Nafasi Ya Matangazo

June 04, 2026





Tanzania imeandika historia mpya katika sekta ya usafiri wa anga na utalii baada ya Shirika la Ndege la Brussels Airlines kuzindua rasmi safari zake za moja kwa moja kati ya Brussels, Ubelgiji na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) katika hafla iliyofanyika Juni 3, 2026.

Kuanza kwa safari hizo ni utekelezaji wa Mkataba wa Huduma za Usafiri wa Anga kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ufalme wa Ubelgiji uliosainiwa Novemba 3, 2021 jijini Dodoma, ukilenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafiri wa anga, biashara, utalii na uwekezaji. 
 
Akizungumza wakati wa mapokezi ya ndege hiyo iliyowasili kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb), amesema uzinduzi wa safari hizo kutoka Brussels, makao makuu ya Umoja wa Ulaya (EU), ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Ubelgiji pamoja na nchi nyingine za Ulaya.
 
Mhe. Millya alieleza kuwa safari hizo zitafungua fursa mpya za kiuchumi kwa kurahisisha usafiri wa wageni, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ulaya kuja Tanzania, sambamba na kuwapa Watanzania urahisi zaidi wa kusafiri kwenda Ulaya kupitia mtandao mpana wa safari za Brussels Airlines.
 
Aidha, kuanzishwa kwa safari hizo kunatarajiwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii nchini ikiwemo Zanzibar, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire. Hatua hiyo pia itasaidia kuongeza mapato yatokanayo na utalii, kuongeza ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.
 
Mbali na sekta ya utalii, safari hizo zinatarajiwa kuimarisha biashara na uwekezaji kwa kuwezesha usafirishaji wa bidhaa na mizigo kati ya Tanzania na masoko ya Ulaya kwa haraka zaidi, hivyo kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa. Uwepo wa safari za moja kwa moja pia utaimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu muhimu cha biashara, utalii na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
 
Hafla ya uzinduzi huo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali mabalozi, watendaji wa sekta ya usafiri wa anga, utalii na biashara, pamoja na wadau wengine wa maendeleo, akiwemo Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Balozi wa Tanzania nchini Belgium Mhe. Jestas Nyamanga, Balozi wa Belgium nchini Tanzania Mhe. Peter Huyghebaert na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Lufthansa Bi. Julia Hilenbrand ambao kwa nyakati tofauti wameeleza matumaini yao kuwa kuanzishwa kwa safari hizo zitachangia kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania, Ubelgiji na Bara la Ulaya kwa ujumla.
Posted by MROKI On Thursday, June 04, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo