Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema, amefichua siri iliyoiwezesha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame (Makame WMA) kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza nchini kwa mafanikio ya uhifadhi unaoshirikisha jamii, akitaja uongozi madhubuti, uwazi, uzingatiaji wa sheria na ushirikiano wa wananchi kuwa nguzo kuu za mafanikio hayo.
Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa viongozi na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo waliotembelea Wilaya ya Kiteto Tarehe 21 Julai,2026 kwa lengo la kujifunza namna ya kuanzisha na kusimamia Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori za Jamii (WMA), Mhe. Mwema alisema mafanikio ya Makame WMA hayakupatikana kwa bahati, bali yamejengwa na misingi imara ya utawala bora na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori.
Alisema viongozi na wataalamu wana jukumu la kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi zinafuatwa wakati wote, huku wakijenga ushirikiano na wananchi kujenga thamani ya kuhifadhi rasilimali zinazowazunguka.
"Uhifadhi wenye mafanikio unaanza na uongozi bora, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi. Jamii, inalinda rasilimali zake kwa moyo mmoja," alisema Mhe. Mwema.
Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa Makame WMA ni miongoni mwa WMA kongwe na zenye mafanikio makubwa nchini katika uhifadhi wa wanyamapori, uwekezaji wa utalii na miradi ya biashara ya kaboni.
Alisema mafanikio hayo yameifanya Makame WMA kutwaa tuzo ya Jumuiya Bora ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (Serengeti Awards 2025) jambo linalodhihirisha kuwa jamii zinaweza kusimamia uhifadhi kwa ufanisi na wakati huo huo kupata manufaa ya kiuchumi.
Aidha, alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006 na kisha kuanza rasmi kunufaika na shughuli za uhifadhi Mwaka 2015 hadi sasa, Makame WMA imeingizia vijiji wanachama zaidi ya Shilingi Bilioni Nane (8) , fedha ambazo zimechangia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mapato yatokanayo na biashara ya hewa ukaa na uwekezaji wa vitalu vya uwindaji.
Katika maelekezo yake kwa viongozi wa Kilolo, Mhe. Mwema aliwataka kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na ujangili, akionya kuwa vitendo hivyo vinaendelea kuwa tishio kwa uhifadhi wa wanyamapori na maendeleo ya WMA.
Pia alisisitiza umuhimu wa kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi, ili waendelee kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali hizo na kunufaika na matunda ya uhifadhi.
Kuhusu usimamizi wa mapato, alisema fedha zinazotokana na shughuli za WMA zinapaswa kusimamiwa kwa uwazi na kuelekezwa katika miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi, huku akisisitiza uzingatiaji wa mipango bora ya matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro na uvamizi wa maeneo ya hifadhi.
Vilevile, aliagiza elimu kwa wananchi kuhusu namna salama ya kuishi na wanyamapori iendelee kutolewa ili kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mhe. Rashid Nzelemela, alisema wameamua kujifunza kutoka Makame WMA kutokana na mafanikio yake makubwa katika usimamizi wa uhifadhi, uwekezaji wa utalii na biashara ya kaboni.
Alisema maarifa na uzoefu walioupata Kiteto utakuwa msingi muhimu wa kuanzisha WMA imara, endelevu na yenye kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Kilolo.










0 comments:
Post a Comment