Nafasi Ya Matangazo

July 07, 2026

Na Dk. Reubeni Lumbagala
Miongoni mwa haki za msingi za mfanyakazi serikalini au sekta binafsi ni pamoja na kulipwa mafao yake kwa wakati pindi anapostaafu utumishi wake.

Mafao hayo yanatokana na michango aliyochangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka kwenye makato ya mshahara wake pamoja na michango ya mwajiri wake.

Kwahiyo, mfanyakazi anapomaliza muda wa utumishi wake eidha kwa kustaafu kwa hiari au kwa lazima, mifuko ya hifadhi ya jamii inapaswa kumlipa mafao yake ili kuendeleza maisha mengine, kwani maisha lazima yaendelee hata baada ya kustaafu.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wastaafu kucheleweshewa kulipwa mafao yao, ambayo kama nilivyoeleza awali ni haki yao ya msingi na si hisani. Kwa ufupi, wanastahili kulipwa bila usumbufu wowote.

Kucheleweshewa mafao ya wastaafu kumesababisha usumbufu mkubwa kwa wastaafu, na hata kuwasababishia msongo wa mawazo kwa kujiuliza kwani kustaafu ni kosa la jinai hadi kusumbuka kiasi hicho? 

Ni faraja kuona kuwa, sasa kero hiyo ya kuchelewa kulipwa kwa mafao ya wastaafu inakuwa historia nchini.

Mwezi Aprili, 2026, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeanzisha kaulimbiu isemayo "Tunalipa Jana" yenye malengo ya kuharakisha malipo ya mafao ya wastaafu kwa wakati mara tu mfanyakazi anapostaafu.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, amesema mfuko huo umejizatiti kuhakikisha wastaafu wanalipwa mafao yao kwa wakati ili kufurahia utumishi wao.

"Tunapoanza kumsajili mwanachama, tunahakikisha taarifa zake zinakuwa sahihi na zinahuishwa kila inapobidi. Lengo letu ni kwamba anapofikia umri wa kustaafu asiwe na changamoto yoyote ya malipo. Tunataka alipwe siku ya kustaafu. Hiyo ndiyo tafsiri halisi ya kaulimbiu yetu ya Tunalipa Jana, amesema Magambo.

Katika hatua nyingine, Magambo ameishukuru serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa deni la shilingi trilioni nne kwa Mfuko huo, jambo lililoimarisha ukwasi na uendelevu wa kulipa mafao.

Kwa hakika, mkakati wa PSSSF wa kulipa mafao ya wastaafu mara tu wanapostaafu ni jambo la kupongezwa. 

Wapo baadhi ya wastaafu kwa kuchelewa kulipwa mafao yao, wamejiingiza katika mikopo yenye riba kubwa, jambo linaloathiri mafao yao kwani wanapokuja kulipwa, hujikuta wakilipa deni kubwa linalochukua asilimia kubwa mafao yao. 

Kwa hili la kumlipa mstaafu kwa wakati, kutaleta utulivu wa akili, kustamwezesha mstaafu kutumia fedha zake kadri ya mipango yake aliyonayo na kufurahia utumishi wake na kuona kustaafu ni heshima na si mateso au adhabu. Sitakosea kusema PSSSF mmeutendea haki msemo wenu wa "Kesho Yako, Kipaumbele Chetu".

Maoni : 0620 800 462.
Posted by MROKI On Tuesday, July 07, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo