Nafasi Ya Matangazo

January 09, 2013

 Sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania ambayo hutumiwa na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kupokelea bidhaa zao.

Uchumi katika kanda ya Afrika Mashariki uliendelea kuimarika mwaka uliopita, 2012 licha ya changamoto lukuki iliyokabiliana nazo.Kanda nzima ilionyesha uchumiwake kukua kwa nguvu na kusukuma juhudi za kuimarisha mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). 

EAC inajumuisha nchi tano wananchama ikiwa ni pamoja na Kenya,Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, Mwandishi Isaac Mwangi wa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) anaadika zaidi katika Makala haya:

Kwa mujibu wa taarifa rasmi zinazotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kila baada ya miezi mitatu, pato la mwaka katika robo ya kwanza ya mwaka uliopita liliongezeka kwa asilimia 7 katika nchi za Rwanda na Tanzania na kiasi kikubwa cha kuongezeka kwa pato pia liliripotiwa nchini Uganda.

Uganda iliripoti pato chanya la kukua kwa uchumi wake katika robo ya kwanza ya mwaka 2012 kufuatia kukua kwa hasi kwa uchumi wake katika robo ya mwisho ya mwaka 2011.

Uchumi wa Burundi kwa upande wake uliendelea kuathirika vibaya kutokana na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mfumuko wa bei,kushuka kwa makusanyo ya mapato ya serikali na wabia wa maendeleo kujitoa kuunga mkono juhudi za serikali.

Viashiria vya uchumi katika kanda hiyo ya Afrika Mashariki, vimeonyesha dalili kubwaya kukua kwa uchumi wa kanda hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka jana, ikiwa ni pamoja na kwenye sekta za huduma nchini Rwanda na viwanda nchini Uganda na Tanzania.


Hali ya kushuka mara kwa mara kwa thamani ya fedha katika kanda hiyo pia ilipungua katika kipindi chote cha robo ya pili ya mwaka 2012 ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa sera nzuri za fedha zilizowekwa na mamlaka za udhibiti wa fedha katika kanda.

Viashiria vingine vya kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na kupungua kwa bei ya mafuta na mavuno mazuri ya vyakula yaliyotokana na hali nzuri ya hewa na kuimarisha mikakati ya uzalishaji kama vile Mpango wa Kuimarisha Mazao nchini Rwanda na Kilimo kwanza nchini Tanzania. 

Pia viwango vya wastani vya ubadilishanaji wa fedha za kigeni umepunguza makali ya kuleta mfumuko wa bei miongoni mwa nchi wananchama.

Utafiti uliofanywa na jarida moja la African Business Magazine umebaini kwamba ukuaji endelevu wa uchumi wa Tanzania unatokana na uendeshaji mzuri wa makampuni kwa kufuata sheria na taratibu na hivyo kuongeza idadi ya makampuni ya Kitanzania katika Kundi la Makampuni 25 ya Juu Afrika Mashariki kutoka matatu yaliyokuwepo hadi sita katika kipindi cha mwaka mmoja tu. 

Kampuni ya Azam ni moja ya vielelezo tosha vya Ukuaji wa Uchumi kwa Kanda ya Afrika Mashariki hasa nchini Tanzania kutokana na jinsi kampuni hiyo ya uzalishaji wa Bidhaa mbalimbali za Chakula inavyofanya kazi zake katika Nchi za Afrika Mashariki 

Kwa upande mwingine uchumi wa Kenya haukukua kwa kasi kama nchi nyingine za Afrika Mashariki na badala yake ilipata ongezeko la ziada la idadi ya watu. Uchumi wa Uganda umeongezeka kutokana na matarajio ya kupata mafuta nchini humo.

Kenya imeripoti kukua kwa uchumi wake kwa kiwango cha chini zaidi cha asilimia 3.5 katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Kiwango hicho kinashindana kihafifu na ukuaji kwa nchi nyingine za kanda hiyo. Rwanda asilimia 7.9, Uganda asilimia 7.2 na Tanzania asilimia 6.7. Kenya pia amejikuta ikiwa na kiwango kikubwa zaidi cha mabadiliko ya mfumuko wa bei kutoka asilimia 19.7 Novemba mwaka jana hadi kufikia asilimia 4.1 mwezi huu. 

Ufanisi wa uchumi wa Kenya kwa mwaka huu wa 2013 utapatikana kwa kiasi fulani kutegemeana na jinsi gani nchi hiyo itakavyoendesha uchaguzi wake mkuu mwezi Machi.Kwa kuwa ndiyo nchi yenye nguvu zaidi za kiuchumi katika kanda hiyo,ufanisi wake pia utaathiri nchi nyingine wananchama wa EAC.

Nchini Burundi, mfumuko wake wa bei umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka kutoka asilimia 25.2 mwezi Aprili (ikiwa ni kiwango cha juu zaidi Afrika Mashariki) hadi asilimia 17.3 mwezi Juni kutokana na kushuka kwa bei za vyakula. Hatua ya kupungua kwa mfumuko wa bei za vyakula inatokana na juhudi za serikali kuondoa kodi za vyakula vya msingi vinavyoingizwa nchini humo kutoka nje.

Hatua hiyo ambayo ilianza kutumika tangu Mei 15, iliishia Desemba 31, mwaka jana. Bidhaa za vyakula zilizohusika kutotozwa kodi ni pamoja na unga wa muhogo, mahindi na mtama na maharage, mchele, viazi,samaki na mafuta ya alizeti. Mavuno mazuri ya mazao ya vyakula pia yamesaidia kupungua kwa bei za vyakula.

Licha ya kuongezeka kwa hofu ya vitendo vya ugaidi,sekta ya utalii ilifanya vizuri huku kukiwa na idadi kubwa ya hoteli mpya na maeneo ya kupumzikia yaliyofunguliwa ili kuendana na idadi kubwa ya watalii waliokuwa wanamiminika ndani ya kanda hiyo ya EAC.
Posted by MROKI On Wednesday, January 09, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo