Nafasi Ya Matangazo

March 02, 2017


NA BASHIR NKOROMO
Ikiwa sasa ni takriban miaka miwili tangu aliyekuwa Mkurugenzi wa Tanzania One Theatre (TOT), Kampteni John Komba, kufariki Dunia, Mtoto wake Gerald John Komba, ameibuka na kutoa wimbo wa kuiunga mkono Serikali katika mapambano yake mapya dhidi ya dawa za kulenya nchini Tanzania.

Gerald aliyezaliwa mwaka 1986 jijini Dar es salaam, amesema, ameamua kutoa wimbo huo wenye maudhi ya kwaya, ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kifo cha Baba yake, Marehemu John Komba aliyefariki  Dunia, Februari 28, 2015 katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni jijini Dar e Salaam, alikopelekwa baada ya kuzidiwa ghafla akiwa nyumbani kwake, Tangibovu kwa Komba.

Mtoto huyo wa Jihn Komba aliyekuwa mwanamuziki nguri wa utunzi na uimbaji wa nyimbo za kwaya, amesema, wimbo aliotoa nimarejeo ya wimbo ambao ulitungwa na nguri huyo, kukemea usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya miaka zaidi ya kumi iliyopita, lakini baada ya kuurekodi haukuwahi kuimbwa na TOT wala kuchezwa kwenye vituo vya Radio au Televisheni.

Gerald ambaye amesomea Sheria katika Chuo Kikuu cha Saint Augustine kilichopo Mwanza,  Tanzania,  baada ya masomo ya shule ya Msingi katika shule ya Kawe "A" na shule yasekondari Mbezi Beach High school, anasema katika kuutoa wimbo huo, hakubabaisha kwa kuwa na yeye anacho kipaji cha kuimba japo amekuwa hakitumii sana. Zamani Shule ya Kawe A' ilifahamika kwa jina la Tanganyika Packers, lakini baada ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kubaini kuwa kiwanda cha kusindika nyama cha Tanganyika Packers kimeshakufa, akaamua shule hiyo kubadilishwa jina.

"Nimeanza kupenda sanaa ya muziki tangu nilipokuwa mtoto, kwa kuwa nilikuwa naenda na Baba (John Komba) kwenye maonesho yake na kundi la TOT,  na nilikuwa navutiwa sana na namna baba yangu alivyokuwa akitamba jukwaani wakati akiimba", alisema Gerald.

"Tangu wakati huo, nilikuwa napenda kukariri nyimbo zote za Baba, na hakuna wimbo nisioujua kuanzia ala hadi mpangilio wa mashairi, lakini pia pia shuleni nilikuwa naimba kwenye kwaya ya shule, na siku za karibuni nimekuwa pia nikiimba kwaya kwenye Kanisa la Praise team, hapa jijini Dar es Salaam", aliongeza.

Anasema, ameambua  kuurudia wimbo wa Marehemu Baba yake kwa sababu, kwanza yeye binafsi anachukia mamia ya vijana wanavyoharibika kwa matumizi ya dawa za kulevya kwa namna ambavyo wanatumiaji wengi wa dawa hizo hukatishwa ndoto zao mbalimbali za kuwa watu muhimu katika ujenzi wa taifa la Tanzania.

"Kwanza ukizingatia hakuna aliyezaliwa teja, wengi  wanaokuwa hivyo wanakutana na hili balaa wanapoingia kwenye jamii kwa hiyo nikaona nifanye kitu ili jamii iweze kutoa mchangu wangu katika kuelimisha jamisha jamii ili izinduke na kuelewa namna dawa hizi za kulevya zilivyo za hatari.

Pili niliamua kuurudia wimbo huu kwa sababu, watu wengine hasa Walimu na Wazazi wengi wao wanajisahau katika kusimamia malezi ya vijana. Wazazi wanamwachia Mwalimu jukumu la kutazama mwanafunzi akiwa shule bila kujua mtoto anaharibika katikati ya shule na nyumbani wakati wa kwenda na kurudi nyumbani, kwa hiyo Mwalimu na mzazi  ni Watu muhimu wa kuchunga mwanafunzi", alisema Gerald.

Anasema, sababu yake ya tatu ya kuamua kuurudia na kuongeza vionjo kwenye wimbo huo ni kusisitiza kuwa mapambano hayo ni ya Watanzania wote ambapo anasema ameweka baadhi ya majina ya wakuu wa mikoa kwenye wimbo huo kwa kuwa vita hii ya mapambano dhi ya dawa za kulevya ni ya Watanzania wote na hao ndiyo wawakilishi wa Rais kwenye kila mkoa.

"Nimeongeza vionjo kwa kutaja hawa wakuu wa mikoa kwa kuwa najua hawa ndiyo waakilishi wa Rais, na Rais Dk. John Magufuli hawezi kukabiliana nayo peke yake hivyo unahitajika ushirikiano na wananchi kuanzia ngazi ya Kaya, Vijiji, Kata, wilaya hadi mkoa.

Na mwisho niliamua kuurudia kama Kumbukumbu ya miaka miwili ya kifo cha Marehemu Baba, ukiuusikiliza wimbo huu utangua kuwa sauti yangu na yake zimefanana kwa karibu sana katika uimbaji, hivyo itaweza kuashiria kuwa yale alyolenga kuyakemea kwenye nyimbo zake, hata baada ya kufariki dunia lakini bado kuna mtu mwingine ambaye ni mtoto wake atakayeendelea nyimbo hizo kufanya lengo lake la kuionya jamii ibaki pale pale", alisema Gerald

"Mtindo nilioutumia kwenye wimbo huu ni uleule wa kwaya aliotumia Baba, na nimeuimba upya kwa kushirikiana na Mama yangu Mzazi, Jane Mkondwa ambaye ni mwimbaji wa miaka mingi katika Kundi la TOT, Nimeurekodi katika Studio za PM Records chini ya Mtayarishaji anayefahamika kwa jina la Testimony.

"Baadhi ya maneno yaliyomo kwenye wimbo huu ni maneno ambayo ambayo hutumiwa zaidi na mateja na nimefanya hivyo kwa kuwa ni miongoni mwa walegwa katika vita hii. Hivyo, nikaona nitumie maneno wanayoweza kuyaelewa haraka kama;  'nywele misumari', 'twende kilioni', 'Macho kufutuka', 'akili inayeya' ambapo neno kama akili inayeya kwa teja humaanisha anavyokuwa baada ya kulewa dawa za kulevya yaani ufahamu katika akili zake unapotea.

"Maneno mengine ni Gheto na Washkaji (nyumba wanapoishi vijana wa kiume au wa kike, lakini neno mshkaji au washkaji unategemea na umri, wale wa miaka ya 1960 walimaanisha wanawake wao lakini wa sasa wanamaanisha marafiki wao ingawa maana zote mbili zina maana sawa", anafafanua Gerald.

Anasema, kwa sasa wimbo huo bado upo katika sauti tu (Audi), kwa kuwa hajapata uwezo wa kuurekodi katika video, ingawa yupo katika jitihada za kutafuta uwezo ili kuhakikisha anaurekodi katika video ili ujumbe uweze kufika kwa urahisikwa walengwa wote.

Gerald anatoa mwito kwa Watanzania kuungana ili tulitokomeza usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya bila kujali itikadi za vyama, kabila, jinsia kwa kuwa ni janga linaloweza kuingia katika familia, Taasisi, Chama cha siasa, kabila au jinsia yoyote.

"Watanzania wenzangu naomba kila atakayepata fursa ausikilize kwa makini wimbo wangu huu,  ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli katika mapambano haya mapaya dhidi ya usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania", anasema Geral
Posted by MROKI On Thursday, March 02, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo