Serikali imelaani vikali vitendo vya ubakaji na ukatili wa kijinsia vinavyosababisha waathirika kupata mimba, huku ikiwataka wazazi, ndugu na wananchi kwa ujumla kutokuingilia mchakato wa kisheria katika kesi zinazohusu ubakaji na ulawiti, ili kuhakikisha waathirika wanapata haki na wahusika wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Hawa Mchafu Chakoma, kuhusu kauli ya Serikali juu ya matukio ya ubakaji yanayoendelea na kusababisha waathirika kupata mimba, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazolinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili, ikiwemo ubakaji na ulawiti.
Katika majibu ya Serikali, imeelezwa kuwa kuanzia Januari hadi Desemba 2025, jumla ya makosa 7,219 ya ubakaji yaliripotiwa na kushughulikiwa, hatua inayoonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha mikakati ya kukabiliana na vitendo hivyo na kuhakikisha waathirika wanapata huduma na ulinzi unaostahili.
Aidha, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na ukatili pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa waathirika kupitia Ofisi za Ustawi wa Jamii, Madawati ya Jinsia na Watoto ya Jeshi la Polisi na Ofisi za Serikali za Mitaa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mahundi amewasihi wazazi na ndugu kutokuingilia kesi za ubakaji na ulawiti zilizo katika vyombo vya sheria, ikiwemo kwa kuzuia utoaji wa ushahidi au kushinikiza hatua zinazoweza kuathiri mwenendo wa haki.
Serikali pia imewahimiza wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili na kushirikiana na vyombo vya dola katika kutoa ushahidi ili wahusika wawajibishwe. Wananchi wanaweza kutoa taarifa kupitia namba ya Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi 0699 913200 au kupiga namba 116 wakati wote wanapohitaji kuripoti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.









0 comments:
Post a Comment