Nafasi Ya Matangazo

January 18, 2013

Wanamichezo 50 kati ya 52 waliochukua fomu kuomba kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika Februari 24 mwaka huu wamerejesha fomu hizo.

Waombaji ambao hawakurejesha fomu ni Geofrey Nyange aliyekuwa akiomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha mikoa ya Morogoro na Pwani, na Shufaa Jumanne aliyekuwa akiomba kuwakilisha Kanda ya Dar es Salaam.

Orodha kamili ya waombaji ambao wamerejesha fomu ni Athuman Nyamlani, Jamal Malinzi, Omari Nkwarulo na Richard Rukambura (Rais). Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia (Makamu wa Rais).

Kwa upande wa ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Abdallah Musa, Salum Chama na Kaliro Samson (Kagera na Geita), Jumbe Magati, Mugisha Galibona, Richard Rukambura, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).

Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo, Elly Mbise na Omari Walii (Arusha na Manyara), Ahmed Mgoyi na Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama na Stanley Lugenge (Njombe na Ruvuma).

Athuman Kambi, Francis Ndulane na Zafarani Damoder (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Hassan Othman Hassanoo, Riziki Majala na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), David Lugenge, Elias Mwanjala, Eliud Mvella na John Kiteve (Iringa na Mbeya), Davis Mosha, Khalid Mohamed na Kusiaga Kiata (Kilimanjaro na Tanga) na Alex Kamuzelya, Juma Pinto, Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda (Dar es Salaam).

6 WAOMBA UONGOZI BODI YA LIGI KUU, WOTE WAREJESHA FOMU
Waombaji wote sita wa uongozi katika Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) ambayo uchaguzi wake utafanyika Februari 22 mwaka huu wamerejesha fomu.

Kwa upande wa Mwenyekiti waombaji ni Hamad Yahya wa Kagera Sugar na Yusuph Manji wa Yanga wakati Makamu Mwenyekiti aliyeomba ni Said Mohamed wa Azam.

Nafasi mbili za ujumbe wa Bodi ya Ligi Kuu kwa klabu za Daraja la Kwanza zimeombwa na watu watatu. Waombaji hao ni Christopher Peter Lunkonde wa Moro United, Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba ya Mwanza na Omari Khatibu Mwindadi.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF itaanza kukutana kesho kwa ajili ya kupitia fomu zote zilizowasilishwa na waombaji kwa ajili ya uchaguzi wa TFF na ule wa Bodi ya Ligi Kuu.

Pia Kamati inapenda kuwakumbusha waombaji uongozi kuzingatia Kanuni za Uchaguzi, kwani baadhi yao wameanza kufanya kampeni kupitia vyombo vya habari. Kwa walioanza kufanya kampeni kabla ya wakati wanajiweka katika hatari ya kuenguliwa kushiriki katika uchaguzi.

RWIZA, LIUNDA KUSIMAMIA MECHI ZA CAF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua Watanzania Leslie Liunda na Alfred Rwiza kuwa makamishna wa mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika zinazoanza mwezi ujao.


Rwiza ameteuliwa kuwa kamishna wa mechi kati ya APR ya Rwanda na Vital’O ya Burundi itakayochezwa nchini Rwanda kati ya Februari 15 na 17 mwaka huu.


Naye Liunda atakuwa kamishna wa mechi ya marudiano kati ya Tusker ya Kenya na St. Michel United ya Seychelles itakayochezwa Kenya kati ya Machi 1 na 3 mwaka huu. Mechi zote ni za raundi ya awali.


WATANZANIA KUZICHEZESHA URA, COTTON SPORT
Waamuzi wanne wa Tanzania wameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuchezesha mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa kati ya URA ya Uganda na Cotton Sport ya Cameroon itakayochezwa jijini Kampala kati ya Machi 1 na 3 mwaka huu.


Orden Mbaga ndiye atakayekuwa mwamuzi wa kati na atasaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Jesse Erasmo wakati mwamuzi msaidizi namba mbili ni Hamis Chang’walu. Mwamuzi wa mezani ni Israel Mujuni na Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Souleiman Waberi wa Djibouti.


Wakati huo huo, waamuzi kutoka Afrika Kusini ndiyo watakaochezesha mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa kati ya Simba ya Tanzania na Clube Recreation Libolo ya Angola itakayofanyika Februari 17 mwaka huu jijini Dar es Salaam.


Waamuzi hao ni Daniel Volgraaff atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake ni Enock Molefe, Lindikhaya Bolo na Lwandile Mfiki. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Lesita kutoka Lesotho.


KIM AZIFUATA IVORY COAST, MOROCCO AFCON
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameondoka leo mchana (Januari 18 mwaka huu) kwa ndege ya South African Airways kwenda Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Ivory Coast na Morocco zinazoshiriki Fainali za 29 za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoanza kesho (Januari 19 mwaka huu) nchini humo.


Ivory Coast na Morocco ziko kundi moja na Tanzania (Taifa Stars) katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.


Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, na inayoshika nafasi ya pili katika kundi hilo ambalo pia lina timu ya Gambia itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Posted by MROKI On Friday, January 18, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo