Nafasi Ya Matangazo

June 30, 2024









Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amelifunga kanisa la CHURCH OF GOD lililoko kijiji cha Mendo, Tarafa ya Itwangi, Wilaya ya Shinyanga ili kupisha uchunguzi maalum.

Akiambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, Wakili Mtatiro amelifunga kanisa hilo baada ya tukio la tarehe 17 Juni 2024 ambapo mmoja wa waamini wa kanisa hilo alishawishiwa na mchungaji wa kanisa hilo akajifungulie kanisani badala ya kwenda kliniki.

Mtatiro amesema, "tumebaini mchungaji husika anakiuka maadili ya mafundisho ya Mungu ama linatoa mafundisho potofu kwa ujumla ambayo ni hatari kwa usalama wa nchi yetu..."

Kwa mujibu wa maelezo yenye ushahidi, yaliyotolewa na wananchi mbalimbali mbele ya Mkuu wa Wilaya, wakati amefanya ziara ya dharura kufuatilia sakata hili, imeelezwa kuwa Mchungaji wa Kanisa hilo amekuwa anawahamasisha waamini wake;

1. Wasiende Kliniki wanapokuwa wajawazito, badala yake wakachukue huduma za Kliniki kwake
2. Wanapokaribia kujifungua wasiende Kliniki - badala yake wakajifungulie kanisani kwake (Tarehe 17 Juni 2024 muumini mmoja, miaka 24, alishikwa na uchungu, wazazi wakamchukulia usafiri aelekee Kliniki, akakataa katakata, akakimbilia kwa Mchungaji, wakaanza maombi, wakamzalisha kwa kuvuta kichanga kama vile unavyovuta kamba kwenye mashindano, kikatoka kikiwa kimefariki baada ya kichwa kushindwa kutoka kwa muda mrefu. Madaktari waliwahi eneo la tukio na kuokoa maisha ya muumini huyo.
3. Mchungaji anahamasisha waamini wasiwapeleke Kliniki watoto wa miaka 1 - 5.
4. Mchungani anawakataza katakata waamini wake wasitoe majina ya ukoo kwa watoto wao, majina kama MASANJA, NG'WANA MABULA na mengine kwake ni mwiko - waamini nao wametii.
5. Mwaka jana aliwatia waamini hasara kubwa, aliwakataza kulima mazao yoyote katika mvua za Novemba na Disemba 2023 kwa maelekezo kuwa mvua hizo ni za laana na Mungu amemuotesha, akawataka watumie mvua za Januari - Machi 2024. Waamini waliofuata maelekezo yake, wameambulia patupu - waliolima kwa mvua za LAANA za Nov na Dec 2024, wamevuna hasa.

Katika Mkutano wa Hadhara uliofanywa na Wakili Mtatiro akiiongoza Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Shinyanga, hatua zifuatazo zimechukuliwa;
1. Kulifunga Kanisa hilo kwa muda ikiwa ni pamoja na kulifanyia upekuzi wa nyuzi 360.
2. Mchungaji huyo ametakiwa asirejee katika kijiji cha Mendo, chenye kanisa hilo, ukizingatia kwamba yeye ni mkazi wa kijiji kingine - Mtatiro ameeleza kuwa lengo ni kuhakikisha timu ya uchunguzi haiingiliwi.
3. Mchungaji na wenzake waliomshawishi na kujaribu kumpa huduma za kikunga mama huyo mwenye mimba tayari wamehojiwa na vyombo na watafikishwa mahakamani.
4. DC Mtatiro amemuelekeza Katibu Tawala wa Wilaya, Ndg. Said Kitinga, aunde Kamati Maalum ya kukagua ikiwa ujenzi wa kanisa hilo umefuata taratibu za kisheria.

Wakili Mtatiro amesisitiza kuwa "nchi ya Tanzania haina dini, lakini watu wake wana dini zao".

Mtatiro amesisitiza kuwa nila kuathiri imani ya kila Mtanzania, kwa dhamana aliyonayo, hawezi kusubiri matukio mabaya kamaya ya KIBWETERE (Uganda) au SHAKAHOLA (Kenya), yatokee Shinyanga. 

Mtatiro ametoa onyo kwa aina ya wachungaji wenye mafundisho potofu wajue kuwa serikali iko macho.
Posted by MROKI On Sunday, June 30, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo