Naibu Waziri Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa akijibu maswali bungeni
jijini Dodoma wakati wa Kikao cha 50 cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania leo Juni 16, 2026.Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa (nyuma kulia) akiwa na Naibu Mawaziri wa Wizara mbalimbali wakati wa Kikao cha 50 cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo Juni 16, 2026.
**************
Serikali imesema utekelezaji wa miradi ya biashara ya
kaboni hasa kaboni ya buluu utakapokamilika na mauzo kufanyika, itanufaisha
jamii inayozunguka maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani.Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma
leo Juni 16, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Azan Mwinyi aliyetaka kufahamu ni
maeneo gani ya Ukanda wa Pwani yamenufaika na Blue Carbon.
Mhe. Kwagilwa alisema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya
Makamu wa Rais na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) imeendelea
kusajili miradi mbalimbali ya biashara ya kaboni nchini hususan kaboni ya buluu
inayofyonzwa na kuhifadhiwa na mazingira ya baharini na pwani kama vile misitu
ya mikoko na nyasi za bahari hivyo husaidia kupambana na mabadiliko ya
tabianchi na kuongeza kipato cha jamii za pwani.
Alitaja miradi iliyosajiliwa katika maeneo ya ukanda
wa pwani kuwa ni pamoja na Mradi wa Mimbiki uliopo Chalinze, Mradi wa Mikoko
Carbon Sink uliopo Mkinga, Mkuranga, Tanga Mjini na Pangani.
Miradi mingine ni Mradi wa Carbon for Farmers
uliopo mikoa ya Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara, Mradi wa Organic West
Composite Tanzania uliopo Mkuranga na Mradi wa Buyuni Redd+ Farm Carbon
uliopo Mkoa wa Pwani, ambayo yote ipo katika hatua za awali za utekelezaji.
Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Kwagilwa alibainisha kuwa
biashara ya bluu kaboni ni eneo la kipaumbele kwa nchi ambalo limewekewa
msisitizo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Serikali
kupitia Sera ya Uchumi wa Bluu ya mwaka 2023 pamoja na Mkakati wake wa utekelezaji,
imeweka kipaumbele cha kuanzisha miradi ya bluu kaboni na kuvutia wawekezaji
kuwekeza katika biashara hiyo, kwa lengo la kunufaisha jamii za pwani na
kuongeza pato la Taifa,” alisema.
Katika hatua nyingine Naibu
Waziri huyo ameeleza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na eneo kubwa la ukanda wa
pwani ya bahari lenye fursa kubwa ya kaboni ya buluu hivyo, Serikali imeanza
kutoa elimu ili wananchi watambue fursa hizo.
Alisema hayo wakati akijibu
swali la nyongeza la Mhe. Maryam aliyeuliza kuhusu mikakati ya Serikali katika
kutoa elimu ya buluu kaboni ili wananchi wanufaike hususan wanawake.
Akijibu
swali hilo, Mhe. Kwagilwa alisema eneo la bahari
linakadiriwa kufikia kilomita za mraba zaidi ya 60,000 na eneo la ukanda wa uchumi
wa bahari ni kilomita za mraba 223,000 wakati eneo la mikoko lina hekta 147,000
ambalo linafaa kwa jamii kulitumia kukuza uchumi.
“Kutokana na hali hiyo sisi
kama Serikali imetufanya kuanza kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya
habari na pia tumetoa elimu kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kule Zanzibar,
tunataka elimu ifikie hadi shuleni ili watambue fursa hizo za kaboni ya buluu,”
alisema.
Mhe. Kwagilwa alimalizia kwa
kusema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kushirikiana
taasisi za elimu kikiwemo Chuo Kikuu cha Zanzibar na wadau wanaotarajia
kuwekeza kwenye biashara ya kaboni ya buluu kwa kujisajili NCMC.



.jpg)
.jpg)



0 comments:
Post a Comment