Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetumia siku ya Valentine kwa kupeka tabasamu kwa wananachi wa mkoa wa Mwanza kwa kutoa Hatimiliki za Ardhi kwa watu ambao wamekamilisha taratibu zote za umiliki wa ardhi.
Akizindua Kliniki ya Ardhi inayoendelea katika viwanja vya Ofisi ya Kata ya Igoma jijini Mwanza Februari 14, 2026, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amesema wizara hiyo imepeleka tabasamu kwa wananchi wa Mwanza ambao wamekamilisha mchakato wa kupata Hati kwa kufuata taratibu zote za umiliki na eneo lake halina mgogoro na kupelekea kupata hati kwa muda mfupi.
“Inawezekana hati kutoka, hakuna madalali katika kupata hati, Watanzania tusigombanishwe na madalali katika mchakato wa kupata Hatimiliki ya Ardhi. Katika mchakato wa kupata hati hayupo dalali, huu ni muda wa kuwaletea wananchi tabasamu, tabasamu la wananchi wa Mwanza ni kupata hati” amesema Naibu Waziri Mmuya.
Ameongeza kuwa Kliniki ya Ardhi ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwaletea wananchi tabasamu.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa Sekta ya Ardhi kuwafuata watumishi wa sekta mbalimbali katika ofisi zao na kutumia fursa ya matukio yanayoendeshwa ndani ya maeneo yao kwa kutoa huduma za ardhi hatua inayowarahisishia wananchi hao kujisajili katika mfumo wa e-Ardhi ili kuwarahisishia mchakato wa kupata hati.
Katika kuendelea kuwapelekea tabasamu watanzania, Naibu Waziri Mmuya. amesisitiza kuwa Waziri ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo ameelekeza watumishi wa Ardhi mikoa yote Tanzania Bara kuendesha Kliniki ya Ardhi Maalum kwa wananwake kuanzia tarehe 2 – 7 Machi 2026 kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo hufanyika kila tarehe 8 Machi kila mwaka ili kuendelea kuwaletea tabasamu watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema Ofisi yake Pamoja na Mkuu wa Mkoa huo, wametenga siku za Jumanne na Alhamisi kila wiki kushughulikia changamoto mbalimbali na kuhakikisha wanamaliza migogoro iliyopo na kutokuzalisha migogoro mipya.
Naye mwananchi wa Kata ya Igoma jijini Mwanza ambaye amepokea hati ya kiwanja chake Bi. Zuwena Soudy amesema furaha yake ni kupokea hati ya kiwanja chake ambayo ataitumsaidia kiuchumi na sasa ana uhakika wa eneo lake lipo salama.
Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza kuanzia tarehe 13 hadi 18 Machi 2026 ambapo atashiriki zoezi la Kiliniki ya Ardhi Igoma jijini Mwanza, Wilaya ya Ukerewe pamoja na halmashauri ya Buchosa katika Kijiji cha Kasisa.














0 comments:
Post a Comment