo hapa nchini bila ya watu kulazimika kwenda India. Mpango huu pia utasaidia kupunguza gharama. Nawatakia kila la heri.

Ndugu Wananchi,
Mimi na wenzangu Serikalini tunatambua kuwa suluhisho la uhakika kwa juhudi zetu tuzifanyazo kwa lengo la kupunguza kupeleka wagonjwa nje ni kuimarisha afya za Watanzania ndilo jawabu la msingi. Kutokana na kutambua huko ndiyo maana tumechukua hatua za makusudi za kuboresha, kupanua na kuimarisha huduma ya afya nchini.

Tumeongeza bajeti ya huduma ya afya na kuwa ya tatu kwa ukubwa baada ya elimu na miundombinu. Tumeanzisha mpango kabambe wa miaka 10 wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ambao sasa uko katika mwaka wa tatu wa utekelezaji wake. Mimi naamini kama tutautekeleza mpango huu kama ilivyokusudiwa tutaimarisha afya za wananchi na kujenga uwezo wetu wa ndani na kupunguza kutegemea nchi za nje kwa tiba ya watu wetu.
Tamko la TUCTA Kutangaza Mgomo

Ndugu Wananchi,
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia ni tamko lililotolewa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) la kutaka kuitisha mgomo wa wafanyakazi wote wa nchi nzima kuanzia terehe 5 Mei, 2010. Lazima nikiri mapema kabisa kuwa nilipata taabu kulizungumzia jambo hili hasa kwa jinsi kauli za viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanaohamasisha mgomo huo zilivyokuwa kali.

Wakati mwingine baadhi ya viongozi huwa na jazba na kutoa maneno ya kejeli. Nilichelea nami kuingizwa katika zogo la kutupiana maneno. Lakini kwa uzito wa jambo lenyewe na wajibu wangu wa uongozi na ulezi wa taifa letu, naona ninao wajibu wa kusema angalau maneno machache tu.

Ndugu Wananchi;
TUCTA inataka siku hiyo watu wote walioajiriwa wagome na kwa muda usiojulikana. Tamko hilo linawahusu wafanyakazi wa umma Serikalini na katika Mashirika ya Umma pamoja na wafanyakazi wa sekta binafsi walioajiriwa popote pale mashambani, maofisini, viwandani, majumbani, mahotelini, madereva, n.k. Kwa maneno mengine wanataka shughuli zote nchini zinazofanywa na watu walioajiriwa zisimame kwa muda usiojulikana kuanzia siku hiyo. Sababu ya msingi inayotolewa na viongozi wa wafanyakazi ya kufikia uamuzi huo ni kuwa haki zao na maslahi yao yanapuuzwa na waajiri na hasa Serikali.

Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi viongozi wa TUCTA kuufikiria upya uamuzi wao, waachane na mgomo na wakubali kufanya mazungumzo na Serikali na Waajiri wengine kwa kutumia mfumo uliopo kisheria.

Nayasema haya kwa kuwa naamini kwa dhati kuwa huo ndiyo uamuzi wenye maslahi kwa taifa letu na kwa wafanyakazi pia.

Hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kufikia kwenye malengo yenye maslahi kwao na kwa waajiri wao. Mgomo ni hatua ya mwisho baada ya mazungumzo kushindwa kutoa jawabu. Mimi siamini kuwa tumeshafikia hatua hiyo. Lakini, ni ukweli pia kwamba hata pale wafanyakazi wanapogoma hatimaye mambo humalizwa kwa kuzungumza. Katika hali hiyo nawasihi tuchague kuzungumza sasa kuliko kuzungumza baada ya mgomo kwani kuna hatari ya mahusiano yetu kuchafuliwa na misuguano inayotokana na mgomo.

Tunawajali na Kuwathamini Wafanyakazi

Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia wafanyakazi wote nchini na wananchi wenzangu wote kuwa tunawajali na kuwathamini sana wafanyakazi: wawe wa Serikali au wawe wa sekta binafsi. Kamwe hatujawapuuza na mimi binafsi nitakuwa mtu wa mwisho kufanya hivyo.

Tangu tuingie madarakani tumechukua hatua thabiti za kuendeleza haki na maslahi ya wafanyakazi mambo yanayothibitisha ukweli huu kwamba tunawapenda, tunawathamini na kuwajali wafanyakazi nchini. Orodha ni ndefu lakini niruhusuni nitaje baadhi ya mambo. Tumeongeza mshahara wa kima chini mara tatu kuanzia mwaka 2006 kutoka shilingi 65,000 hadi 104,000 sasa, na hivi sasa tunajiandaa kuongeza tena katika bajeti ijayo. Tumeongeza mishahara kwa makundi mbalimbali kwa nyakati mbalimbali: walimu, madaktari na wauguzi, wakufunzi wa vyuo vikuu, wafanyakazi wa vyuo vikuu wasiokuwa wakufunzi, wanasheria n.k. Hivi sasa tunajiandaa kuangalia makundi mengine na hata baadhi ya yale tuliyoongeza siku za nyuma tutayaangalia tena.

Tumekuwa tunautumia utaratibu huu kwa sababu tukifanya hivyo, bajeti ya Serikali inaweza kumudu. Lakini, tukifanya tofauti na kuwaongeza wafanyakazi wote mara moja bajeti haitamudu au kitakachotokea ni watu wote kupata kidogo kidogo kisichokuwa na tija yoyote. Utaratibu wetu huu umetusaidia sana mpaka hapa tulipofikia sasa na naamini utaendelea kutufaa hata huko mbele tuendako.

Ndugu Wananchi;
Ninaposema hivyo, sina maana sitambui kuwa mishahara hiyo ni midogo na haitoshi, la hasha! Nautambua ukweli huo na ndiyo maana tumekuwa tunachukua hatua za mara kwa mara kuongeza mishahara na kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Aidha, nimeelezea nia yetu ya kuendelea kufanya hivyo tena mwaka huu pamoja na changamoto za kibajeti kwa upande wa Serikali ambazo hatuwezi kuzipuuza.

Kwa upande wa mafao ya wafanyakazi wa Serikali za Mitaa, Serikali imesikiliza kilio chao na kukubali kuubadili mfumo wa malipo baada ya kustaafu kutoka ule wa akiba ya uzeeni (provident fund) na kuwa ule wa pensheni. Mabadiliko hayo yanahitaji shilingi 103 bilioni ambazo Serikali imeamua kuubeba mzigo huo badala ya kuacha wafanyakazi waubebe wenyewe. Kwa ajili hiyo kila mwaka Serikali italipa zaidi ya shilingi 10 bilioni. Hivi asiyekujali anakufanyia mema haya?

Ndugu Wananchi;
Ni, Serikali yetu hii ndiyo iliyochukua hatua za kutekeleza Sheria Na.6 ya mwaka 2004 kuhusu Taasisi za Kazi na Sheria Na.7 ya mwaka 2004 kuhusu Mahusiano Kazini. Katika Awamu hii ndipo tulipotengeneza Kanuni za Sheria hizo na kuanza utekelezaji wake.

Sheria hizo zimeweka mfumo mpya na bora zaidi wa kulinda na kutetea haki na maslahi ya Wafanyakazi nchini. Matokeo yake ni kuundwa kwa Bodi za Kisekta 8 ambazo kazi yake ni kupanga kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi na maslahi mengineyo ya wafanyakazi katika sekta binafsi. Kazi nzuri iliyofanywa na Bodi hizo ndiyo iliyowezesha kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi katika sekta binafsi kupanda kutoka shilingi 30,000 kwa wafanyakazi wa mashambani na majumbani na kuwa shilingi 60,000. Na, kwa wafanyakazi wa viwandani kupanda kutoka shilingi 45,000 mpaka shilingi 80,000 na 150,000 kutegemea na uwezo wa viwanda.

Aidha, tumeunda Tume ya Usuluhishi na Maamuzi ambayo imewezesha kesi za wafanyakazi zilizokuwa zinachukua miaka mingi, wakati mwingine mpaka miaka 5 kumaliziwa, sasa huchukua muda mfupi kwani Sheria inataka kesi hizo zimalizwe ndani ya siku 30. Tume hiyo imeshafanya kazi nzuri sana mpaka sasa. Kesi zinamalizwa kwa wastani wa siku 21.
Mpaka Desemba 31, 2009 kesi 20,021 zilikuwa zimewasilishwa, ambapo kati ya hizo kesi 16,161 zimesikilizwa ambapo 12,748 zimesuluhishwa na 3,413 zimepelekwa kwa maamuzi, yaani arbitration. Aidha, Tume hiyo imefanikisha kuundwa kwa Mabaraza ya Wafanyakazi katika Wizara zote na Halmashauri zote za wilaya na Miji. Mabaraza haya ni majukwaa muhimu yanayowapa fursa wafanyakazi kukaa na waajiri kuzungumzia ufanisi wa kazi, tija na maslahi yao.

Ndugu Wananchi;
Serikali yetu imefanya kazi kubwa wakati mwingine usiku na mchana kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya miaka mingi ya wafanyakazi wa Serikali kuhusu kupandishwa madaraja na madai ya stahili zao. Wapo watu tuliowakuta hawajapandishwa vyeo kwa miaka 10 au zaidi, sasa wamepata haki yao. Maelfu ya wafanyakazi waliokuwa na malimbikizo ya madai ambayo mengine yalikuwepo tangu mwaka 2003 tumeweza kuwalipa. Hivi sasa tatizo hilo si kero tena kama ilivyokuwa siku za nyuma. Inawezekana wapo wafanyakazi wachache wachache wanaodai ambao nao ukweli ukijulikana watalipwa.

Mwaka 2008 tulitunga Sheria mpya ya fidia kwa wafanyakazi wanapoumia. Sheria hiyo ilifuta sheria ya zamani ambayo wafanyakazi walikuwa wanalipwa viwango vidogo sana. Viwango vya fidia vimeboreshwa na kubwa zaidi ni kwamba mfanyakazi akipata kilema cha kudumu akiwa kazini alipwe fidia mpaka kufa kwake. Hayo ni mabadiliko ya kimapinduzi yanayofanywa na viongozi na Serikali inayojali.

Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yetu ni sikivu. Na, ushahidi wa ukweli huo ni haya yote niliyoyasema ambayo ni baadhi tu ya mazuri mengi tuliyoyafanya, hayangewezekana kama sisi tungekuwa ni watu tusiosikiliza, kama baadhi ya wasemaji wa vyama vya wafanyakazi walivyokuwa wanataka ieleweke hivyo katika madai yao ya kuhamasisha migomo.

Mimi nimeshaonana na kuzungumza na viongozi wa wafanyakazi mara nne. Mwaka jana mwezi Machi, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda ametumia karibu mwezi mzima kukutana na kuzungumza na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kimoja baada ya kingine. Mawaziri Hawa Ghasia, Juma Kapuya na kabla yake Capt. John Chiligati wamekuwa wanakutana nao mara kwa mara. Katibu Mkuu Kiongozi, Ndugu Phelomon Luhanjo nae halikadhalika. Hapo sijataja mikutano ya Baraza la Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma ambapo naambiwa mwaka wa jana pekee walikutana mara sita badala ya mara moja. Hata mwaka huu mkutano wa Machi 20, haukufanyika kwa sababu viongozi wa wafanyakazi walikataa kwa vile wanajiandaa kwa mgomo.

Ndugu Wananchi;
Nayasema haya kwa kirefu kiasi hiki kutaka kuondoa dhana potofu ati kuwa sisi katika Serikali tunawapuuza wafanyakazi na ndiyo maana wanalazimika kugoma. Tunawajali, tunawasikiliza na ndiyo maana tumeweza kufanya mambo mengi kiasi hiki. Najua yapo mengine ya kuzungumza na kufanya baina yetu. Lakini sidhani kwamba hayo yamefika mahali pa kutokuelewana mpaka wafanyakazi wabaki na uamuzi mmoja tu wa kugoma. Mimi naamini hata hayo wanayoamini wao ni magumu yanazungumzika na kumalizika kwa njia ya mazungumzo kwa mujibu wa mfumo wetu uliopo kisheria. Napenda kurudia kuwasihi tuzungumze. Wazungumzao hawagombani. Nashauri tuzungumze sasa siyo tungoje kufanya hivyo wakati au baada ya mgomo. Kwa sasa mazingira ni mazuri, sina hakika hali itakuwaje baada au wakati wa mgomo. Linalowezekana leo lisingoje kesho; alitufundisha Baba wa Taifa.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Jambo langu la tatu na la mwisho kwa siku ya leo ni kuwatakia sikukuu njema ya Pasaka. Ni matumaini yangu kuwa tutaisherehekea kwa furaha, utulivu na usalama.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza
.
Posted by MROKI On Thursday, April 01, 2010 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo