Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Rais Mwai Kibaki wa Kenya mara baada ya kufanya mazungumzo naye ikulku jijini Dar es Salaam leo mchana.Rais Kibaki yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili
Rais wa Kenya Mwai Kibaki akikagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake na Jeshi la Wananchi Tanzania.
Rais Jakaya Kikwete akimkaribisha nchini Rais wa Kenya Mwai Kibaki kwa ziara ya kiserikali.
Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akiwa na mgeni wake Rais Mwai Kibaki wa Kenya wakilakiwa na akinamama wakazi wa Dar es Salaam baada ya Rais Kibaki kuwasili katika uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana kwa ziara ya kiserikali.
Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania uko imara na ziara ya siku mbili ya Rais Mwai Kibaki hapa nchini imezidi kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili.
Marais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania na Rais Mwai Kibaki wa Kenya wameyasema hayo katika kikao cha pamoja kilichofanyika Ikulu ya Dar-es-salaam, leo mchana mara baada ya Kuwasili nchini.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wawili kila mmoja alipata nafasi ya kumueleza mwenzake kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi ya nchi yake na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Akimkaribisha mgeni wake, Rais Kikwete ameelezea hali ya kisiasa nchini Tanzania kuwa shwari na pia kuelezea nia ya kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili kwa upana zaidi kwa kuongeza nafasi za uwekezaji na biashara baina yao.‘
Tunahitaji kuongeza nafasi za kfanya biashara baina yetu zaidi na kupanua wigo wa kushirikiana katika sekta mbalimbali zikiwemo Biashara, Nishati, Utalii, Usafirishaji, Kilimo na Usalama.
Katika usalama, swala kubwa wakilokubaliana viongozi hao ni kushirikiana katika Mikoa ya Mara kwa Tanzania na Mara Magharibi kwa upande wa Kenya ambako kumekuwa na mapigano ya wizi wa mifugo baina ya watu wake.
Viongozi wamekubaliana swala hili lifanyiwe kazi haraka kwa viongozi na maafisa wa pande zote mbili kukutana na kutafuta njia muafaka wa kutafuta suluhu la kudumu kwa tatizo hili kubwa.
Rais Kibaki nae amemueleza Rais Kikwete kuwa serikali yake kwa sasa inafanya juhudi za kurejesha Kenya kwenye hali ilivokuwa kabla ya machafuko ya kisiasa yaliyoikumba nchi yake baada ya uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka 2007.
‘Tumekuwa na tofauti zetu lakini sasa tunafanya kazi pamoja, vyama vimekubaliana na kazi kubwa tuliyonayo sasa ni kuirudisha nchi katika hali yake ya awali” amesema Rais Kibaki.
Mara baada ya mazungumzo yao Rais Kibaki na ujumbe wake walishiriki chakula cha mchana kilichoandaliwa kwa heshima yake na Rais Kikwete ambapo amemshukuru kwa kutikia mualiko wake wa kuja nchini.Rais Kikwete pia amempongeza Rais Kibaki kwa uongozi na jitihada za serikali yake katika kutafuta amani hususan katika nchi za Sudan, Somalia na Jamhuri ya Watu wa Congo (DRC).
Kesho Rais Kibaki, anatarajia kufungua rasmi jengo la ubalozi wa Kenya hapa nchini ambapo ataandamana na mwenyeji wake Rais Kikwete na baadaye kuelekea uwanja wa ndege ambapo Rais Kibaki ataelekea Zanzibar na kupokelewa na Rais Amani Karume ambapo watafanya mazungumzo katika Ikulu ya Zanzibar kabla ya kuondoka na kurejea nchini kwake.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu, Dar-es-salaam.
16 July, 2009.
0 comments:
Post a Comment