Nafasi Ya Matangazo

June 08, 2014

Mzee Small afariki Dunia.
Habari za kusikitisha zilizotufikia hivi punde zinaarifu kuwa Mwigizaji maarufu na mkongwe katika fani ya vichekesho nchini Tanzania, Said Ngamba maarufu kwa jina la Mzee Small (59) amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mzee Small amefikwa na umauti majira ya saa 4 za usiku wa Juni 7, 2014 katika Hospitali ya Taifa Muhumbili.

Akiongea kwa njia ya simu mke wa marehemu, Bi Fatuma Saidi, ameithibitishia Father Kidevu Blog, kuwa Msanii Said Ngamba hatunae.

Bi Said amesema kuwa marehemu mumewe amefikwa na umauti baada ya hali yake kubadilika jana (Juni 7) asubuhi na kumbikiza Muhimbili ambako alishinda nae akipatiwa matibabu na majira ya saa tatu usiku alirudi nyumbani na kumwacha kijana wake akimwangalia mgonjwa na ilipotimu saa tano usiku kijano huyo alirudi na kusema baba amefariki.

“Nikweli Mzee Small amefariki”….yalikuwa ni maneno machache yaliyobenba uchungu mzito kufuatia kifo cha mumewe.

Mipango ya Mazishi inafanyika nyumbani kwa marehemu Tabata Mawenzi, Dar es Salaam.

Blog ya Father Kidevu inatoa pole kwa familia yake yote, Ndugu jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huo.


MAISHA NA SANAA
Katika historia fupi, Mzee Small alipata elimu ya msingi katika Shule ya Mingumbi huko Kilwa mkoani Pwani. Mbali na kuwa mkongwe, Mzee Small kila ulipobahatika kuzungumza naye alikuwa  na kawaida ya kutamba kuwa yeye ndiye msanii wa kwanza kabisa Tanzania Bara kuchekesha runingani.

Mzee Small alianza sanaa hiyo yapata miaka 31 iliyopita na alipata kufundishwa na mwigizaji Said Seif ‘Unono’ (ambaye pia kwa sasa ni marehemu).

Mbali na kushiriki sanaa katika vikundi mbalimbali, Mzee Small wakati wa uhai wake ametumika katika vikundi vya mashirika kama vile Reli, NASACO na mengine mengi, ambayo kwa sasa hayajihusishi tena na shughuli hizo.

Mzee Small alianza kujulikana sana katika fani ya uchekeshaji hasa pale alipoibuka na mchezo uliojulikana kama 50, 50, 100, na ule wa Mjini Shule uliomwelezea mwanamke wa kijijini aliyeolewa mjini.

Mbali na kutamba na michezo hiyo, Mzee Small alikuwa ni mcheshi na mwenye kupenda utani wakati wote, aliibuka na kichekesho kisemacho Nani Mwenye Haki, ambacho baadaye alikiboresha zaidi.

Baadaye aliibuka na kitu kingine kikali kilichokwenda kwa jina la Nani Kama Shule, huku akiwa amewashirikisha wakali wengine kama King Majuto, Kingwendu na wachekeshaji wengine wanaotamba kwa sasa Bongo.

Mzee Small alikuwa ndiye mmiliki wa kundi la sanaa linalojulikana kama Afro-Dance ambalo alilisajili mwaka 1994 kwenye Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kutoa ajira kwa vijana wa mitaani.

Pamoja na kuwa na uzoefu wa kisanaa, lakini mkongwe huyo hakuwahi kuwa na mpango wa kujiunga na kundi lingine, ila alichokuwa akifanya ni kurekodi na wasanii wengine alipokuwa akiitwa kwa makubaliano maalum.

Pia mkali huyo wa vichekesho enzi za uzima wake na uhai wake alikuwa akijishikiza katika duka moja Kariakoo la Home Shopping Centre kimatangazo.

Kutokana na vichekesho, Mzee Small huwa anatania kuwa sanaa ilimpa mke wa ndoa katika televisheni ambaye ni Bi Chau huku akianisha kuwa mkewe, Bi Fatuma huwa hana tatizo lolote na Bi Chau kwani anajua kinachoendelea kuwa ni kazi tu.


Mzee Small amefariki na kuacha mjane na watoto watano, watatu wa kiume na wawili wa kike. Kipindi cha uhai wake Marehemu Small alikuwa akisisitiza sana elimu na Sanaa iwe baada ya kumaliza masomo yao.



MATESO YA KIAFYA

Wakati akiendelea na harakati za kisanaa, mwaka juzi Mzee Small aliripotiwa kupatwa na ugonjwa wa kiharusi (stroke) alipokuwa kwenye shughuli za kisanaa Kanda Ziwa.



Ugonjwa huo ulimpa mateso makubwa huku akiwa hana msaada wowote.

Wakati akiteseka na kiharusi alipata tatizo linguine kwenye ubongo huku akitakiwa kila mwezi kwenda kliniki kwa ajili ya ‘check-.



Hakika kila nafsi itaonja mauti na leo Mzee Small ambaye mbali na kuiburudisha alikuwa akitoa mafunzo kwa jamii yetu kupitia kazi zake, leo ameonja mauti na Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ampunzishe Mkali huyo wa vichekesho mahali pema.
Posted by MROKI On Sunday, June 08, 2014 1 comment

1 comment:

  1. REST IN PIECE MZEE SMALL, U WILL BE REMEMBERED FOREVER.

    ReplyDelete

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo